Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ulanga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba moja kwa moja niende katika Hospitali yangu ya Wilaya ya Ulanga. Hospitali ya Ulanga hali yake ni mbaya sana kiasi kwamba haiendani na hali ya Mbunge kama ilivyo, Mbunge mahiri na machachari. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, katika Hospitali ya Wilaya ya Ulanga, watumishi ni wachache, yaani wachache kupindukia. Madaktari ni wachache, wataalam kama wa X- ray yuko mzee mmoja ambaye alishastaafu miaka mingi iliyopita ndiye tunamtumia huyo huyo kwa kumwajiri kwa mkataba. Pia ultrasound na yenyewe haina mtaalam, Serikali imejitahidi imenunua ultrasound mpya lakini hamna mtu wa kusoma. Hali hii imesababisha kumtafuta mtu kutoka Hospitali ya Saint Francis – Ifakara ambaye anapaswa kusafiri mpaka Ulanga kwa ajili ya kuja kusoma hivyo vipimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wodi zilizopo ni za tangu enzi za Mkoloni, na ni chache. Mheshimiwa Waziri naomba ujaribu kutembelea uone kwa kiasi gani Wilaya ya Ulanga tunavyopata tabu. Wagonjwa wanachanganywa, kwa mfano akinamama ambao wamefanyiwa operation wanaenda kulazwa wanachanganywa na wagonjwa wengine. Hali hii inapelekea hatari kwa magonjwa nyemelezi ambayo yanaweza yakasababishwa kutokana na vidonda vyao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, chumba cha upasuaji cha Hospitali ya Ulanga kina hali mbaya sana, kiasi cha kwamba kama ingekuwa Hospitali ya Private ingefungiwa. Chumba cha upasuaji hakina monitor matokeo yake Madaktari wanatumia uzoefu wao binafsi kama waganga wa kienyeji kwa ajili ya kuwafanyia operation. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Wilaya ya Ulanga mashuka ya wagonjwa yanafuliwa kwa mkono, kiasi cha kwamba inapelekea hatari kwa hawa wafanyakazi. Hebu fikirieni mashuka ya wagonjwa yanafuliwa kwa mkono, Mheshimiwa Waziri akienda kweli machozi yatamtoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Ulanga haina gari ya wagonjwa, gari iliyokuwepo niliyonunua mimi ambayo haiendani sawa na ukubwa wa Jimbo. Gari yenyewe ni haice, nimejitahidi nimenunua basi Serikali iseme jamani kijana wetu umejitahidi hata mniunge mkono muongeze lingine. Liko lingine ambalo nimelichukua najikongoja kulitengeneza sasa hivi mwaka mzima lakini nimeshindwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyakazi wa Hospitali ya Ulanga, uniform mwaka wa saba huu wanajinunulia wenyewe, hakuna uniform allowance, hebu fikirieni Maaskari wananunuliwa uniform, sehemu zingine wananunuliwa uniform, Ulanga pamoja na hali ngumu ya uchumi lakini wanajinunulia wenyewe, kwa hiyo naomba muwaunge mkono kwa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu dawa; Wilaya ya Ulanga, ndio inaongoza kwa wagonjwa wa kifafa duniani, dawa za ugonjwa wa kifafa zinatolewa bure Tanzania lakini cha ajabu dawa hizi Ulanga zinauzwa. Ukienda Hospitalini hazipo, lakini kwenye maduka ya private zipo. Kwa hiyo naomba mliangalie hili hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naomba nipingane kwa nguvu zote kutokana na maoni ya Kamati wanasema huduma za NHIF ziboreshwe ili mashirika ya umma yajiunge. Wewe ni shahidi ili nyumba uimalizie vizuri inatakiwa uhamie ndani ndiyo utamalizia, ukisema nisubiri niimalize hutoweza kuhamia. Kwa hiyo tunataka, kwa sababu NHIF inaendeshwa kwa michango, haya Mashirika ya Umma yaingie, yakishaingia michango yao ndiyo itakayoboresha hizo huduma. Kwa sababu gani tunasema huduma bora, NHIF ndiyo yenye vituo vingi Tanzania, hakuna shirika lingine la bima ya afya ambalo linatoa huduma katika vituo vingi, NHIF inatoa huduma bila kikomo. Shirika gani la bima ya afya ambalo linatoa huduma bila kikomo tuseme tusubiri huduma ziboreshwe? NHIF ina wanufaika wengi kuliko bima za afya zingine, tunataka huduma zipi ndizo ziboreshwe? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leo yangu ni hayo machache kwa ajili ya kutunza muda. Ahsante sana na naunga mkono hoja.