Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Riziki Shahari Mngwali

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. RIZIKI S. MNGWALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuwa nilipata dakika chache za kuchangia kwa kuzungumza, hivyo, maelezo haya ni nyongeza ya mchango wangu huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ndiyo Taifa lenyewe. Bila ya afya, bila mazingira mazuri ya wazee wetu na watoto wetu, bila mfumo nzuri wa jinsia - mahusiano ya wanawake na wanaume maendeleo ya jamii hayatapatikana. Kwa masikitiko makubwa Wizara hii imekumbwa na tatizo sugu la utendaji wa Serikali ya CCM tatizo la kutopeleka fedha zinazoidhinishwa na Bunge kwa Wizara na Taasisi husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa ya Kamati ya kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii inasema katika ukurasa wa 19 kuwa, bajeti ya Wizara hii kwa mwaka 2016/2017 haijatekelezeka kwa asilimia 60%. Hii ni kwa mujibu wa takwimu za mwaka 30 Machi, 2017. Hii ni kucheza na uhai na maisha ya Watanzania/wananchi wetu. Katika mjadala wa bajeti kwa mwaka 2016/2017, nilishauri kuhusu kubadili mfumo/utaratibu/mchakato wa bajeti nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchakato wa bajeti unafanyika kama ni jambo la kawaida tu kufanyika miaka nenda rudi matatizo na kasoro zile zile zinaendelea kujitokeza lakini Serikali haioneshi dalili za kubadilika ili kuwa na mchakato wa bajeti inayotekelezeka na unaoweza kuleta tija katika jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda kuishauri Wizara na Serikali kwa ujumla kulifanyia kazi kwa umuhimu wa kipekee ni takwimu kuhusiana na upungufu wa wataalam wa afya zilizotolewa na hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani kwenye ukurasa wa saba. Picha hii inatisha sana na si jambo la kupuuzia hata kidogo. Tukibadili mchakato wa bajeti na kuufanya kuwa ‘integrated’ itasaidia kuwa na vipaumbele vichache vya Taifa badala ya huu utaratibu wa sasa unaokuwa na vipaumbele vingi kwa kila Wizara, matokeo yake ndiyo hili tatizo sugu la bajeti zisizotekelezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, intergrated budget process itasaidia kuondoa tofauti kubwa za kimaendeleo na utoaji huduma za msingi za jamii. Kujenga barabara za kisasa, flyovers na usafiri wa mwendo kasi katika Jiji la Dar es Salaam, kwa kigezo cha mchango wake katika pato la Taifa ni sawa lakini muhimu vilevile kuangalia spill-over effects zake kwa maeneo mengine na haki ya Taifa. Maeneo mengi ya vijijini likiwemo Jimbo langu la Mafia yanaendelea kubaki nyuma katika maendeleo na upatikanaji wa huduma muhimu zikiwemo za afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Wilaya ya Mafia ina matatizo lukuki kuanzia wafanyakazi mpaka vifaa, inafikia wakati Nesi mmoja anapangiwa wodi mbili. Uwepo wa hospitali iliyo kamili/inayojitosheleza ni muhimu sana kwa Wilaya ya Mafia kutokana na jiografia yake kuwa kisiwani. Wilaya ya Mafia haina usafiri wa kuvuka kwenda Dar es Salaam au Mkuranga ili kupata huduma kama za X-ray au rufaa husika. Namwomba Mheshimiwa Waziri aiangalie Hospitali ya Wilaya ya Mafia kwa jicho la kipekee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hotuba ya Kambi ya Upinzani na taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge. Hata hivyo, nawapongeza sana Waziri na Naibu wake kwa uwajibikaji wao mahiri. Ni matumaini yangu Serikali itawapa mazingira mazuri ya kufanya kazi hii adhimu. Nashukuru sana.