Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ZAINABU N. MWAMWINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kuipongeza Serikali yangu kwa jitihada inazoendelea kuzifanya katika kuboresha sekta ya afya nchini. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa utendaji wake mzuri uliotukuka kwa kuisimamia vizuri Ilani ya CCM. Nampongeza pia Mheshimiwa Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa pamoja na Mawaziri wote wakishirikiana na watendaji, wanafanya na kutekeleza majukumu yao kwa weledi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu na Naibu wake Dkt. Hamisi Kigwangalla nawapongeza sana kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kutekeleza majukumu yao katika Wizara hii, hongereni sana.
Hata hivyo Watanzania wengi zaidi ya nusu ya wakazi wote nchini wanaishi vijijini. Hivyo basi tunapoimarisha huduma za afya katika maeneo vijijini tutawanusuru maisha ya watu wengi ambao ndio nguvu kazi ya Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kuangali ikama ya watumishi wa sekta ya afya kwa lengo la kuondoa mlundikano wa madaktari na wahudumu wengine wa afya katika miji mikubwa na kuwapeleka maeneo ya vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna zahanati ambazo zikijengewa uwezo kama vile wa vifaa, majengo na wataalam zitapunguza mlundikano katika hospitali za Wilaya na Mikoa. Moja ya zahanati hizo ni zahanati ya Ulanga iliyoko Wilaya ya Iringa, Mkoa wa Iringa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba Mheshimiwa Waziri binti yangu mchapakazi, mbunifu na msikivu, uje kuitembelea zahanati hii iliyoko Kalenga ambayo ipo katika hali mbaya sana. Uchakavu wa majengo, miundombinu kama nyumba za watumishi, hata chumba cha wazazi, inasikitisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nimalizie kwa kuipongeza tena Wizara kwa kazi kubwa ikiwemo kuikarabati Hospitali ya Mkoa wa Iringa na kuipandisha hadhi kuwa Hospitali ya Rufaa, ila nashauri tena Wizara ikae na Wizara ya Mambo ya Ndani ili kurahisisha upanuzi wa hospitali hiyo kwa kuondoa Gereza la Iringa Mjini katika eneo lilipo hivi sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja.