Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Spika, Tasnia ya Sanaa za Ufundi ndio yenye ushiriki mkubwa wa Wasanii kuliko sanaa nyingine nchini Tanzania. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na BASATA 2006, idadi ya wasanii nchini ni milioni sita; zaidi ya milioni nne kati ya hao ni wale wanaojishughulisha na sanaa za ufundi wakiwemo, wachongaji, wachoraji, wachoraji katuni, tingatinga, wasusi, wabunifu wa mitindo, walimbwende na kadhalika.
Mheshimiwa Spika, tafiti mbalimbali ikiwemo ya (WIPO) Word Intellectual Property Organization 2012), pia zinaonesha ni kiasi gani tasnia hii inachangia kwa kiasi kikubwa kwenye ajira na pato la Taifa kuliko hata madini.
Mheshimiwa Spika, pamoja na mchango huo kwa Taifa, sanaa hii haipewi kipaumbele na Serikali, hivyo kudumaza maendeleo yake. Changamoto zifuatazo ni baadhi ya vikwazo vya maendeleo katika tasnia hasa sanaa ya uchoraji. Sheria kandamizi hasa kuporwa kwa maeneo mfano, kama ilivyokuwa katika maeneo mengine ikiwemo Nyumba ya Sanaa, sasa kumetokea watu wanaotaka kupora eneo la wachongaji Mwenge, eneo ambalo lilikabidhiwa Chama cha Wasanii Wachongaji Tanzania (CHAWASATA) na Serikali ya Awamu ya Kwanza mwaka 1984. Kufuatia kuhamishwa kutoka barabara ya Ali Hassan Mwinyi Road (Zamani Bagamoyo Road) ili kupisha upanuzi wa barabara hiyo.
Mheshimiwa Spika, kwa mshangao mkubwa wamejitokeza waporaji wenye nguvu za kifedha wanaoshirikiana na Kamishna wa Ardhi ili eneo lile lipewe watu wengine. Jitihada mbalimbali zimefanywa na chama cha CHAWATA ili kunusuru eneo hili lisiingie mikononi mwa wanyang’anyi ikiwemo kuomba msaada kwa vyombo vya umma ikiwemo BASATA ambao kwa barua yao ya hivi karibuni walisema jambo hilo haliwahusu.
Mheshimiwa Spika, naomba Wizara ituambie, nani anayehusika kufuatia hali hii tete ya sintofahamu. Hali ya amani katika Kijiji cha Mwenge Vinyago ni tete na wachongaji wasingependa kulazimishwa kuingia katika uvunjifu wa amani. Jamani, naomba suala hili lipatiwe majibu ili hali ya utulivu iendelee. Naomba sana Wizara hii ambayo iko chini ya Mwanasheria Dkt. Mwakyembe aliyebobea alisimamie hili kwa nguvu zote ili haki ya wachongaji hawa isipotee na wanamtegemea sana na wana imani na Waziri na watendaji wote.
Mheshimiwa Spika, changamoto nyingine kubwa inayokabili fani ya uchongaji ni watu wa Maliasili na Utalii ambao wamekuwa wakizuia vinyago visipite Airport hata kama vina stakabadhi halali za TRA. Hali hii imedumaza soko la vinyago toka asilimia 59 hadi asilimia 15 kitu ambacho ni hatari na hii ni fursa kwa majirani zetu hususan Kenya. Kupitia Idara ya Sanaa, watu wa maliasili wameambiwa wakae nao ili kwa pamoja wajue na kufikia muafaka, lakini bila mafanikio. Inasikitisha sana.
Mheshimiwa Spika, pia kama ukifuatilia utendaji wa Mamlaka zingine hususan Tume ya Ushindani, bidhaa zote feki huwa zinachomwa zile zinazokamatwa tena hadharani, je vinyago vinavyokamatwa vinapelekwa wapi? Hatujawahi kuona vinateketezwa au kupigwa mnada ili kusaidia wenye mahitaji mbalimbali na kadhalika. Kuna tetesi kuwa, vinyago hivyo vinavyokamatwa pale airport hurudishwa Mwenge kwa mlango wa uwani. Naomba ukweli wa jambo hili na maelezo.