Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mwibara
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, majeshi yetu ya Polisi, Magereza, Uhamiaji pamoja na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ni majeshi ambayo yamesahaulika, ni majeshi ambayo yanachukuliwa kama ni ya kawaida, ni majeshi ambayo yanadhaniwa watendaji walioko mle hawana professionalism ya aina yoyote. Ndiyo maana majeshi haya yamefanywa kama majeshi ya miujiza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Yesu peke yake Mwana wa Mungu aliye hai ambaye ni bingwa wa miujiza, ambaye alikufa akafufuka, ambaye alimfufua Lazaro, ambaye alitembea juu ya maji. Hivi kweli kama majeshi haya hatutawekeza, hatuwezi tukapunguza uhalifu katika nchi yetu, hatuwezi tukajenga nidhamu ya majeshi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwakumbushe kidogo Waheshimiwa Wabunge, hima himaaa, Tanzania sauti hii ukiona vyaelea vimeundwa, msidhani magwaride haya mnayofurahi jinsi majeshi wanavyopiga mguu chini, jinsi wanavyotoa sauti yao ya kutoa heshima ya utii kwa Amiri Jeshi Mkuu, mkadhani sauti hii imekuja hivi hivi. Sauti hii inatengenezwa na lishe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inakuwaje askari wetu tunawapa shilingi 10,000, shilingi 10,000 hii aiache kwa familia, shilingi 10,000hii aende nayo kwenye lindo la benki, shilingi 10,000 hii aende nayo doria, asubuhi mpaka jioni haitawezekana. Ndiyo maana Waziri anapotuambia katika
ukurasa wake wa 21 katika hotuba yake kwamba Serikali inaendelea kuboresha maslahi ya watendaji wa vyombo vya usalama kwa kuwapatia ration allowance za kila mwezi. Mheshimiwa Waziri unasema unaendelea kuboresha ration allowance mbona kwenye kitabu chako humu hujaboresha, umeweka maneno tu yasiyoboresha? Tunahitaji uboreshe maslahi haya ili askari wetu waweze kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, askari hawa mnaosikia wengine wanatekwa kwenye mabenki, wengine wanavamiwa kwenye doria, wakati mwingine wanakuwa kwenye stress, hajui leo familia yake itakula nini, hajui yeye atakula nini, anabaki askari wa kupiga miayo tu kwenye benki matokeo yake wanamnyang’anya bunduki. Tunahitaji kuboresha maslahi ya Jeshi la Polisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye mafunzo, Mheshimiwa Mwigulu ulipokuwa Wizara ya Kilimo ulikuwa na kauli mbiu mkitaka mali mtaipata shambani. Sasa leo uko Wizara ya Mambo ya Ndani nataka nikushauri, ukitaka kupunguza msongamano magereza, siyo kujenga mabweni ni kupunguza uhalifu katika nchi yetu. Ukitaka kupunguza uhalifu katika nchi yetu lazima uzingatie mambo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya miaka kumi sasa hakuna traffic courses kwenye Jeshi la Polisi, imebaki tu wewe askari kesho unapigiwa simu unakuwa traffic na ndiyo maana ghafla mnaona traffic anachoropoka kwenye vichaka kwa sababu hawana mafunzo ya aina yoyote. Mnagombana na askari traffic hawana mafunzo, tunataka mafunzo ya askari wa usalama barabarani wasomee magari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna masuala ya CID. Msongamano utaendelea kwa sababu upelelezi uko kiwango cha chini sana, kesi zinachukua muda mrefu kwa sababu ya kutokuwa na mafunzo katika kupeleleza, kwa sababu ya kutokuwa na fedha ya kutosha kwenye Criminal Investigation Fund, mfuko ambao unatumika kuwapatia watu wanaoleta taarifa, taarifa ni za kununua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la CRO wenzangu ambao hamkupita kwenye Jeshi kama hilo maana yake mimi nimepita huko nina-declare interest. Pale mnapoita kaunta pale, pale ni CRO pale kulikuwa na mafunzo ya CRO, lazima anayekuwa in charge pale awe amefundishwa namna ya kupokea mashitaka, namna ya kujua hili ni kosa la jinai au ni kosa la civil, matokeo yake kunakuwa na malalamiko mengi ndani ya Jeshi la Polisi, kwa sababu hakuna kozi kama hizi za CRO.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba Mheshimiwa Mwigulu kozi hizi zirudi na wafundishwe Askari ili wajue kupokea mashtaka, tunaposema watu wanabambikizwa kesi ni pamoja na kutokujua hii ni ya criminal au ni ya civil kwa sababu hawajapata mafunzo ya CRO muda mrefu.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye vitendea kazi. Kwenye PGO lazima askari anapopanga ile duty roster pale kituoni, kunakuwa na askari wa standby…
(Hapa Kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.