Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Muhammed Amour Muhammed

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Bumbwini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kuniwezesha kuwa hai, mzima na kunipatia nguvu ya kuweza kuchangia mada ambayo ipo hewani sasa. Pia napenda kutoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Spika kwa namna ambavyo analiongoza Bunge hili kwa upendo na umahiri pia na uvumilivu mkubwa anaouonyesha ndani ya Bunge hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia mambo sita yafuatayo:-

Moja, UKIMWI; Taifa letu sasa linahujumika kwa maradhi haya na wengi wao ni vijana ambao ndio manpowers ya Taifa. Naomba hapa Wizara husika iendelee kutoa elimu ndani ya nchi yetu namna unavyoambukizwa bila ya kuona haya, hali inatisha. Kwa upande mwingine ni vyema hizo dawa za ARV zikawekwa maeneo mengi zaidi tena kwa waziwazi pasi na kuficha.

Pili, malaria; nikienda kwenye malaria, haya ni maradhi bado yapo ijapokuwa yamepunguka. Jitihada za makusudi za kuyamaliza maradhi haya zinahitajika. Malaria ni maradhi ambayo huenezwa zaidi na mbu, mbu hawa kama tukiweka mikakati ya kusafisha maeneo, kupiga dawa za kuulia wadudu (insecticides) nchi nzima hasa kwenye mitaro ya maji machafu utapungua ama kwisha kabisa. Pia malaria ina kina, ni vyema tukaangalia zaidi kuwapatia watu wetu chanjo ya malaria.

Tatu, Madaktari na Wahudumu wengine wa Afya; ni vyema wakaongezewa mishahara kwani kazi ambazo wanafanya ni kubwa sana na maslahi bado ni duni kwa watumishi hawa. Nikiendelea kuchangia mada hii ni kwamba kwenye hospitali zetu na vituo vya afya bado watumishi ni haba, hawatoshi. Niombe Serikali kwa heshima zote iongeze watumishi katika sekta hii.

Nne, vituo vya afya; naomba Serikali iangalie tena upya namna ya kuboresha vituo vya afya hasa vilivyoko vijijini kwani havitoshi kulingana na mahitaji.

Tano, vifaa vya kisasa; hapa ndipo penye matatizo makubwa. Hospitali zetu hasa za Serikali hazina vifaa vya kisasa vya kutosha. Niiombe Serikali kwa heshima zote iliangalie suala hili kwa huruma sana, tunahitaji X-ray, Ultra- sound, CT Scan na vifaa vingine maana ni vichache sana.

Sita, maradhi yasiyo ya kuambukiza. Maradhi haya kama pressure, sukari yanazidi kuendelea kuwaumiza watu wetu. Kwa heshima zote niiombe Serikali/Wizara husika itoe elimu ya kutosha juu ya kujilinda na maradhi haya nchi nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.