Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Prof. Norman Adamson Sigalla King

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. PROF. NORMAN A. S. KING: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kuungana na wenzangu kutoa pole kwa ajili ya msiba mkubwa ambao Taifa letu limepata na bila shaka Mungu atawatunza watoto hawa maana ni wenye haki mbele zake.

Mheshimiwa Spika, nianze kuchangia kwenye eneo la timu yetu ya Taifa. Mwaka 1985/1986 mimi ni mmoja wa wachezaji walioitwa kwenye Timu ya Taifa ya vijana. Wakati huo tulikuwa tunafundishwa na kaka yetu Joel Bendera, sifa ya kujiunga na timu hizo ilikuwa ni ubora wa wachezaji hao waliotafutwa Sekondari na kwingineko, maadam umri wao ulikuwa chini ya miaka 24.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi watu wengi wanapoongelea timu ya Taifa, wanaongelea kana kwamba tatizo kubwa la Timu ya Taifa kufanya vibaya ni kwa sababu hakuna timu za watoto wadogo. Ni tabia yetu kutokukumbuka historia ya mafanikio yetu.

Mheshimiwa Spika, ni vizuri Waziri afahamu kwamba ili ufanye vizuri, cha kwanza ni wachezaji bora, lakini cha pili ni Mwalimu mwenye weledi. Nijikite hapo kidogo. Timu yetu ya Taifa kwa miaka nane mfululizo imekuwa ikifundishwa na kocha ambaye kwenye timu yake binafsi, yaani klabu yake hajawahi chukua ubingwa. Yaani kocha kwenye timu yake anakuwa katika tano za mwisho, lakini anapewa Timu ya Taifa ili ishinde, it is impossible! Haiwezekani! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukitaka kocha mzawa afundishe Timu ya Taifa ni lazima uchukue the best coach. Unampataje? Aliyefanya vizuri kwenye ligi! Sasa kocha amepewa timu, ameshika nafasi ya mwisho au tano mwishoni kwa miaka karibu nane, tisa, kumi; bado kwa sababu ya vyeti vizuri tu, ndiye awe kocha wa Timu ya Taifa; haiwezekani kushinda.

Mheshimiwa Spika, Mwalimu wa timu ya mpira wa miguu kama ni mzawa ni lazima achukuliwe katika makocha waliofanya vizuri na ndiyo maana ni maoni yangu kwamba kijana wetu Mecky Mexime pamoja na kwamba ni kijana mdogo, lakini as of now, ndiye kocha mzawa ambaye kwa miaka minne, mitano mfululizo timu alizoshika amefanya vizuri. Yanga au Simba akichukua ubingwa, anachukua ubingwa akiwa na foreign coach, lakini kocha mzawa anakuwa yeye. Hata akishika utatu, lakini that is the best coach.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba sana Mheshimiwa Waziri afahamu kwamba ni muhimu sana unapo-dedicate team kwa Mwalimu, ni lazima awe ni Mwalimu mwenye good performance. Bahati mbaya sana siyo wakati wote vyeti vinaashiria uwezo na hasa unapoongelea kupima mpira, siyo wakati wote.

Mheshimiwa Spika, ni muhimu niongelee kidogo viwanja vya mpira. Wizara inayosimamia michezo ni vizuri sana ishirikiane na Wizara ya TAMISEMI ili kuona ni jinsi gani wanaweza wakaboresha viwanja vyetu hasa vya shule za sekondari na msingi.

Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye Majimbo yetu na Tanzania nzima ni viwanja vichache sana vya shule za sekondari au msingi ambavyo vina vipimo vizuri na ambavyo level yake unasema atapatikana hapa mchezaji mzuri. Viwanja vingi ni vibovu, kwa hiyo, havitoi tafsiri ya kwamba watoto wanaoandaliwa katika viwanja hivi, watakuwa ni wachezaji bora.

Mheshimiwa Spika, ni muhimu sana viwanja vyetu angalau viwe na level ile inayoonesha kwamba watoto wetu watajifunza mpira; na vile vipimo pia vifanane na huko wanakokwenda. Hili likifanyika kwa ushirikiano wa TAMISEMI pamoja na Wizara inayosimamia michezo, itasaidia sana kupika wachezaji ambao ni wazuri.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, unaweza ukakumbuka kwamba wakati amekuja kocha Maximo, yule wa Brazil, moja ya vitu ambavyo vilimsaidia yeye kufanya vizuri ni kwa sababu alipewa ushirikiano mkubwa na Serikali; malipo mazuri. Ndiyo wakati pekee ambapo wachezaji walijifunza hata kulala kwenye hoteli za kitalii au hoteli kubwa kama Golden Tulip kwa mwezi, miezi miwili au mitatu. Hamasa hiyo ilitosha timu hiyo kuipa nafasi ya kufanya vizuri.

Mheshimiwa Spika, ombi langu; ni muhimu sana Wizara ikishakabidhi timu kwa kocha mzawa, vile vile facilities ikiwa ni pamoja na malipo kwa kocha huyo yafanane na makocha wa kigeni ambao tunawaenzi. Mbona inawezekana kuwalipa makocha wa kigeni fedha nyingi? Tunashindwa nini kufanya hivyo hivyo kwa makocha wanapokuwa sio wa kigeni? Hili likifanyika itakuwa muhimu kutia ubani na kutia nguvu kwa makocha wetu kuweza kufanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nisingependa nichukue muda mrefu kwenye hili. Nisisitize tu kwamba Timu yetu ya Taifa na michezo kwa ujumla ndiyo heshima yetu. Bahati mbaya sana mchezo unaopewa heshima kila wakati ni mpira wa miguu. Naomba sana, Wizara ipeleke nguvu pia kwenye michezo mingine. Iko michezo mingine kama michezo ya ngumi ambayo wengine tunaicheza, ni rahisi kufanikiwa kwa sababu michezo yote ambayo inajali uwezo wa mtu binafsi ndiyo michezo rahisi kushinda.

Mheshimiwa Spika, wewe ni mwanamichezo, unafahamu. Mpira wa miguu ndiyo mpira mgumu zaidi katika michezo kwa sababu akikosea mtu mmoja mnafungwa wote. Anakosea mtu mmoja, mnafungwa wote hata kama mmecheza vizuri, lakini mtu mmoja akizembea tu mnahesabika Tanzania mmefungwa; lakini ngumi, ukikosea wewe, unapigwa wewe. Ndiyo michezo mepesi kufundisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, michezo kama table tennis, kwa maana ya singles, ni rahisi! Table tennis ni rahisi, long tennis ni rahisi maana ukikosea wewe unafungwa wewe na ndiyo rahisi kufanikiwa na kushinda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nisije nikaketi bila kukumbuka kuipongeza timu ya Taifa zima kwa jina la Simba Sports Club kwa kazi kubwa ambayo wanafanya ya kufanikiwa kucheza michezo ya Kimataifa kila wanapowakilisha nchi yetu, wamekuwa wakituwakilisha vizuri na hawajawahi kutuangusha. (Makofi)

Mungu ibariki Simba Sports Club na Mungu wabariki wanamichezo wote. Ahsanteni.