Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Pauline Philipo Gekul

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Babati Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kunipa nafasi na mimi nitoe maoni yangu katika Wizara hii ya Mambo ya Ndani. Pia ninamshukuru Mwenyenzi Mungu kutupa afya njema, sisi wote katika Bunge hili ili kuishauri Serikali.

Pili, niendelee kuwapa pole wananchi wangu wa Jimbo la Babati Mjini kwa msiba ambao tulipata wa wale watoto ambao walipata ajali na Watanzania wote niwape pole, siku ya leo ni mazishi pale mtaa wa Mrara, Mungu awatie nguvu, ni msiba mzito sana ambao kwa kweli ni kazi kuupokea katika mioyo yetu, lakini Mungu atupe faraja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, haya ninayochangia ni ambayo naona niyaseme kutoka moyoni mwangu. Naomba niseme neno moja la kiswahili kwamba Wabunge tuko hapa kwa ajili ya kusimamia Serikali, lakini kama hatutaacha unafiki toka moyoni, haya malalamiko ya wanajeshi na wananchi wetu hayawezi kufanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema hili kwa sababu unafiki huu tusipouacha tutaendelea kusema Magereza ya Jimboni kwangu, Polisi wa Jimboni kwangu, Zimamoto wa Jimboni kwangulakini wenye matatizo ni sisi Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii bajeti yake ni shilingi bilioni 930, lakini bajeti ya maendeleo ni shilingi bilioni 40, kati ya shilingi bilioni 940 ndio za maendeleo. Waheshimiwa Wabunge tunaongea hapa kinafki, tunaongea tu kwa kupapasa wakati wa kupitisha vifungu tunaongeaongea tunakwenda kwenye guillotine haya hatuyaongei. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatufiki kwenye vifungu, hatuongei kwa dhati ya mioyo yetu na kama tukisimama kuisimamia Serikali niwaombe Waheshimiwa Wabunge wenzangu pamoja na mimi tuache unafiki. Ikifika saa ya kupitisha vifungu tuitake Serikali waongeze fedha za maendeleo kwa sababu kila Mbunge analalamika kuhusu Polisi kwenye Jimbo lake, Magereza kwenye Jimbo lake, Polisi kwenye Jimbo lake, na Jeshi la Zimamoto kwenye Jimbo lake hawana magari, hawana maji na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikifika kwenye kupitisha vifungu tunaenda mtu anatoa shilingi baadaye anarejesha kishkaji, wakati fedha hazipo huku kwenye maendeleo. Kwa hiyo, ni aibu Wizara ya Mambo ya Ndani ambayo inalinda Tanzania, fedha za maendeleo shilingi bilioni 40 wakati wanajeshi wanakaa kwenye mabanzi, kwenye bati ndiyo nyumba zao. Unafiki huu utatupeleka pabaya. Mimi ninawaomba Waheshimiwa Wabunge leo, bajeti hii isipite wanongezewe fedha wanajeshi hawa na magereza na wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpe pole Mheshimiwa Waziri wetu Kivuli Mheshimiwa Godbless Lema, jana alibaguliwa kule Arusha na maeneo mengine. Nimtie moyo tu kwamba ubaguzi huu siyokwa sisi peke yetu, ubaguzi huu upo hata kwa wanajeshi wetu. Nitoe mfano, Jeshi la Magereza katika bajeti hii, hivi tunavyoongea nimeona kwamba Jeshi la Magereza hawajawahi kusikilizwa mambo yao. Niwape mfano, Mheshimiwa Rais mwaka jana mwezi Novemba, alizungumza kuhusu duty free hizi bidhaa ambazo zinapelekwa kwenye majeshi yetu, akasema hizi fedha badala ya kuwaletea vinywaji tutakuwa tunawaletea kila baada ya miezi mitatu shilingi 300,000. Ninavyoongea hapa Jeshi la Magereza hawajawahi kupewa fedha hizi, lakini majeshi mengine wamepewa.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri utuambie kwa nini mnabagua Jeshi la Magereza. Jeshi la Polisi mmewapa Januari, Aprili mmewapa awamu mbili. Jeshi la Wananchi mmewapa mwezi wa Novemba, Desemba, awamu mbili. Jeshi la Magereza hamjawahi kuwapa hizi fedha,kwa nini mnawabagua jeshi hili? Wakati Jeshi la Magereza ndiyo linakaa na wananchi ambao wanaonewa, wanabambikiziwa kesi, wanawalinda wahalifu, wanakaa na watu kule wanawavumilia. Wengine hawa mahabusu na wafungwa mnawapeleka kule.

Mheshimiwa Waziri nimekuwa nikikuambia hawana hata uniform, hawana hata nguo, mnawapeleka mnawafunga. Wafungwa wetu katika magereza nilifanya ziara katika Gereza la Babati, mtu mzima unakwenda pale unapewa suruali na shati la juu tu hakuna nguo nyingine yoyote ni mfungwa huyo! Jeshi hili wanakaa na watu hawa wasiokuwa na nguo mnawapa suruali tu na shati la juu, nguo zingine pull neck na nguo za ndani hamuwapi, halafu watu hawa hawapewi fedha zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu mnaita Jeshi la Magereza mnawapenda, mnawasikiliza, hata kwenye nyumba kwenye kitabu cha development nimekwenda, nyumba zote ambazo mnakwenda kujenga mnafanya renovation ni nyumba za polisi, sina tatizo na polisi wetu lakini Jeshi la Magereza mmewasahau kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atuambie kwa nini ubaguzi huu mnaotufanyia sisi, sasa mnaupeleka kwenye majeshi yetu? Mtakuwa salama vipi? Wewe ni mfungwa mtarajiwa kaka yangu, kesho na kesho kutwa, utakuwa mahabusu pia, uko hapo tu wengine walikuwa hapo na wengine walishaondoka unafahamu, usicheze na Jeshi la Magereza wapelekeeni mahitaji yao na hizi pesa mlizowaahidi muapelekee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo niliseme, hizi shilingi bilioni 40 ambazo ninasema tusipoacha unafiki, ndiyo hizi ambazo zinatakiwa ziende kwenye maendeleo. Wafungwa na mahabusu wapate magodoro. Gereza la Babati wafungwa wetu na mahabusu wanalala kwenye magodoro kama slice za mikate. Wanaunganishaunganisha vipande vya magodoro halafu havitoshi wanalala chini. Ukitaka kwenda kupeleka pale mlolongo ni mrefu mpaka uende Magereza Makao Makuu. Mkuu wa Gereza pale hatakuruhusu kupeka hivyo vitu mpaka uandike barua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama mnaleta mlolongo kwa nini hamnunui vitu hivyo? Magodoro hamnunui, uniform hampeleki lakini pia hata chakula ration wanazokula hazitoshelezi! Mtuambie ni kwa nini hizi fedha za maendeleo msiongeze kwa sababu kila mmoja ni mfungwa na mahabusu mtarajiwa. Hakuna magodogo huko.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mwigulu alifika babati, alifika pale Jeshi la Polisi, nashukuru alienda pale rangi ikapigwa pigwa kwa sababu alienda pale, lakini nilimweleza masuala ya Gereza la Babati, hali ni mbaya na Magereza ya nchi nzima hali ni mbaya, hata magodoro hakuna. Ni vizuri tukakubaliana kwamba fedha hizi ziongezwe.Mfano, Jeshi la Magereza wanatakiwa nyumba 10,526 asilimia 71 hizi nyumba hazipo.Achilia mbali Magereza wanakokaa, lakini asilimia 71 ya Jeshi la Magereza hawana hizo nyumba.Polisi hawana hizo nyumba, Wilaya tano tu ndiyo mmeweka katika bajeti hii. Hivi kweli Waheshimiwa Wabunge tukae tu tunalalamika, kwamba jimboni kwangu, jimboni kwangu, nafikiri hili tulichukue kama Wabunge. Kwamba Wizara hii tunataka fedha za development angalau hata bilioni 200 ili tuache kelele za nyumba za Polisi wetu, tuache nyumba zetu za Magereza zijengwe, vinginevyo mnatuachia mzigo mkubwa sana na hili halitokubalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la Magereza Wilaya moja kutokuwa na Gereza. Mfano, Babati pale tuko Makao Makuu ya Mkoa, lakini wenzetu wa Hanang’ hawana gereza tunaletewa mahabusu, gereza la Babati sasa lina watu zaidi ya 400 wafungwa pamoja na mahabusu, wanakaa mahabusu wa Hanang’ wiki tatu hawapelekwi Mahakamani, OCD wa Babati na wa Hanang’ hawana mafuta, Polisi wetu hawa wamewaachia mzigo mkubwa sana, kwenye ziara zao wakubwa wakija pale, wanawaambia watafute magari, wanaanza kuomba matairi yako wapi, mafuta yako wapi, hata fedha hawapeleki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanashindwaje kujenga Gereza Hanang’ wanarundika pale, watu wanasukumana pale, chakula hakitoshi, hawapelekwi Mahakamani, wanakosa haki zao. Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujibu, naomba nifahamu na atuunge mkono kwa kweli, siyo baadaye aseme hela hazitoshi wakati anajua Hanang’ hakuna gereza, Babati msongamano ni mkubwa kwenye Gereza letu la Wilaya. Atuambie ni lini la Hanang’ litajengwa ili wananchi wa Babati wanapoingia kwenye lile Gereza, wasisongamane kiasi hicho kwa sababu hizi fedha hazitoshi na yeye atuunge mkono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine suala la Zimamoto. Jeshi la Zimamoto wanafanya kazi nzuri na wanakusanya…

TAARIFA...

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru nisaidie tu kulinda muda wangu. Naomba nipokee taarifa ya Mheshimiwa Nagu ni dada yangu, naomba tu nikwambie dada ulikuwa haujalisemea ndiyo maana mpaka leo hakuna Gereza, kwa hiyo acha nikusaidie mdogo wako nikusemee.