Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Mussa Bakari Mbarouk

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijaalia afya njema na kuniwezesha kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, afya ndiyo utajiri mkubwa kuliko utajiri wowote na hospitali, vituo vya afya, zahanati hizi zote ndizo ambazo tunaweza kuzisema garages za binadamu. Lazima pawepo na vifaa vya aina zote (apparatus) ili ziweze kuwarahisishia utendaji kazi madaktari na wahudumu wetu wa afya (nurses) ambao kwa kweli wanafanya kazi katika mazingira magumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu changamoto za vituo vya afya; katika maeneo ya vijijini kuna kero ya kufunga vituo vya afya na zahanati saa 8:30 mchana, hili ni tatizo. Mfano katika Jimbo langu la Tanga Mjini, vituo vifuatavyo ni miongoni mwao; Kituo cha Afya Pande (Kiomoni), Kirare, Manungu, Chongoleani, Mabokweni, Tongoni na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri/ombi langu ni kuwa hivi vituo vikifanya kazi 24 hours kuna tatizo gani? Naishauri Serikali yangu sikivu iwatumie madaktari 258 waliokuwa waende kufanya kazi nchini Kenya wakati wa mgomo na ambao Mheshimiwa Rais Magufuli ameshatangaza kuwaajiri, tupatiwe madaktari 70 kati yao waende katika vituo vya afya na zahanati zetu za Jiji la Tanga pamoja na vitongoji na viunga vilivyopo maeneo ya vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jiji la Tanga lilianzisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Tanga ili kuweza kupunguza msongamano katika Hospitali ya Mkoa ya Bombo. Halmashauri ilishaanzisha ujenzi wa Administration Block (Jengo la Utawala) kwa gharama ya shilingi milioni 400 katika mwaka 2013/2014. Kwa sasa mpango wa Halmashauri ya Tanga 2017/2018 tumetenga shilingi 300,000,000.00 ili kujenga jengo la OPD (Out Patient Department).

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu naiomba Serikali iunge mkono juhudi za Jiji la Tanga kwa kuipatia fedha takribani bilioni 1.2 ili iweze kuendeleza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya katika ujenzi wa wodi za kulaza wagonjwa, theatre, sehemu za tiba ya macho, moyo, mifupa na kadhalika; lakini pia gari la wagonjwa (ambulance). Halmashauri ya Jiji la Tanga kwa kushirikiana na Wizara ya Afya tukifanikiwa kuikamilisha Tanga District Hospital tutasaidia kuboresha afya za wananchi wa Jiji la Tanga na Watanzania lakini pia tutaipunguzia Bombo Regional Hospital msongamano wa wagonjwa wanaotoka Wilaya zote nane na Halmashauri tisa za Mkoa wa Tanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ajira za madaktari/ wahudumu, naomba pia wahudumu (nurses) wengi wanaosoma katika Vituo vya Hospitali Teule za Tanga, Matc na Eckenforde Nursing Training waajiriwe katika hospitali yetu ya Wilaya tunayoitarajia pamoja na vituo vyetu vya afya na zahanati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la dawa MSD, medicine supply chain iwekwe wazi. Naomba kwa kuwa Jiji la Tanga tayari tunao mpango na utekelezaji wa Hospitali ya Wilaya, mgao wa dawa za MSD ungepelekwa katika zahanati na vituo vya afya vilivyopo (ama msaada au kwa kununua ili kupunguza upungufu wa dawa katika Jiji la Tanga).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hospitali ya Mkoa ya Bombo Hospital, naiomba Serikali (Wizara) kuingilia Hospitali ya Mkoa wa Tanga (Bombo Regional Hospital) ambayo imepandishwa hadhi na kuwa Hospitali ya Rufaa lakini haina hadhi hiyo kwa kuwa haina:-

(i) Madaktari Bingwa wa kutosha;
(ii) Vifaa tiba vya kutosha (oxygen machine, x-ray, ultra sound, CT Scan;
(iii) Intensive Care Unit ina mapungufu mengi;
(iv) Barabara za ndani za hospitali mbovu kupita kiasi;
(v) Lift ya Bombo imekufa zaidi ya miezi 36 iliyopita (paundi 126,000 zinahitajika); na
(vi) Gari za wagonjwa mbovu inayofanya kazi ni moja tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri na maombi yangu kwa Serikali (Wizara) ni kwamba Serikali iangalie kwa jicho la huruma Hospitali hii ya Mkoa ya Bombo kwa mapungufu yote kuanzia (i) – (vi) na namkumbusha Mheshimiwa Ummy (Waziri) kwamba charity begins at home.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu huduma za ustawi wa jamii, ukurasa wa 57; nawazungumzia walemavu wa akili. Serikali itenge fedha kila Halmashauri ili kuwepo kitengo cha kuwatunza walemavu wa akili (vichaa) ili kuwapatia nguo, kuwakata nywele, kucha na kuwatibu kwa kufuatilia chanzo cha maradhi yao, kama ni matumizi ya dawa za kulevya, mtindio wa akili na kadhalika, watibiwe kwa kuwa nao ni Watanzania wenzetu. Inatia aibu kuwaona vichaa watu wazima wanatembea uchi mitaani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma za watoto, wajawazito na wazee; naiomba Serikali iangalie katika eneo hili kwa sababu kuna maneno kuliko vitendo. Akina mama, wazee na watoto wanalipa, naomba Wizara itoe vifaa vya kujifungulia na dawa za wazee bure.