Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sikonge
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii muhimu na adhimu kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema ya uhai na uzima. Nikushukuru wewe kwa kuniruhusu na mimi nichangie ingawa kwa ufupi mapambano ya UKIMWI pamoja na kuendelea ndani ya nchi yetu lakini inaonekana bado UKIMWI unaongezeka pamoja na maambukizi mapya na kama juhudi za makusudi hazitachukuliwa basi Taifa letu litafika pabaya sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivi sasa UKIMWI umekuwa uko sirini sana kiasi ambacho watu wengi wamekuwa na matumaini makubwa kwamba UKIMWI umepungua kwa style za watu zilivyo. Watu ambao wanaishi na virusi vya UKIMWI si rahisi kuwatambua kama hajajieleza mwenyewe. Hii inatokana na kuitikia wito wa kujiunga na vituo vya dawa za ARV, kwa hiyo, watu wengi kwa kupungua athari za kuonekana moja kwa moja wanadhani UKIMWI umepungua. Kwa hiyo, ushauri wangu, mikakati na juhudi ziendelee kuelimisha Watanzania kwamba UKIMWI upo na bado unaua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wataalam wa UKIMWI wametoa taarifa kwamba Mkoa wa Njombe unaongoza kwa UKIMWI ambao una 14.8% hii ni asilimia kubwa na ya kutisha. Naomba Serikali ifanye utafiti ni jambo gani linalosababisha maambukizi makubwa kiasi hiki katika Mkoa huu, tatizo lijulikane, itolewe elimu ya uhakika kuondoa tatizo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumzie kuhusu wazee. Tunafahamu fika kwamba wazee wa sasa ndio vijana wa juzi na jana ambao walijituma kwa utumishi uliotukuka na mafanikio ya utumishi wao mwema ndiyo uliolifikisha Taifa letu hapa lilipo. Hivyo, naishauri Serikali kutokuwasahau na kuwadharau wazee ambao ndiyo waliokuwa dira ya Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kusikitisha ni kwamba, wazee hawapati huduma inavyopasa na badala yake wazee wanaonekana kama hawakuwa na mchango wowote katika Taifa hili. Mfano, katika huduma za matibabu, wazee wamekuwa wakisumbuka kana kwamba hawastahili kupatiwa huduma hii. Wamekuwa wakitozwa malipo makubwa ambayo hawayamudu lakini ni haki ambayo imeidhinishwa na Serikali kupatiwa. Naishauri Serikali kuweka kipaumbele juu ya kuwajali wazee kwa kuwapatia huduma wanazostahili. Serikali ina nia na dhamira thabiti juu ya wazee ila inaonekana changamoto hii inayowakumba ni utendaji mbovu usiojali mchango wa wazee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia hoja yangu, napenda kugusia angalau kidogo suala la mazoezi ya viungo kwa jamii. Mazoezi ni jambo muhimu sana kwa afya ya mwanadamu na michezo ni sehemu ya mazoezi. Kwa hivyo, michezo ni muhimu sana kwa maendeleo ya jamii na kiuchumi na hasa katika kuimarisha miili yetu kiafya na kuwa wakakamavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu imekumbwa na magonjwa mengi sana ambayo kama tungekuwa makini na mazoezi tusingeathiriwa sana na magonjwa haya. Mfano wa magonjwa hayo ni kama vile kisukari, moyo na kadhalika. Magonjwa haya kwa ujumla wake yanaitwa magonjwa sugu yasiyoambukiza na yanayogharimu pesa nyingi za wananchi na Serikali. Naishauri Serikali na Wizara ya Afya kuhamasisha jamii kuhusu suala zima la kufanya mazoezi na kutoa misaada pale inapobidi ili kuendeleza mazoezi.