Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. LUCY F. OWENYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia. Nianze na utamaduni. Palikuwepo na mchakato wa kuanzisha vazi la Taifa na fedha zilitumika katika mchakato wa kupata vazi hili ilifikia mpaka kutolewa mifano ya vazi la Taifa. Je, mchakato ule umefikia wapi na mpaka sasa fedha kiasi gani zimetumika?
Mheshimiwa Spika, kwa sasa hivi vijana wetu maadili yameporomoka sana, kuanzia mavazi hata baadhi ya lugha wanazotumia, heshima kwa wakubwa hakuna na kupoteza kabisa mila na desturi ya Watanzania ya kuheshimu hata wakubwa zao. Je, Serikali imejipangaje kurudisha maadili na utamaduni wetu wa Kitanzania wa kuheshimiana? Tukiimarisha utamaduni wetu, wa kucheza ngoma za kienyeji, mapishi ya kienyeji na kadhalika inaweza kuwa ni moja ya vivutio vya utalii hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, michezo. Kutokana na magonjwa kuongezeka duniani magonjwa yasiyoambukiza kama sukari ya kupanda, shinikizo la damu la kupanda juu na magonjwa ya moyo, mazoezi ya mara kwa mara yanaweza kupunguza magonjwa haya. Je, Serikali wamejiandaa kwa kiasi gani kuhakikisha wanajenga viwanja vya michezo kwa Wilaya kwa kuanzia lakini ziteremke chini kila Halmashauri?
Mheshimiwa Spika, kiwanja cha King Memorial kilichopo Manispaa ya Moshi. Uwanja huu ni mkubwa kabisa na michezo zaidi ya saba. Hakuna uwanja Moshi na uwanja huu ni wa Mkoa. Tumekuwa tukitumia uwanja wa ushirika ambao ni mdogo, tulishuhudia sherehe za Mei Mosi 2017 pale uwanja wa Ushirika walishindwa kufanya maonesho ya magari kwa sababu ya udogo wa uwanja. Hata mashindano yajulikanayo kama Kilimanjaro marathon huwa yanafanyika uwanja wa Ushirika, lakini michezo hii imekuwa sana inaleta wageni duniani pote kwa sasa ni padogo na suluhisho ni kuutengeneza uwanja wa King Memorial. Hivi inaingia akilini King Memorial penye heka zaidi ya 10 patumike tu kama soko la kuuzia mitumba ambayo hawatumii hata eneo lisilozidi heka mbili? Kwa nini wasipatiwe sehemu nyingine kama kule Pasua, Manyema na kadhalika, sehemu zipo nyingi.
Mheshimiwa Spika, habari. Ni haki ya Watanzania kupata habari. Hii ikiwa ni pamoja na wananchi hawa kupata habari zinazoendelea Bungeni ili wajue Wabunge wao kama wanawasilisha matatizo yao. Kwa kuwanyima haki hii ni uvunjifu wa Katiba. Je, ni lini shughuli zote za Bunge zitarudishwa na kuanza kurushwa live ili wananchi waweze kupata habari kuhusu nini kinaendelea Bungeni? Kwa nini Serikali inaogopa?