Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Ummy Ally Mwalimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. Pia niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote, waliochangia hoja yangu ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa mwaka 2017/2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nimshukuru sana Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Mheshimiwa Peter Serukamba ambaye amewasilisha Maoni na Ushauri wa Kamati kuhusu utekelezaji wa bajeti yetu. Pia niishukuru sana Kamati kwa sababu wamechambua mapendekezo yetu na tunawashukuru Kambi ya Upinzani kwa hotuba yao ambayo imewasilishwa na Mheshimiwa Ester Bulaya, tunapokea pia maoni na ushauri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa maoni na ushauri wao na niseme tu kwamba tumepokea hoja nyingi na kwa sababu ya muda sitaweza kupitia book lote hili kumjibu Mbunge mmoja mmoja, lakini katika hatua hii niseme tumepokea maoni na ushauri wenu. Kubwa ambalo limetupa faraja wote Bunge hili tumeungana tunakubaliana kwamba afya ni maendeleo, afya ni elimu, afya ni kilimo, afya ni viwanda, afya ni ulinzi, afya ni uchumi, kwa hiyo, tunawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, Waheshimiwa Wabunge waliochangia hoja yangu ni 164. Waliochangia kwa kuzungumza ni 61 na kwa maandishi ni 99 na wakati wa mjadala wa Mheshimiwa Waziri Mkuu Waheshimiwa Wabunge wanne pia wamechangia.

Mheshmiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda sitawataja, lakini nitaomba sasa nitoe maeneo makubwa ambayo yameelezwa na Kamati na vile vile yameelezwa na Kambi ya Upinzani pamoja na Waheshimiwa Wabunge. Kabla ya kuondoka katika Bunge hili la bajeti, tutawasilisha majibu ya hoja zote. Nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa ufafanuzi alioutoa katika baadhi ya hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitajikita katika mambo makubwa matano. Jambo la kwanza nitazungumzia rasilimali fedha kwa ajili ya sekta ya afya; pili, nitazungumzia upatikanaji wa dawa; tatu, nitazungumzia afya ya uzazi na motto; na nne nitazungumzia suala la kuthibiti vifo vya watoto wadogo na pia nitazungumzia kuwawezesha wanawake kiuchumi na masuala ya Sheria ya Ndoa ikiwemo sheria zinazolinda haki ya mtoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo limetolewa maoni na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, ni kuhusu rasilimali fedha ambazo zimetengwa kwa ajili ya Sekta ya Afya, kwamba ni ndogo ni chache na haziakisi hali halisi ya changamoto zilizopo katika Sekta ya Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie hali halisi ya ukusanyaji wa mapato katika nchi yetu. Pili, ningetaka kuwatahadharisha Waheshimiwa Wabunge watofautishe Bajeti ya Wizara ya Afya na Bajeti ya Sekta ya Afya. Kuna mambo mawili niyaweke wazi. Kwa mfumo wa Nchi yetu ambao Mheshimiwa Simbachawene ameuongelea, hela kwa ajili ya kutatua changamoto za sekta ya afya zipo chini ya Fungu 52, lakini pia tutazikuta chini ya Fungu 56 kwa ajili ya Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa pamoja na halmashauri. Kwa hiyo, kuna Mheshimiwa amesema bajeti ya sekta ya afya, ni asilimia tatu, si sahihi. Bajeti iliyotengwa kwa ajili ya Sekta ya Afya ni trilioni 2.2. Nikichukua fedha za TAMISEMI na fedha zilizotengwa chini ya Wizara yangu ni trilioni 2.2.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuwapitisha Waheshimiwa Wabunge wakaangalia. Mwaka 2015/2016, Sekta ya Afya ilitengewa shilingi trilioni 1.8; mwaka 2016/2017, Sekta ya Afya imetengewa trilioni 1.9, mwaka 2017/2018 Sekta ya Afya imetengewa shilingi trilioni 2.2. Nafurahi kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba, kati ya vipaumbele vitatu vya Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, sekta ya afya ni ya tatu baada ya miundombinu inafuatia elimu halafu inakuja sekta ya afya. Sisemi kwamba fedha hizi zinatosha, lakini Serikali inajitahidi kwa dhahiri kuonesha kwamba afya za Watanzania ni kipaumbele na ni jambo ambalo tumeliahidi katika Ilani ya Uchaguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija sasa nikiangalia Bajeti ya Wizara ya Afya, Fungu 52, unaiona kabisa dhamira ya dhati ya Serikali ya kuendelea kuwekeza katika afya za Watanzania. 2014/2015, bajeti ya Wizara ya Afya ilikuwa ni bilioni 713; mwaka 2015/2016 bilioni 780; na sasa hivi kwa ajili tu ya Fungu 52 na nimechukua tu, nimeondoa maeneo mengine sasa hivi (2016/2017) inaenda kwenye bilioni 796 na jana nimeomba trilioni 1.1 kwa ajili ya Vote 52. Kwa hiyo, jambo ambalo nataka kuwasisitiza Waheshimiwa Wabunge, ni kweli tumeridhia Azimio la Abuja la kutenga asilimia 15 kwa ajili ya Sekta ya Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lile ni azimio lazima tuangalie pia vipaumbele vingine vinavyoikabili nchi yetu. Nataka kuwathibitishia Waheshimiwa Wabunge, tutaendelea kushauriana na wenzetu wa Wizara ya Fedha kuhakikisha kwamba wanatoa kipaumbele kwa ajili ya sekta ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo limeongelewa pia na Kamati ya Kudumu ya Bunge pamoja na Kambi Rasmi ya Upinzani pamoja na Waheshimiwa Wabunge Lucy Owenya, Suzan Lyimo na rafiki yangu mpenzi Azza Hilary kwamba tunategemea sana fedha za wafadhili kwa ajili ya kuendesha kutatua changamoto za sekta ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuwathibitishia Waheshimiwa Wabunge tumeanza kuwekeza, tumeanza kutumia rasilimali zetu za ndani kwa ajili ya kutatua changamoto za sekta ya afya. Natoa kutoa mfano, mwaka 2014/2015 fedha za ndani kwa ajili ya bajeti ya sekta ya afya zilikuwa bilioni 54; mwaka 2015/2016 bilioni 66; mwaka 2016/ 2017 na hizi ni fedha za maendeleo sizungumzii OC; zimeenda mpaka bilioni 320 na mkiangalia fedha za ndani ambazo sasa tunaomba kwa ajili ya kuetekeleza miradi ya maendeleo ni takribani bilioni 336.

Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, ongezeko hili linaonesha ni jinsi gani Serikali inatekeleza ushauri wa Waheshimiwa Wabunge, kwamba ni lazima tutumie rasilimali za ndani kwa ajili ya kutatua changamoto za sekta ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubali katika miradi kwa mfano ya UKIMWI, ukoma, malaria na kifua kikuu asilimia kubwa ya fedha zinatoka kwa wafadhili, lakini kwa mfano dawa za UKIMWI, tumeanza kutenga rasilimali zetu za ndani kwa ajili ya masuala ya UKIMWI. Pia katika masuala ya uzazi wa mpango kwa mara ya kwanza, tumetenga bilioni 14, fedha za ndani kwa ajili ya masuala ya uzazi wa mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nihitimishe hoja hii kwa kusema kwamba zipo chngamoto za rasilimali fedha, kwa sababu pia zipo changamoto nyingi za kimaendeleo katika nchi yetu. Nataka kwathibitishia dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Rais ya kuwekeza katika sekta ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ni faraja kwetu, kwa mara ya kwanza tumekuwa tukipata fedha za kutekeleza miradi, nitatoa mfano wa fedha za dawa. Mwaka 2015/2016 fedha za dawa zilizotolewa ilikuwa ni bilioni 24 tu, nchi nzima iliendeshwa kwa fedha za dawa kwa bilioni 24 tu. Leo ninapoongea jana nilisema ni bilioni 112 lakini tumepata bilioni 20. Kwa hiyo sasa hivi tunaongea bilioni 132 ambazo zimetolewa na Hazina kwa ajili ya fedha za dawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala ambalo limeongelewa na Waheshimiwa Wabunge wengi pamoja na Kamati ya Kudumu ya Maendeleo ya Jamii, kuhusu upatikanaji wa dawa. Tunapokea pongezi za Waheshimiwa Wabunge, kwamba tumeboresha upatikanaji wa fedha za dawa, lakini pia tumepokea changamoto kwamba kupatikana kwa fedha za dawa sio kupatikana kwa dawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe ufafanuzi hapa. Katika Hotuba yangu, nimezungumzia upatikanaji wa dawa katika Bohari ya Dawa ni asilimi 81 nimetumia vigezo gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi haiwezi kuwa na dawa zaidi ya; tukasema bohari ya dawa ina dawa 3000, 4000 tunaangalia tunaita dawa muhimu zaidi (Essential Medicine) ziko 135. Kwa hiyo, tunaposema upatikanaji wa dawa ni asilimia 81 maana yake katika kila zile dawa 135 asilimia 81 ya dawa hizo zinapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka kuwathibitishia Waheshimiwa Wabunge kwamba, hizi takwimu sio za dawa 2,000, dawa 3,000, ni dawa 135 ambazo ndizo za kuokoa maisha. Hata hivyo, sasa tumeenda mbali zaidi, kutokana na maoni na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge, mlitushauri tusiishie tu katika Bohari ya Dawa, ndiyo maana katika bajeti yangu kwa mara ya kwanza tumeenda mpaka katika mikoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu ambazo nimeziweka katika jedwali la pili, tumeletewa na Waganga Wakuu wa Mikoa na Waganga Wakuu wa Wilaya. Katika hotuba yangu tumeeleza tunaendelea kuboresha mfumo ili tujiridhishe kwamba, takwimu hizi tulizoletewa ni sahihi. Kwa hiyo, nakubali zipo changamoto za dawa kuwepo katika vituo vya afya na katika zahanati. Changamoto ya kwanza, maoteo ya mahitaji yanaletwa kwa kuchelewa. Nitumie fursa hii kuzitaka halmashauri zote kuleta maoteo ya mahitaji ya dawa kama Kanuni ya Sheria ya Manunuzi inavyotaka. Wanatakiwa watuletee by terehe 30 Januari ya mwaka huo kusudi tuweze kuisaidia MSD kununua dawa kwa wakati.
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kaka yangu Mheshimiwa Bobali aliniambia kama haya majedwali yanatofautiana; nadhani hajanielewa. Tutofautishe fedha za dawa na upatikanaji wa dawa. Mheshimiwa Mwenyekiti ni Mwanasheria, moja ya sifa kubwa ya Wanasheria ni kusoma kila kitu na kukitafakari. Kwa hiyo, nimeisoma hotuba zaidi ya mara 10 siletewi. Kati ya jambo ambalo labda Watumishi wa Wizara ya Afya wananichukia ni kwa sababu, nasoma kila kitu, niko tayari hata nirudishe mara 10. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimejifunza kwako wakati nafanya internship yeye alikuwa ndio Mwanasheria Mkuu wa Serikali, lakini pia, nimejifunza kwake wakati ni Mwenyekiti wa Kamati Namba Moja, Kamati ya Kuandika Katiba inayopendekezwa. Kwa hiyo, wanasheria tunasoma, hatuletewi tu ukapitisha. Hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefurahi sana Mheshimiwa Sannda, shemeji yangu, amezungumzia tatizo la prescription. Kwamba, dawa zipo, lakini saa nyingine wataalam wetu badala ya kuandika dawa zilizopo katika kituo anaamua kuandika dawa pengine zilizo katika duka lake nje ya hospitali, kwa hiyo, hili tutalisimamia. Kwenye kuandika dawa wanatakiwa watu waandikiwe dawa zile ambazo ni dawa muhimu zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kuwafahamisha Waheshimiwa Wabunge, dawa zitapatikana kwa sababu tayari tumeingia mikataba mitano na wazalishaji wa dawa. Kwa hiyo, dawa zitatoka moja kwa moja kwa wazalishaji, maana yake zitapatikana kwa urahisi. Nataka kuwathibitishia Waheshimiwa Wabunge na mimi siogopi kuwajibika, nilisema nataka kupimwa kwa mambo ikiwemo upatikanaji wa dawa na hili nataka kuwathibitishia, dawa 135 zitapatikana kwa angalau asilimia 95, hizo nataka kuwathibitishia Waheshimiwa Wabunge, lakini kama kuna mtu atataka dawa ambayo ni brand, si dawa zile 135, hilo siwezi kumthibitishia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliahidi kuboresha upatikanaji wa dawa Ocean Road. Sasa hivi Ocean Road ina dawa kutoka asilimia tatu mpaka asilimia 60. Dawa za Saratani ya mlango wa kizazi ni mpaka asilimia 60. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kulitolea ufafanuzi ni; Mheshimiwa Zedi, tumepokea ushauri wako, lakini taarifa zetu kidogo zinakinzana. Nataka kukuahidi kwamba tutaendelea kufanyia kazi. Nitoe ufafanuzi kwa Waheshimiwa Wabunge, tumeshatoa maelekezo kwa MSD suala la OS (Out of Stock), tumemwelekeza MSD kama umeombwa upeleke dawa ndani ya saa 24 kama hiyo dawa huna, umwambie halmashauri hiyo dawa sina kwa hiyo, nakupa kibali ukanunue kwa mshitiri mwingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitoe rai kwa Waheshimiwa Wabunge, halmashauri zetu zianze kuwatambua washitiri (Suppliers) kwamba, kama MSD hana na una hela yako, akupe OS ndani ya 24 hours kusudi mkanunue dawa maeneo mengine. Nawathibitishia dawa zitapatikana na niko tayari kuwathibitishia Waheshimiwa Wabunge hili suala linawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Bulembo, Mheshimiwa Umbulla na Kambi ya Upinzani mmezungumzia kuboresha Bohari ya Dawa. Kama nilivyosema hayo mabadiliko ndiyo tumeanza na kubwa kwa kweli sasa hivi, nashukuru Waheshimiwa Wabunge mmekubali, si fedha ni mifumo. Hii mifumo ndio tunahangaika nayo ikiwemo mifumo ya ugavi na usambazaji wa dawa. Kwa hiyo, Mungu akijalia, nikija kwenye bajeti nyingine tutakuja na takwimu mpaka za zahanati. Tutakuja na takwimu za dawa mpaka katika ngazi ya vituo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, limezungumzwa kwa hisia kubwa suala la kuhusu kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi. Walioongea hili ni Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kambi Rasmi ya Upinzani, Mheshimiwa Risala, Mheshimiwa Moshi, Mheshimiwa Mgeni, Mheshimiwa dada yangu Amina Makilagi, Mdogo wangu Mheshimiwa Neema Mgaya, Mheshimiwa Ester Mahawe, Mheshimiwa Bukwimba, Mama yetu Mheshimiwa Mama Salma Kikwete na Mheshimiwa Kemilembe. Tunapokea maoni yote kuhusu kuboresha jitihada ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe ufafanuzi mmoja; nakubali kwamba vifo vitokanavyo na uzazi bado ni tatizo katika nchi yetu. Naomba niseme, siyo kwamba tumejikwaa wapi? Wala siko hapa kubisha kuhusu takwimu; kwa sababu, ukiangalia sensa limekuwa ni jambo ambalo kidogo limeshtua watu kwa sababu, sensa ya mwaka 2012 ilikuwa inaonesha vifo vya akinamama wajawazito ni 430 katika kila vizazi hai laki moja, lakini takwimu za 2015/2016 ndiyo zinatupa 556.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa Waziri mwenye dhamana, mama, mwanamke, nikisema takwimu hizi sizikubali nitakuwa siwatendei haki Waheshimiwa Wabunge, siwatendei haki wanawake wenzangu wa Tanzania. Nataka kuwathibitishia, ndiyo maana jana nilisema ukiniuliza Waziri wa Afya, Bajeti hii inajibu kero gani? Kama Ilani ya Uchaguzi ya CCM inavyotuelekeza tupunguze vifo; bajeti hii inajibu kupunguza vifo vya akinamama wajawazito. Tumeonesha, kwanza tumewekeza katika huduma za uzazi wa mpango. Kwa sababu wataalam wanasema, uzazi wa mpango unaweza kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa asilimia 30.

Waheshimiwa Wabunge, niwape changamoto, tunapofanya mikutano katika Majimbo yetu, tuhimize masuala ya uzazi wa mpango. Mheshimiwa Shally Raymond umeongea vizuri kwamba, sasa hivi bado kiwango cha uzazi Tanzania ni asilimia 2.7, I mean population growth; na mwanamke wa Tanzania sasa hivi anazaa watoto kati ya watano mpaka sita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tena nyie watani wangu Wasukuma tena, ndiyo kidogo kule Kanda ya Ziwa matumizi ya uzazi wa mpango hayako vizuri. Nataka kuwaambia, zama… (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaona Wasukuma watani zangu. Nataka kuwaambia kwamba zama zimebadilika. Sasa hivi ukizaa hata watoto wawili, watatu na tumeboresha huduma za chanjo, watoto wale wanaishi. Kwa hiyo, zile zama za kwamba lazima mtu azae watoto 10, 12, lakini tuangalie pia, hao watoto utaweza? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka kukuthibitishia jambo la pili ambalo tutalifanya sambamba na kuimarisha huduma za uzazi wa mpango, tutaimarisha huduma za akinamama wakati wa ujauzito. Ni kweli, unaweza ukaenda katika Kituo cha Afya ukakuta mama mjamzito hapimwi hata wingi wa damu, hapimwi protini, hapimwi hata kama pressure iko juu au haiko juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Simbachawene hayupo, lakini nitoe maelekezo kwa Waganga Wakuu wa Wilaya na Mikoa, hufai kuwa Mganga Mkuu wa Wilaya na Mkoa kama zahanati yako inakosa hata mashine ya kupimia BP kwa mwanamke mjamzito. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kitu wataalam wanaita albu stick kwa ajili ya kupima mkojo kwa akinamama wajawazito kama protini ni nyingi. Stick 50 zinauzwa sh. 9,000/= tu, DMO unasubiri Mheshimiwa Waziri Simbachawene akuletee sh. 9,000/= kwa ajili ya kununua vipimo vya kupima protini kwa akinamama wajawazito! Kwa hiyo, kati ya eneo ambalo nitakuwa mkali ni suala la huduma za wajawazito wakati wanapohitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili namshukuru sana Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan; yeye amekuwa ndio nguzo yangu, ndio chachu yangu na amekuwa akinipa moyo wa kuendelea kupambana, kwa sababu mimi na yeye na bahati nzuri tulipita wote kuomba kura, eneo ambalo tunataka kukumbukwa na wanawake wa Tanzania ni katika afya ya uzazi na mtoto na hili tutaweza kulifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti hii tumeonesha kwamba tutajenga Benki za Damu tano. Haijawahi kutokea katika bajeti ya Wizara ya Afya. Benki za Damu katika mikoa mitano. Tumeonesha Manyara, tutajenga Katavi, tutajenga Rukwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine katika bajeti hii, jana nimeeleza kwa uchungu mkubwa, kwa mara ya kwanza tunatenga fedha zetu za ndani kwa ajili ya huduma za msingi za uzazi za dharura (BIMOC). Kwa hiyo, sasa hivi na ninarudia tena, Waheshimiwa Wabunge nataka muwe mashahidi, hakuna mwanamke mjamzito atafariki kwa kukosa sindano ya oxytocin kwa sababu tu amevuja damu. Hakuna mwanamke mjamzito wa Tanzania atafariki kwa kukosa dawa inaitwa Magnesium Sulphate kwa ajili ya kifafa cha mimba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsanteni. Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka bajeti hii tunaanza na hizo dawa mbili, lakini mipango yetu baadaye; sababu nyingine ya vifo vitokanavyo na uzazi ni uambukizo. Kwa nini wanawake wajawazito wanakufa? Kwanza wanavuja damu; pili, wanapata kifafa cha mimba; tatu, wanapata maambukizi na nne, wanapata uzazi pingamizi. Kwa hiyo, kwenye kifafa cha mimba na kwenye masuala ya kuvuja damu, tumekuja na hiyo intervention.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la uzazi pingamizi, ndiyo maana tumesema tutaboresha Vituo vya Afya 150 ili viweze kufanya upasuaji, huduma za uzazi za dharura, ikiwemo upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni. Mheshimiwa Bobali kwa kweli, unajua kuna jambo ulilisema, Mheshimiwa Waziri, unajua tumekupigia makofi kwa sababu ni mtu wa Tanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu watu wa Tanga tumeumbwa wanyenyekevu, watu wema, hatujui kujikweza; lakini licha ya kwamba natoka Tanga na unyenyekevu wangu na kutojikweza, lakini haya ninayoyaongea siyo ya kwenye makaratasi, nimetafuta hela kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya kuboresha Vituo vya Afya 100. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, pesa shilingi bilioni 67 ipo tayari kwenye akaunti za Wizara. Tumeshawaelekeza TAMISEMI watuletee mapendekezo ya Vituo vya Afya vya kuboresha. Katika hivyo vituo 100 tutajenga theatre, tutajenga wodi ya wazazi, tutajenga Maabara ya Damu na tutajenga nyumba ya watumishi.

Kwa hiyo, kaka yangu Mheshimiwa Bobali siyo maneno ya kwenye makaratasi, ni maneno ya vitendo na Waheshimiwa Wabunge wanawake nawashukuru sana kwa kuniunga mkono na naamini wote Waheshimiwa Wabunge… (Makofi/Kicheko/Vigelegele)

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, imetosha. Ahsante kwa heshima mliyompa Mheshimiwa Waziri. Tuendelee.

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niombe kupitishiwa bajeti, maana naona Waheshimiwa Wabunge wameridhika.

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuonesha dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kushughulikia tatizo la vifo vitokanavyo na uzazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme suala la vifo vya watoto wenye umri wa chini ya siku 30, Mheshimiwa Kemilembe, Mheshimiwa Mama Salma Kikwete wameliongea sana. Tumetoa maelekezo; tumetoa mchoro mpya kwa ajili ya hospitali. Hatutapitisha mchoro wowote wa hospitali ambao hautakuwa na chumba kwa ajili ya watoto wachanga (neonatal ward). Kwa hiyo, suala la pili, tumeshazielekeza Hospitali za Rufaa za Mikoa zote kuanzisha wodi kwa ajili ya watoto wachanga na sisi Wizara ya Afya tutaendelea kushirikiana na TAMISEMI na Wizara ya Fedha kutafuta rasilimali fedha kwa ajili ya vifaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeongea mambo mengi kwa ajili ya Sekta ya Afya, lakini naomba kabla sijazungumza maendeleo ya jamii, nizungumzie kidogo kuhusu lishe. Lishe ni muhimu sana. Nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote ambao mmetoa maoni, ushauri, jinsi ya kuboresha huduma za lishe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa ambalo tumelifanya kupitia Taasisi ya Chakula na Lishe, tumetengeneza mkoba kuonesha umuhimu wa siku 1,000 za kwanza za mtoto. Maana yake toka mimba ilipotungwa hadi mtoto anapofikia umri wa miaka miwili. Kwa hiyo, tutaendelea kutumia community health workers, wahudumu wa afya wa jamii, tutatumia pia redio na TV ili kuwahamasisha wananchi pamoja na wanawake kuwekeza katika afya zao na watoto wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la chanjo. Taarifa ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imesema kuna uhaba wa chanjo. Kuna mambo mengine mnachukua yamepitwa na wakati, mambo ya kwenye mitandao. Hatuna tatizo la uhaba wa chanjo za watoto nchini. Kwa hiyo, hayo yalikuwa ni mambo ya kwenye mitandao yanaletwa katika Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo chanjo za kutosha na ndiyo maana nimesema, ili kuhakikisha upatikanaji endelevu wa chanjo, tumetenga fedha za chanjo tumezitofautisha na fedha za dawa. Kwa sababu mtu akikosa dawa ataenda kununua kwenye pharmacy, lakini chanjo hazinunuliwi sehemu yoyote, zinatolewa na Serikali tu. Kwa hiyo, tunakiri kuanzia mwaka 2016 kidogo tulikuwa na changamoto, lakini sasa hivi hayo mambo yamepitwa na wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la maendeleo ya jamii. Kubwa ambalo limeongelewa na Waheshimiwa Wabunge, akiwemo Mheshimiwa Faida, kuhusu Benki ya Wanawake Zanzibar, Mheshimiwa Dada yangu Mheshimiwa Faida ameongea kwa uchungu sana, wifi yangu Mheshimiwa Munde, lakini pia Mheshimiwa Neema Mgaya, mdogo wangu amezungumzia suala la Benki ya Wanawake kwa nini haiko Njombe? Kamati ya Kudumu ya Bunge pia, imezungumzia suala la Benki ya Wanawake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepokea ushauri kwamba, sasa hivi kidogo kuna changamoto katika Benki ya Wanawake, kwa hiyo, tayari tumeshamwomba Mkaguzi Mkuu wa Serikali afanye ukaguzi maalum ili kubaini changamoto zinazokwamisha na kuweka mikakati ya kuboresha. Kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Wabunge mtuvumilie kidogo, kabla hatujaenda kufungua matawi mikoani, tusubiri taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali tuone ni mapendekezo gani atayatoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, suala la riba ya Benki ya Wanawake, naomba nijibu kwamba, tusubiri pia hiyo taarifa ya ukaguzi maalum wa CAG ili tuweze kuboresha utendaji kazi wa Benki ya Wanawake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati pia ya Kudumu ya Bunge imezungumzia suala la sheria kandamizi dhidi ya wasichana na watoto, ikiwemo Sheria ya Ndoa. Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria alitueleza changamoto tunazozipata katika kufanyia marekebisho Sheria ya Ndoa. Ninachoweza kuwaahidi Waheshimiwa Wabunge ambao mmeongea kwa hisia kubwa, wakiwemo Mheshimiwa Sebastian Kapufi, Mheshimiwa Juliana Shonza, Mheshimiwa Taska Mbogo, Mheshimiwa Ester Mahawe, Mheshimiwa Aida Khenani, Mheshimiwa Suzan Lyimo, Mheshimiwa Richard Mbogo na Mheshimiwa dada yangu Sophia Mwakagenda, ni kwamba, nitaendelea kushirikiana na wenzangu Serikalini kuangalia ni jinsi gani tunaweza kufanyia marekebisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri nami ni Muislamu, ziko changamoto zinazohusiana na masuala ya dini. Nimekutana na Mashehe na wameniambia ukisoma vizuri Kitabu cha Mwenyezi Mungu unaweza ukasema wala hakuna tatizo katika kufanyia marekebisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe changamoto ambayo nimeshampelekea Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali; Bangladesh asilimia takribani zaidi ya 90 ya Bangladesh ni Waislamu, lakini wamepitisha Sheria ya Ndoa mwezi Januri mwaka huu, 2017 ambapo wao sasa wamefanya hivi, wameongeza umri wa ndoa, wamesema umri wa ndoa kwa mwanamke utakuwa miaka 18 na kuendelea, lakini wakasema under special circumstances ndoa chini ya umri wa miaka 18 inaruhusiwa.

Kwa hiyo, nitaenda kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali angalau kutoa pendekezo hili, angalau na-raise minimum age of marriage kutoka 14 years to 18 years, lakini unatoa exceptions kidogo. Kwa hiyo, nimeangalia Malawi wenzetu wamepitisha Sheria ya Ndoa…

MHE. JOHN J. MNYIKA: (Hakusikika)

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Hapana Mheshimiwa Mnyika. Kuna watoto saa nyingine, Bangladesh wamesema kama ni mtoto under 18 years na under a special circumstances such as pregnancy, wameandika kama amepata mimba. Kwa hiyo, hiyo kidogo naweza nikawashawishi wenzangu ndani ya Baraza la Mawaziri na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwamba tunaweza tukabadilisha. Kwa sababu kilio kikubwa ni minimum age of marriage (umri wa kuolewa). (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum, Njombe, amezungumzia sana kwamba tumesema watoto ni asilimia 51, kwa hiyo, mnafanya jitihada gani za kuwekeza kwa watoto wadogo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rose Tweve nataka kukuthibitishia, kati ya jambo kubwa katika kulinda haki za watoto wanaonyonya; na Mheshimiwa Jenista nakushukuru sana; tulipeleka kwa Mheshimiwa Jenista mapendekezo ya kufanyia marekebisho ya Kanuni za Sheria za Kazi na Ajira; kwa sababu ile sheria ukiiangalia inasema mwanamke akimaliza maternity leave anaruhusiwa kunyonyesha, lakini sheria haisemi ananyonyesha kwa muda gani.

Mheshimiwa Jenista nakushukuru sana, tumepeleka mapendekezo, sheria inasema hivi, kwamba mwanamke mjamzito anaruhusiwa kunyonyesha baada ya maternity leave kwa muda wa miezi sita ndani ya masaa mawili na muda wowote ndani ya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili tutaendelea kuwataka waajiri kuzingatia mabadiliko ya sheria ambayo Serikali ya Awamu ya Tano imeyapitisha kuhakikisha watoto wananyonyeshwa na mama zao. Kwa hiyo, sasa hivi ni miezi sita baada ya martenity leave na masaa mawili, muda mwanamke mwenyewe mfanyakazi atakaosema. Akisema anaingia kazini saa 4.00 badala ya saa 2.00 sheria inamruhusu, akisema atatoka masaa mawili kabla ya muda wa kazi kwisha, sheria inamruhusu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisipozungumzia suala la ukatili dhidi ya watoto, sitawatendea haki watoto wa Tanzania. Nataka kuwathibitishia, licha ya kwamba tumetunga sheria kali dhidi ya vitendo vya ukatili dhidi ya watoto, lakini bado vinajitokeza kama nilivyoonesha katika taarifa yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kubwa ni kuendelea kuhamasisha jamii, walezi na wazazi. Mheshimiwa Mbunge aliongea jambo zuri sana, sasa hivi hata kama ni mila zetu mgeni kulala na mtoto mdogo; nataka niwaambie siyo salama kwa mgeni; awe ni mjomba, awe ni baba mdogo, kulala na mtoto wa kiume. Kwa sababu, kwa mujibu wa taarifa zetu, ubakaji dhidi ya watoto na ulawiti unafanywa na watu wa karibu ndani ya familia zetu. Kwa hiyo, tuchukue tahadhari ya kuwalinda watoto wetu dhidi ya vitendo vya ukatili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo ni mengi kama nilivyosema, lakini tunawashukuru sana kwa michango yenu. Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa kuchangia na kwa ushirikiano mzuri mnaotupatia, lakini kipekee nirudie kuwashukuru sana wafadhili wetu ambao wanatuwezesha kutekeleza miradi yetu ya Sekta ya Afya, ikiwemo wanaochangia Mfuko wa Pamoja wa Afya, niliwataja jana; Denmark, CDC, Ireland, Canada pamoja na Korea ya Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee jana sikuweza kuwashukuru Shirika la Afya Duniani ambao kwa kweli wanatupa msaada mkubwa katika kutekeleza masuala ya afya, hasa masuala ya kitaalam. Vile vile tunawashukuru sana UNICEF kwa michango yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu, sitaki kupigiwa kengele, niseme kwamba tumepokea changamoto. Nimalize moja, la Sheria ya Wazee, ni kweli, tuliahidi Sheria ya Wazee tutaileta Bungeni. Tumekwama kwa sababu, zipo taratibu ndani ya Serikali za kutengeneza sheria. Kwa hiyo, litakapomalizika tutakuja katika Bunge lenu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema jana, sote ni wazee watarajiwa. Ni jukumu la kila mtu ikiwemo Serikali kuhakikisha tunaweka mazingira mazuri na salama kwa ajili ya kuwalinda na kuwatunza wazee wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo sasa, naomba kutoa hoja.