Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Devotha Methew Minja

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nashukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia Wizara hii muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, niwapongeze waandishi wa habari ambao wanafanya kazi yao vizuri sana. Tuna kila sababu ya kuwapongeza waandishi kwa sababu tujiulize tu kama Taifa hili lingekuwa halina waandishi hakuna vyombo vya habari sijui tungekuwa kwenye giza la namna gani. Tunapenda tuwapongeze kwa kazi ambayo wanaifanya, japo tunajua wanafanya kazi katika mazingira magumu kuliko ilivyo kawaida. Tunaendelea kuwapa moyo waendelee kupambana kuendelea kutoa elimu na kuelimisha taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata katika hotuba ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani (Waziri Kivuli) alikuwa ametoa pongezi nyingi kwa harakati mbalimbali ambazo Waandishi wa Habari wanaendelea kufanya katika kujaribu kujitetea na kuhakikisha kwamba wanaendelea kuifanya kazi yao. Pamoja na kwamba hotuba ile imechinjiwa baharini lakini mimi nawapa comfort kwamba tutaendelea kuwasemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikiliza Waziri wakati wa hotuba yake, amewasifu wadau mbalimbali wakiwemo wanahabari, wanamichezo lakini sijasikia mahali akizungumza kuhusu habari ya mateso ya waandishi wa habari. Waandishi wa habari ambao walivamiwa na kuumizwa wakiwa katika press conference ya Chama cha Wananchi (CUF) ambao nao ni wadau muhimu nilitarajia angewapa pole. Hali kadhalika kwa wasanii, Ney wa Mitego na Roma Mkatoliki nao waliteswa ambao nao pia ni wadau wake, alipaswa nao awape pole kwa kazi kubwa ambayo wanafanya pamoja kupitia madhila mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni Mheshimiwa Waziri amenukuliwa akisema kwamba yeye ni msikivu na yupo tayari kuhakikisha kwamba anaendelea kusaidia tasnia hii ya habari iendelee kusonga mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni zaidi ya waandishi 30 wamepitia manyanyaso makubwa, wengine wakiwekwa ndani na Wakuu wa Wilaya, vyombo vya habari vikivamiwa ikiwemo redio ya Clouds, tunamuomba Mheshimiwa Waziri wakati ana windup hapa atueleze ni nini hatma ya ripoti iliyoandaliwa na Mheshimiwa Nape Nnauye wakati akiwa Waziri kuhusu sakata la kuvamiwa Clouds. Si hiyo tu pia atuambie ni sheria ipi ambayo inamruhusu DC kumzuia mwandishi wa habari asiingie katika Wilaya eti apate kibali cha kuandika habari.

Tunaomba Mheshimiwa Waziri atueleze kwa hii sheria ambayo RC, DC ana uwezo wa kumuweka mtu rumande kwa saa 48 iletwe Bungeni irekebishwe kwa sababu imekuwa ikitumika kama kigezo cha kuwaumiza waandishi wa habari. Tumeona Ndugu Mnyeti ambaye ni DC wa Arumeru amewaweka Waandishi wa Habari ndani kisa wameingia katika eneo lake la kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kuhusu Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 ambayo waandishi wa habari walitambuliwa rasmi kwa maana ya kuhakikisha professional hii ya waandishi wa habari inafanya vizuri. Tunashukuru hivi sasa Serikali inatambua kwamba tasnia ya habari ni muhimu na inafanya kazi. Hata hivyo, yapo mambo mengine ya msingi ambayo tunajiuliza, kama uandishi wa habari ni tasnia muhimu kama ilivyo professional zingine mfano za udaktari, wanasheria kuna mambo ya msingi sana ambapo yanatufanya tunashindwa kuielewa sheria hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikitokea mwandishi wa habari amefanya makosa ya kitaaluma sheria hii inasema akamatwe na polisi afikishwe mahakamani, lakini taaluma kama ya udaktari, endapo daktari atafanya makosa ya kitaaluma kuna sheria kwamba bodi inapitia, inamuajibisha lakini hakuna harakati za haraka haraka za kumpeleka polisi na kumfikisha mahakamani. Imewahi kutokea daktari ambaye alikuwa afanye operesheni ya kichwa akafanya ya mguu, lakini alifikishwa mahakamani? Kwa nini tunapokuja kwenye suala la uandishi wa habari wakamatwe na polisi wafikishwe mahakamani, tunaona hapa kuna double standard. Tunaomba kama kweli hii ni sheria na tumeamua kuitambua tasnia ya waandishi wa habari basi kama mtu atakuwa amefanya kosa la kitaaluma bodi zihakikishe zinamwadhibu kwa kuangalia taaluma hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze kuhusu ukata wa hivi sasa kwa vyombo vya habari, hii haijawahi kutokea. Hivi sasa waandishi wa habari hawana kazi za kufanya, kuna poromoko kubwa la waandishi kuachishwa kazi. Kampuni za The Guardian, Free Media, Azam na New Habari Cooperation zimepunguza waandishi. Ni kwa nini waandishi hawa wanapunguzwa? Ni kwa sababu hali imekuwa ngumu, wanafanya kazi katika mazingira magumu. Gazeti ambalo lilikuwa linatengeneza nakala 26,000 sasa hivi linatengeneza nakala 5,000. Hali hii inakuwa ngumu zaidi kwa sababu Serikali haipeleki matangazo kwenye hivi vyombo vya habari hususani vya private.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Rais akihitaji kufanya press conference anaita vyombo vyote, Mkuu wa Wilaya au RC wakitaka kufanya press conference anaita vyombo vyote lakini ikija kwenye suala la matangazo vyombo vya binafsi vinabaguliwa. Kwa nini tusitende haki tuwezeshe hizi private sector zifanye kazi zipate matangazo ziweze kuhudumia Taifa hili? Kama kuna mkakati wa kuhakikisha kwamba tunadumaza vyombo hivi tuelewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima Serikali iangalie imetoa mamlaka hivi hivi sasa kwa Idara ya Habari - Maelezo yenyewe ichuke jukumu la kuratibu matangazo yote. Katika matangazo ambayo yanakwenda kwenye vyombo vya habari, Idara ya Habari - Maelezo ambayo imepewa jukumu ya kuratibu matangazo inapata commission ya asilimia 10, kwa hiyo imeacha kazi yake ya msingi sasa hivi inahakikisha inatafuta matangazo. Hii ni kama ilivyo sasa hivi traffic ambapo wameacha kazi zao za msingi za kuhangaika na ajali inahangaika na tochi za kukusanya. Tunaomba tusaidiwe tujue kama kweli suala hili la kuratibu matangazo ambalo linakwenda kwa njia ambayo ni ya kibaguzi kupitia Idara ya Habari - Maelezo, ni kwa nini utaratibu wa zamani usitumike na vyombo vyote vipate haki katika kupata matangazo ili viweze ku–retain waandishi ambao wameajiriwa katika vyombo hivi vya habari. (Makofi)

Mheshimwa Mwenyekiti, tukitoka hapo tuzungumze kuhusu hofu iliyopo hivi sasa kwa vyombo vya habari. Hakuna uhuru kabisa wa vyombo vya habari hapa nchini. Tumemsikia Mheshimiwa Rais katika ziara zake Mkoani Shinyanga alisema yapo magazeti matatu ambayo yupo karibuni kuyafungia, japo hakuyataja lakini hii moja kwa moja kama mkuu wa nchi inaleta hofu kwa waandishi wa habari na wamiliki wa vyombo vya habari kuona kwamba pengine ni mimi au yule. Kwa hiyo, waandike habari ya kuipendeza Serikali na kuacha kuandika habari za kukosoa Serikali pale ambapo inakwenda kinyume na utaratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sakata la Bashite kuvamia Clouds, Rais alinukuliwa kwamba vyombo vya habari haviko huru kwa kiasi hicho na kutoa karipio kali. Tulitegemea kwamba Rais angesaidia kwa mtu kama huyu ambaye amekiuka maadili ya utumishi wa umma kwa sheria ya mwaka 1995 mpaka sasa hivi asingekuwa kazini. Kwenda kuivamia studio na waandishi wa habari ambao wanafanya kazi zao kihalali na kuhakikisha waandishi...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.