Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Maryam Salum Msabaha

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Awali ya yote na nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia tena kusimama katika Bunge lako hili Tukufu nikiwa na kauli thabiti na pumzi. Nitoe pole kwa walimu na wanafunzi wa Mkoa wa Arusha waliopatwa na maafa. Mwenyezi Mungu awapumzishe mahali pema peponi na wafiwa wote awape faraja, kila nafsi itaionja mauti kwa wakati na wasaa wake.

Mheshimiwa Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri aangalie pia hotuba ambayo imewasilishwa na Kambi ya Upinzani, siyo yote aliyowasilisha ni mabaya yapo mazuri ambayo anaweza kuyachukua akaboresha Wizara yake. Siyo useme Upinzani kila kitu ni kubeza, sisi tupo hapa kushauri na yale mazuri tuliyowashauri kwenye hotuba ya Upinzani muyachukue ili mboreshe Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, nitazungumzia suala la Kiswahili lugha ya Taifa. Zanzibar kuna wataalam wazuri sana wa Kiswahili lakini tumejipanga vipi katika ajira za Afrika Mashariki kuhusu lugha hii? Tunaona wenzetu Kenya hata nafasi zile za kwetu wanajitangaza. Leo hii ukiwa Marekani unakuta wenzetu wao ndiyo wanajitangaza kwenye hii fani ya Kiswahili wanakaa kule mpaka wanakuwa wakalimani, wanasomesha lakini bado Watanzania wako nyuma katika hili suala la kutangaza Kiswahili au kuchangamkia hizi ajira za soko la Walimu wa Kiswahili.

Mheshimiwa Spika, nimuulize Mheshimiwa Waziri, ana mkakati gani kuhakikisha Maprofesa wa Chuo Kikuu ambao wako kwenye masuala ya lugha yetu ya Taifa ajira zinazotoka kwenye hizi nchi za Afrika Mashariki wanapata fursa? Tumemwona Mheshimiwa Rais yuko katika masuala haya ya kukuza Kiswahili na kauweka utaifa mbele hata anavyokwenda kwenye mikutano mara nyingi amekuwa akiongea Kiswahili. Hata hivyo, tuangalie hawa wakalimani ambao wanafuatana na Mheshimiwa Rais ni namna gani wanaweza kujipanga Rais akiwa anahutubia angalau waende hatua kwa hatua yale maneno ya tafsiri yafahamike vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashauri hata wanaopata nafasi ya kuwakilisha nchi yetu ya Tanzania kwenye mikutano mbalimbali na wao watangaze Kiswahili kama lugha ya Taifa. Nasema hivi kwa nini? Hakuna nchi yoyote ambayo imeendelea duniani kwa kuiga lugha za wengine. Ukienda dukani kwa wenzetu Korea huwezi kuuziwa kitu kama hujui Kikorea, lugha yao wameiweka mbele hata Japan na China ni hivyo hivyo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nasi tuangalie ni namna gani tutakuza lugha yetu ya Kiswahili siyo mtu unafika mahali unakwenda kwenye mkutano wa kimataifa unaongea Kiswahili lakini hakieleweki kama unaongea Kiswahili au Kiingereza. Tusimame tusimamie lugha yetu ya Taifa ili nasi tujitangaze na tukuze uchumi kwa kupitia lugha yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la vyombo vya habari. Vyombo vya habari ni suala mtambuka. Vyombo vya habari vinatoa taarifa ya matukio mbalimbali kwa jamii.

Tumeona ni namna gani jamii imetumia vyombo hivi vya habari na wakapata msaada. Mfano kuna Watanzania hasa wa vijijini ambao walikuwa wanaugua au wako katika hali mbaya kiafya au wana maradhi sugu tumeona kalamu za waandishi wa habari zilivyotumika na Watanzania hawa wakapata msaada.

Mheshimiwa Spika, hapa tuna Wabunge wa Majimbo, Viti Maalum (Mikoa) au wa Kuteuliwa na Rais na tuna Mawaziri ambao wamepitia kwenye Majimbo wakapata uwaziri lakini utaona ni namna gani sisi wanasiasa tumeminywa katika vyombo vya habari. Napenda kujua ni kitu gani Serikali mnachoogopa katika suala hili la vyombo vya habari kwa suala la kutangaza Bunge live? Kwa sababu unavyotangaza Bunge live mimi kama mimi nimetoka Zanzibar, kuna wananchi wangu wanataka wajue leo Msabaha kaongea nini kuhusu Zanzibar lakini hawapati. Hamuoni mnajijengea mazingira ambayo ni magumu itakavyofika 2020 kwenda kuomba kura kwa sababu Watanzania wanataka wasikie wawakilishi wao waliowatuma wanasema nini Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wananchi wanakatwa kodi zao kwa ajili ya TBC, kwa hiyo wanategemea iwapatie mijadala ya Bunge la Bajeti waone Mbunge wao kasema nini Bungeni. Hata wengine tukiongea humu huwa taarifa nyingine kama hazijapendeza watu haziwezi kutoka, kila mtu ana haki katika Bunge hili na kila mtu kaletwa hapa na wananchi kuwakilisha sehemu alipotoka.

Mheshimiwa Spika, tuangalie tena suala lingine, hapa kuna wawakilishi kutoka upande wa Zanzibar, kuna Wabunge ambao wametoka kule na kuna Wawakilishi ambao wamekuja hapa kutoka Baraza la Wawakilishi, kwa hiyo ni muhimu tuangalie pia sekta ya Muungano kuhusu vyombo vya habari. Katika sekta hii ya habari wale wanaokuja kuchukua habari zetu kwa upande wa pili nao wamo au habari za Zanzibar zitaishia kubaki Zanzibar na za Bara zitaishia kubaki Bara? Kwa hiyo, tuangalie namna ya kudumisha Muungano kwenye suala la habari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende tena kwenye suala la michezo. Michezo ni afya lakini hata michezo ndani ya Bunge, sisi tumekuwa tukienda kuwakilisha Tanzania Afrika Mashariki. Tumeshuhudia wenzetu waliokwenda Kenya (Mombasa) kwenye mashindano ya Afrika Mashariki utajiuliza kweli Serikali ina mikakati ya kukuza michezo kwani Wabunge waliokwenda kule walitia aibu. Tuangalie tumejipanga vipi hata tunavyoshiriki katika mashindano ya Afrika Mashariki kama Wabunge na sisi tupate hadhi zetu kama Wabunge.

Mheshimiwa Spika, leo michezo haipewi kipaumbele. Tuangalie Brazil, Brazil imeendelea kutokana na michezo, kwa nini sisi Tanzania hatutaki kuipa michezo kipaumbele? Tumefanya michezo ni kama kiburudisho au kuondosha kisukari na presha kwenye mwili, hapana, michezo inaingiza pato la Taifa. Naomba tuangalie namna gani ya kukuza michezo na kutafuta vipaji, tuanze na sisi Wabunge ni mara ngapi tumekuwa tukileta makombe ndani ya Bunge hili, lakini kila tunavyokwenda mbele michezo inasahaulika.

Mheshimiwa Spika, zamani wakati tupo shuleni michezo ilikuwa inaanza kule shuleni, unaanza kuangalia vipaji kule shule, unaanza kumkuza yule mtoto akiwa mdogo mpaka anafika kiwango cha kuwa mwanamichezo bora lakini sisi michezo tumefanya kama sehemu ya kutoa presha na kisukari kwenye miili yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba Serikali itenge bajeti ya kutosha kuhusu michezo na hasa suala la Wabunge wanavyoshiriki kwenye mashindano ya Afrika Mashariki pia watengewe bajeti ya kutosha. Mheshimiwa Spika utalichukua kama wewe ndiyo kiongozi wetu wa Bunge na siyo kama tunashiriki michezo ya Afrika Mashariki tunakwenda kudhalilika mbele ya Wabunge wenzetu. Hilo naomba ulipe kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yameongelewa sana mambo ya sanaa. Kwenye sanaa wanawake…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.