Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Hasna Sudi Katunda Mwilima

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Spika, naomba kuchangia kwa maandishi Wizara hii. Kwanza nianze kwa kutoa pole kwa familia ya watoto na Walimu pamoja na dereva wa basi lililopata ajali Wilayani Karatu, Mkoa wa Arusha. Nitoe pole za dhati ya moyo wangu kwa kweli inasikitisha sana tena sana na kutia uchungu, kikubwa kazi ya Mungu haina makosa. Tuombe roho za marehemu ziwekwe mahala pema peponi amina.

Mheshimiwa Spika, pili nimpe pongezi mzee wangu Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe kwa kuendelea kuaminiwa na Mheshimiwa Rais kupewa Wizara hii ya Michezo, Habari na Utamaduni.

Mheshimiwa Spika, wilaya nyingi nchini hazina viwanja vya michezo ya football, netball, basketball na kadhalika, lakini kuna mikoa hapa nchini ina historia ya kutoa wachezaji bora na wasanii bora kama Mkoa wa Kigoma ninaotokea mimi.

Mheshimiwa Spika, cha kunishangaza ni kuona TFF wanajenga viwanja Mwanza na kuacha kuboresha viwanja vya Lake Tanganyika na Wilaya ya Kigoma ili kuwaenzi wachezaji wa zamani kama kina Sande Manara, Katwila, kina Mambo sasa, Kitwana Manara na wengine na hata kina Mizani Khalfan kina Juma Kaseja na wengine wengi.

Mheshimiwa Spika, pia kuhusu suala la wasanii wa muziki wa kizazi kipya kama kina Diamond, Ali Kiba, Omari Dimpozi, Banana Zoro, Maunda Zoro, Juma Nature na kadhalika wote hawa wanatoka Kigoma.

Mheshimiwa Spika, inaashiria kuwa Mkoa wa Kigoma ni mkoa unaotoa vipaji vya kila aina. Tunachoomba Serikali ni kuona namna ya kuwasaidia wasanii hawa kuwa na hati miliki ili waweze kunufaika na vipaji vyao vya asili kuliko kama ilivyo sasa msanii anatunga yeye, anaimba yeye, anayenufaika ni mwingine.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo nizungumzie suala la utamaduni; tuombe Serikali kupitia Wizara hii kurudisha ngoma za asili mashuleni ili basi tuweze kuenzi ngoma zetu za asili. Kupitia mashuleni sherehe mbalimbali za kitaifa, sherehe za mikoani na wilayani kuwa na utaratibu wa kualika ngoma za asili ili kutunza tamaduni zetu za Tanzania.

Mheshimiwa Spika, nichangie pia kukuza michezo mashuleni kwa kurejesha kwa nguvu kubwa michezo ya UMISETA ili kuanza kuibua michezo mashuleni na hatimaye watoto wakue na vipaji vyao.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie pia suala la TBC; hali ya huko vijijini TBC haisikiki kabisa tuombe Serikali kupitia Wizara hii ione namna gani ya kuboresha vitendea kazi ili waweze kufanya kazi yao ya kutoa huduma kwa watanzania wote hususan kwa wananchi wa vijijini.

Mheshimiwa Spika, niongelee pia suala la mchezo wa kuogelea kuna tatizo la mchezo wa kuogelea pale ambapo tunaacha kwenda kuibua vipaji kwenye wilaya zenye maziwa kama vile Ziwa Tanganyika, Ziwa Nyasa na Ziwa Victoria, hebu tushauri Serikali kuibua vipaji kwenye maeneo hayo kwani watoto wengi hujua kuogelea vizuri. Tukiwapa mafunzo ya kuogelea kwenye swimming pool wanaweza kufanya vizuri na kuiletea ushindi nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, mwisho nizungumzie lugha ya Kiswahili; kuna tatizo kubwa la nchi za nje kama USA, Holland, UK, na kadhalika watu wa DRC na Kenya ndio wanaofundisha Kiswahili kwenye vyuo vikuu vya nchi mbalimbali, kwa nini Serikali isiwaandae Walimu wa Kitanzania wanaochukua somo la Kiswahili na Kiingereza ili wawe na degree ya lugha tu na waweze kuthubutu kwenda nje kufundisha lugha ya Kiswahili.

Mheshimiwa Spika, baada ya hayo, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.