Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Kilombero
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. PETER A. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa leo ni mara ya kwanza nasimama ndani ya Bunge lako kuzungumza tangu nimetoka Gereza la Ukonga, ambako nilikuwa natumikia kifungo batili cha miezi sita, nashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Kilombero, kwa namna ambavyo wananipenda, wananiheshimu na wanajua mchango wangu kwao, kiasi ambacho nilipokuwa nimefungwa hawakukata tamaa, walikuwa wanakuja kuniona, walikuja kwa wingi Idete, mpaka ikaonekana wanaweza wakavunja Gereza, maana walikuwa wengi sana, ikabidi nihamishwe. Nawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitoe shukrani za pekee kwa Chama changu, Mwenyekiti wangu wa Chama Taifa Mheshimiwa Mbowe, Wakili wangu msomi Mheshimiwa Tundu Lissu, pia ninawashukuru watu wote waliokula njama, walionifanyia fitna na uhuni ili nifungwe, Mungu awabariki sana. (Makofi)
Mhehsimiwa Mwenyekiti, vilevile niwashukuru Wabunge wa CCM wakati Kiongozi wa Upinzani Bungeni (KUB) Mheshimiwa Mbowe anazungumza yanayonisibu gerezani na kutaka Bunge lichukue attention nawashukuru kwa kumzomea, ila mjue mlikuwa hamzomei Mwenyekiti, hamkuwa mnamzomea Mbowe ila mlinizomea mimi, Mungu awabariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima kabisa ninawashukuru wafungwa wa Gereza la Ukonga na wale wa Gereza la Idete, maana naamini maisha yangu yalikuwa mikononi mwao. Wangeweza kufanya ubaya wowote lakini waliniheshimu, wakanitunza na niseme Mungu awabariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu programu ya Parole ambayo ni misamaha kwa wafungwa. Misamaha hii ambayo inatumika vibaya na vizuri. Gerezani nimekuta kuna wafungwa wazee ambao wamefungwa miaka ya 1970 mpaka leo bado wapo gerezani, lakini Serikali mmekuwa mkitoa msamaha kwa wafungwa wanaofungwa miezi sita, vifungo vidogo. Nataka nimwambie Waziri, nilimwambia tukiwa wawili na leo ninasema mbele ya Bunge, vifungo hivi vya miezi sita, wahalifu wakubwa wa Taifa hili, wanatumia vifungo vidogo kufanya uhalifu wanakuja gerezani, wanakaa kwa muda mchache, halafu wanatoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano mtu anajipa kesi ndogo ambayo anajua atafungwa miezi sita, anajua atakaa miezi mitatu, atapata msamaha. Anakuwa na kesi hiyo mahakamani, anakwenda anafanya tukio kubwa la mauaji au ujambazi ile kesi ndogo inamfunga, anakuwa amejikinga na lile tukio kubwa ambalo amelifanya mtaani. Waziri wa Mambo ya Ndani unatoa msamaha kwa huyu mfungwa pasipokujua umemsaidia kuficha kesi kubwa ambayo alikuwa nayo mtaani.
Kwa hiyo, mnawafunga watu kwa miezi michache mnawatoa, baada ya muda mfupi kumbe walitakiwa wapate msamaha watu wenye vifungo vikubwa, hii ingesaidia kuwafanya watu wenye vifungo vya muda mfupi peke yao waone kwamba hii siyo kinga.
Mheshimiwa Waziri, hili nilikwambia na leo nasisitiza Parole muwe mnaangalia vifungo, msijali kwamba hiki ni kikubwa mkaona hawa hawafai, hawa wenye vidogo basi ndiyo tuwatoe, vidogo vinatumika kuficha maovu makubwa. Kwa hiyo, naomba hili muangalie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ukiwa Ukonga na magereza mengine, nimeshuhudia askari wakifanya njama pamoja na maafisa wa mahakama, wale admission officers wafungwa wanakosa kupata haki zao za kupata Hati za Hukumu pamoja na upande wa mashtaka, kunakuwa na uhusiano mzuri kati ya mahakama pamoja na askari wa admission. Mfungwa akiomba apate nakala ya hukumu akienda kule mahakamani anaambiwa muone askari fulani, askari yule anamwambia mfungwa lazima utoe hela, ndiyo upate hati ya mashtaka na mwenendo wa mashtaka. Hii maana yake ni kwamba askari wako lazima uwaangalie. Vitengo vya Admission vinatenda rushwa, vinazuia wafungwa kupata haki yao, naomba hilo Mheshimiwa Waziri uangalie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu hii programu mnasema ya urekebishaji. Mimi nilipokuwa gerezani nilitegemea ningeona huo urekebishaji mnaousema, kwamba wafungwa mnawarekebisha kwa programu ambayo ni tangible. Nione kuna programu ya urekebishaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ambacho nimekiona sasa sijui kama huu ndiyo urekebishaji wenyewe, nimeona marungu, mfungwa anapigwa marungu mpaka mguu unageuka. Unapigwa rungu mpaka mguu unashindwa kutoka.Nimeona wafungwa wanafanyishwa, labda niseme nilipoingia mara ya kwanza gerezani, askari wako walinikamata wakanipiga mitama, sijafanya chochote nimeingia hapo. Sasa sidhani kama Mbunge naweza nikafanyiwa hivyo wafungwa wa kawaida sijui wanafanywaje na siamini kama huu ndiyo urekebishaji au nilifanyiwa hivyo kwa sababu mimi ni Mbunge wa Upinzania labda, lakini kama hizo ndiyo programu za urekebishaji, vile ambavyo wafungwa wanafanyiwa mle ndani, wafungwa wanauwawa, wanapigwa risasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti,mimi nimefanyiwa mambo ajabu kama hayo katika Gereza la Idete, askari ananiambia nitakuuwa. Sasa naomba Mheshimiwa Waziri uliangalie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nikuambie wewe ni Waziri mpaka wa wafungwa, usifikiri kwamba wewe ni Waziri tu kwa watu ambao wako mtaani, nenda gerezani kasikilize vilio vya wafungwa. Wafungwa wana matatizo makubwa sana nenda kawasikilize, wanavyofanyiwa mambo ya ajabu mle ndani. Nilikwambia tukiwa wawili na leo nakwambia, nenda kasikilize. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoamini kabisa mtu yeyote wa Mungu anajua kabisa vitabu vinasema waonee huruma wafungwa, wagonjwa, walemavu na wajane. Hizi kauli za wamenyeke tu, Mheshimiwa Rais anasema hawa wafungwa wamenyeke hawafai, wafanye kazi mpaka wachubuke,mimi nilifungwa kihuni, nimeonewa, sina kosa, lakini Rais alisema kwamba nimenyeke. Ningekuwa sina Wakili msomi kama Mheshimiwa Tundu Lissu maana yake yake na mimi ningebaki ninamenyeka. Sasa kuna watu wangapi ambao nchi hii wanamenyeka kwa uhuni tu ambao wamefanyiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Waziri, wale wafungwa ni binadamu, wafungwa ni watu. Yeyote aliyepo hapa ipo siku chochote kinaweza kikatokea. Sheria mnazotunga hapa, wakati mimi nasema haya wewe umevaa crown upo juu unafikiri uko sahihi, ipo siku na wewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee tena kuhusu maisha ya askari. Mheshimiwa Waziri nikuulize, hivi leo ukiambiwa uchague, ukae kwenye choo chako au ukae kwenye nyumba wa Askari wa Magereza wa Idete wewe utachagua ukae wapi? Kati ya choo chako wewe Waziri, choo chako wewe Mbunge na chumba cha Askari wa Magereza uambiwe ukae kwa siku moja utakaa wapi?
Utakaa chooni kwako. Nyumba ya askari wa nchi hii wa magereza ni mbaya choo chako ni kizuri. Wabunge vyoo vyenu ni vizuri, vyoo vya askari wenu, na hawa askari pamoja na yote haya mnayofanyiwa, bado sisi ambao tunaongea haya maneno mnatupiga virungu, Mungu anawaona ninyi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Magereza tangu mwaka 2012 mpaka leouniform hawajapewa. Nimekuta askari wanajinunulia wenyewe uniform.Wananiambia Mbunge hii uniform nimenunua mwenyewe kwa fedha zangu na hivi unavyoona hivi haifanani na nguo za askari wengine. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MHE. PETER A. P. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hii siyo fair, package allowance mnawapa askari wengine, wanajeshi wengine mnawapa package allowance leoMagereza wale mpaka leo hamjawapa, kwa nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru lakini askari polisi msitumike vibaya na hawa jamaa, Mungu anawaona.