Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kikwajuni
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nianze kutumia fursa hii kumshukuru sana kwa mara nyingine Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuendelea kuniamini kwenye majukumu haya muhimu. Naomba nitumie methali ya wahenga fupi tu ambayo inasema kwamba imani huzaa imani, mimi na Mheshimiwa Waziri ambaye kwa kweli amekuwa akinipa ushirikiano wa hali ya juu na msaada mkubwa sana katika kutekeleza majukumu yangu, tutaendelea kuchapa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu muhimu wengi kweli wa kuwashukuru lakini kwa kuwa muda ni mfupi, naomba moja kwa moja niende katika hoja za Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wamechangia mambo mengi sana, wengine kwa kuzungumza na wengine kwa maandishi. Kwa muda huu inawezekana siyo hoja zote za Waheshimiwa Wabunge tutakazoweza kuzipatia majibu, lakini zile ambazo hazitapatiwa majibu kwa njia ya kuzungumza tutawapatia majibu kwa njia ya maandishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na hoja ya suala la usalama barabarani. Leo hii tunazungumzia changamoto ya usalama barabarani katika nchi yetu katika kipindi ambapo Taifa tumepata msiba mkubwa sana wa ajali ya basi lililojeruhi na kuua watoto na vijana wetu ambao walikuwa wana shughuli za masomo. Naomba Mwenyezi Mungu atupe moyo wa subira pamoja na wazazi wa watoto hawa katika kipindi hiki kigumu. Wakati tukiendelea kuomboleza msiba huu mzito, inaweza ikawa vigumu sana kueleza kwamba katika eneo hili la usalama barabarani tumefanya kazi kubwa sana katika kipindi cha mwaka mmoja na tumefanikiwa kwa kiwango cha kuridhisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kufikisha azma yetu hii ya kupunguza ajali za barabarani kuna hatua kadhaa tulizichukua. Moja katika hatua ambazo tulichukua tulianzisha mkakati kabambe wa miezi sita ambao ulikuwa na lengo la kupunguza ajali za barabarani kwa asilimia kumi. Kiukweli mkakati huo umefanikiwa kwa kiasi cha kuridhisha ingawa tumegundua changamoto nyingine za hapa na pale ambazo tutazifanyia kazi. Mkakati huu ulizingatia mambo makubwa matatu ambayo ni vyanzo vya ajali barabarani ambavyo vinasababishwa na makosa ya kibinadamu, ambapo mara nyingi makosa haya yanatokana na uzembe wa madereva wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ni kwa asilimia ndogo ni changamoto ya miundombinu yetu na changamoto ya ubovu wa magari. Kwa hiyo, mkakati wetu ambao ulilenga maeneo 14 zaidi uliangalia maeneo hayo matatu. Leo hii nimesimama hapa mbele yako na mbele ya Waheshimiwa Wabunge kuelezea tathmini kwa ufupi ya mafanikio hayo ambayo tulilenga kupunguza asilimia kumi ya ajali katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kukamilika kwa mkakati ule wa miezi sita tumefanikiwa kupunguza kwa upande wa ajali za magari ambazo zinasababisha madhara makubwa, tumefanikiwa kupunguza ajali za vifo kwa asilimia nane, hatukufikia asilimia kumi lakini tumekaribia, asilimia nane. Katika ajali za majeruhi tumevuka viwango na kufikia asilimia 13. Kwa upande wa pikipiki tumefanikiwa kupunguza ajali kwa asilimia 17 zile ajali ambazo zinasababisha vifo lakini kwa majeruhi wa pikipiki hatukufanya vizuri sana na ajali ziliongezeka kwa asilimia mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla ukiangalia utaona kwamba kwa kiwango kikubwa ajali hizi zimefanikiwa kupungua katika kipindi hiki cha miezi sita. Mkakati huo wa miezi sita ndiyo uliopelekea mafanikio ambayo leo hii tunajivunia kipindi cha mwaka mmoja wa kupunguza ajali kwa asilimia 7.2.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto mbalimbali ambazo tunakabiliana nazo, najua eneo hili limeguswa na Waheshimiwa Wabunge wengi, nitawataja baadaye ambao wamechangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa changamoto ambazo tumekabiliana nazo kama ambavyo baadhi ya Wabunge waliochangia wamezungumza, moja ni changamoto ya sheria yetu tuliyonayo sasa hivi, ambapo baadhi ya mambo yanahitaji kufanyiwa marekebisho. Kuna mambo machache ambayo nitayataja kwa haraka. Kwanza kunahitajika kuongeza ukali wa adhabu katika sheria yetu, vilevile kunahitajika kuongeza idadi na aina ya makosa ambayo hayamo katika sheria ya sasa hivi. Kwa hiyo, katika mambo 14 ambayo tumeyaangalia moja lilikuwa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengine ambayo tumeyaangalia na Waheshimiwa Wabunge wameyazungumza kwa uchungu kabisa, kwamba kuna tatizo kuhusu Askari ya Barabarani, wengine wamefika mpaka kusema Askari wanakaa juu ya miti. Tuna changamoto moja ya kisheria, lakini kuna changamoto vilevile nyingine ya kimfumo wa nchi yetu. Tunapozungumza sasa hivi tunatumia mfumo ambao tumeingia mkataba na kampuni binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mkakati wetu tulikusudia kwamba tuweze kutumia utaratibu wa nukta, kwamba mtu atakapokuwa amefanya makosa aweze kupunguziwa points na baadaye ikiwezekana leseni yake ipunguzwe. Mkakati huu umeshindwa kufanikiwa kwa sababu ya utaratibu wa huu mfumo tulionao. Tunatarajia baada ya mkataba huu kumalizika Juni tutaingia katika mfumo ambao umeandaliwa na Jeshi la Polisi, mfumo huu tunatarajia kuoanisha na mfumo unaotumika TRA ili tuweze sasa kutumia utaratibu wa nukta na hii itasaidia sana kuweza kupunguza ajali za barabarani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna changamoto ya matumizi ya teknolojia ambayo Waheshimiwa Wabunge wamezungumza. Hili ni jambo ambalo katika mkakati wetu wa awamu ya pili tunatarajia kuanzisha na tutalipa kipaumbele ikiwemo utaratibu wa kuweza kuweka vidhibiti mwendo badala ya kutumia hizi tochi za sasa hivi ambazo zinatumika barabarani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kuna mambo mengine ambayo yamezungumzwa kuhusiana na changamoto za Askari wetu wa barabarani. Nataka tu nichukue fursa hii kutoa takwimu za haraka kwamba kuna Askari wengi sana ambao katika kipindi cha mkakati huu katika mambo 14 tuliyoyazungumza kwamba tutahakikisha tunashughulikia wale ambao wanakiuka maadili wakati huo huo tunawapongeza wale ambao wanafanya vizuri. Kuna orodha ndefu ya Askari ambao wamefanya kazi vizuri na kuna orodha ndefu yaAskari ambao tumewapongeza ambapo mara nyingi hawa ambao wanafanya kazi nzuri ambao ndiyo wengi huwa hawaonekani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kulizungumzia ni kwamba tunatarajia kuanzisha awamu ya pili ya mkakati wetu wa kupunguza ajali, baada ya kuona mafanikio na upungufu ambao nimeuzungumza, sasa hivi tunajikita zaidi katika kuangalia utaratibu wa aina ya madereva waliopo nchini mwetu. Leo hii naomba nichukue fursa hii kukazia maagizo ya Mheshimiwa Makamu ya Rais aliyoyatoa juzi kuhusiana na kuhakikisha kwamba ukaguzi wa kina unafanyika kwa upande wa madereva ya mabasi ya wanafunzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nichukue fursa hii kutoa maagizo hapa kwa Jeshi la Polisi kuanza operesheni maalum ya kusaka na kukagua mabasi ya wanafunzi pamoja na madereva ambao wanaendesha magari haya ili sasa hivi tuweze kuona kwamba eneo hili ambalo lilisahaulika kwa kiasi fulani, liweze kupewa kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumzia hali ya usalama barabarani, naomba sasa niingie katika hali ya kisiasa kwa ujumla wake. Upande wa hali ya kisiasa nchi yetu ipo salama juu ya matukio na changamoto za hapa na pale, hali ya usalama kwa ujumla katika nchi yetu ni ya kuridhisha. Tumepita katika kipindi kigumu sana, katika kipindi cha mwaka mmoja nchi yetu imekumbana na majaribu mbalimbali na ninyi ni mashahidi. Tumeweza kuona matukio ya uhalifu ya aina yake ambayo yametokea kule katika Mikoa ya Mwanza, Tanga, maeneo ya Mbagala na mengine ambayo yamehusisha mpaka uuaji wa Askari wetu. Yote haya ambayo yamejitokeza katika kipindi cha nyuma tuliahidi hapa Bungeni kwamba tutashughulika nayo na tumeshughulika nayo kwa mafanikio makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ambayo inaendelea kujitokeza sasa hivi katika Mkoa wa Pwani, nina hakika tutafanikiwa kuweza kudhibiti hali ile na hali ya usalama iweze kurudi kama kawaida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kusisitiza vilevile jambo lingine la muhimu sana na la msingi kwamba katika kufanikisha lengo hili ni lazima wananchi watoe mchango mkubwa, wananchi ndiyo ambao wanakaa na jamii na wahalifu huko. Kwa hiyo, bila kulisaidia Jeshi la Polisi kazi hii inaweza isiwe na ufanisi mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya usalama Zanzibar; Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumzia jambo hili, kimsingi ni kwamba hali ya usalama Zanzibar nayo ni shwari. Nilisikitika sana nilipofanya ziara kama ambavyo baadhi ya Waheshimiwa Wabunge nilipotembelea Majimbo yao akiwemo Mheshimiwa Mwantakaje kuona kwamba katika Zanzibar ambayo naifahamu mimi kuna baadhi ya maeneo yalikuwa hawezi kupita raia. Nachukua fursa hii kulipongeza sana Jeshi la Polisi kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya kuweza kuhakikisha maeneo yale yanaendelea kurudi katika hali ya kawaida na wananchi wanafanya kazi zao kwa usalama na amani. Kwa hiyo, hali ya usalama kwa ujumla katika nchi yetu inaendelea kuimarika na itazidi kuimarika zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine ambalo limezungumzwa; suala hili la mgogoro wa Chama cha CUF. Hapa hatuwezi kupoteza muda kuzungumza migogoro ya Vyama vya Siasa, hiyo siyo kazi yetu. Jeshi la Polisi linafanya kazi yake kwa mujibu wa sheria, weledi na maadili. Kama kuna vyama ambavyo labda maji yapo shingoni migogoro yao imewashinda wenyewe kwa wenyewe wanatafuta mtu wa kumsuluhisha, siyo kazi ya Jeshi la Polisi. Jeshi la Polisi kazi yake ni kusimamia sheria, ndiyo maana nasema kwamba matukio ambayo yametokea ya ugomvi wa vyama vya siasa wenyewe kwa wenyewe hatuwezi tukaruhusu umwagaji wa damu wa raia yeyote. Kama mna migogoro yenu, mtafute njia sahihi ya kuirekebisha. Anapotokea mfuasi wa chama chochote, iwe ndani ya chama hicho hicho anawasilisha taarifa kwa Jeshi la Polisi juu ya mwelekeo wa uvunjifu wa amani, Jeshi la Polisi haliwezi kuruhusu hiyo hali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inashangaza sana, kwamba leo asubuhi nimeangalia TV Channel Ten, nimeona kwenye taarifa ya habari ya Channel Ten leo hivi asubuhi kwamba Chama cha CUF, wamefanya mkutano wa hadhara uliovyoelezwa na Waandishi wa Habari kwa mujibu wa TV ya Channel Ten, wamefanya mkutano wa hadhara na mazingira yameonesha ni mazingira ya maandamano. Nataka nimuagize IGP hapahapa kulichunguza hilo jambo. Tumepiga marufuku mikutano ya hadhara isipokuwa kwa Wabunge wa Majimbo hayo, tumeona watu wamekusanyika wameenda kufanya mikutano ya hadhara, hilo jambo lazima lichunguzwe na hatua stahiki zichukuliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sipo hapa kujibu hoja za Mheshimiwa Khatib maana marehemu Bibi yangu alinifundisha hadithi moja kwamba kama umeenda kuogelea baharini halafu akatokea mwendawazimu akachukua nguo zako huwezi kumkimbiza, wewe utaonekana mwendawazimu zaidi. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la Magereza. Katika jambo ambalo ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais ambalo ni aibu kwamba kwa idadi ya nguvukazi ya wafungwa tulionao na kwa idadi ya rasilimali ya mashamba makubwa tuliyonayo katika maeneo ya Magereza haiwezekani hata siku moja, hatuwezi kukubali chini ya uongozi wa Wizara hii ikiwa Mheshimiwa Mwigulu ni Waziri na mimi Naibu Wake namsaidia, kuona kwamba jambo la Wafungwa kuendelea kula bure, hali ya kuwa tuna mashamba yenye nafasi ya kutosha na tuna rasilimali na nguvukazi ya kutosha. Tumejipanga vizuri katika hilo kuhakikisha kwamba utegemezi wa chakula katika Magereza yetu unapungua kama siyo kwisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya idadi ya Magereza yetu ni 129 ambayo yana jumla ya ekari zaidi ya 300,000. Miongoni mwa Magereza haya, ya kilimo ni 48 ambayo yana takribani ekari zaidi ya 150,000. Kuna mikakati kadhaa ambayo tumeichukua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja; tumejaribu kuangalia uwezekano wa kuwavutia Wawekezaji waweze kushirikiana na Jeshi la Magereza kuzalisha. Nichukue fursa hii kuyapongeza sana mashirika yetu ya pensheni, leo tunapozungumza hapa Gereza la Mbigiri tayari wameshaingia mkataba na NSSF katika kuzalisha siyo tu miwa vilevile kuanzisha kiwanda cha sukari. Wakati jitihada hizo za kuvutia wawekezaji werevu zikiendelea, tunaendelea kuhakikisha kwamba Magereza ambazo zipo karibu na mito tunaanzisha kilimo cha umwagiliaji kama ambavyo tumefanya katika baadhi ya Magereza mfano, Idete, Morogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi tuna mpango katika kipindi chetu hiki cha mwaka mmoja unaokuja kuhakikisha kwamba tume-earmark Magereza 11 kwa ajili ya kuzalisha pamoja na mifugo katika kilimo cha mpunga, mahindi na mawese. Matarajio yetu ni kwamba tuzalishe takribani tani 13,260 kwa kutumia Magereza hayo ambayo tumeyachagua. Mahitaji ya sasa hivi ya chakula kwa wafungwa ni takribani tani 10,740, tutakapozalisha tani 13,260 tuna uwezo wa ku-cover mahitaji yote ya wafungwa, wakati huo tukaweza kuwa na chakula cha ziada cha takribani tani 2,500.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kutusaidia kupata matrekta 50 ambayo mchakato wake umeshaanza, kati ya hayo matrekta 50 yatakayopatikana yatasaidia kuhakikisha kwamba mpango wetu huu wa kuhakikisha kwamba Magereza yanajitegemea kwa kilimo unafanikiwa, leo hii matrekta matatu tayari yapo katika Gereza la Mbigiri kwa ajili ya shughuli za kilimo cha miwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na maagizo ya Mheshimiwa Rais kwamba wafungwa wafanye kazi, tumehakikisha kwamba tumefanya kazi hiyo na mafanikio yake ni makubwa sana. Siyo tu kwamba wafungwa hawa watashirikishwa katika kilimo, leo hii Mheshimiwa Rais ametoa shilingi bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za Magereza Ukonga, leo hii nimesimama hapa nikiwa nimefarijika sana, kwamba tumefanikiwa kuokoa takribani nyumba 80 za ziada kwa kuwatumia wafungwa, jambo ambalo pengine tungetumia utaratibu mwingine nyumba hizi 80 tusingeweza kuzipata kwa ajili ya nyongeza ya Askari wetu. Kwa hiyo, hiyo ndiyo faida ya kutekeleza maagizo ya Mheshimiwa Rais ya kuhakikisha kwamba wafungwa tunawatumia ipasavyo siyo tu kwa kuzalisha lakini kwa kusaidia kuwajengea uwezo ili waweze kwenda kujitegemea watakapotoka huko kwenye Magereza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kana kwamba hiyo haitoshi, tayari tuna programu mbalimbali za kurekebisha wafungwa katika Magereza yetu mbalimbali ambayo sina haja ya kuyataja kutokana na muda kwani yapo mengi. Katika bajeti yetu ya mwaka huu tumewekeza takribani shilingi bilioni 2.2
ambazo zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kuimarisha viwanda vidogovidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia ushiriki wa Magereza katika uchumi wa viwanda hatuzungumzii viwanda vikubwa tu, mpaka viwanda vidogovidogo, tunapozungumzia viwanda vya karanga Mbigiri, lakini wenyewe ndani ya Magereza kuna viwanda kwa mfano, katika bajeti hii katika fedha hizi tunatarajia kuanzisha kiwanda cha helmet pale Ukonga, kiwanda cha useremala Isanga, Dodoma, kwenye kambi ya Kimbiji tunatarajia kununua mashine vilevile kwa ajili ya kiwanda cha kuzalisha mawese, pamoja na Gereza la Lindi - Machole ambapo kuna kiwanda cha chumvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na muda, naomba niende kwenye Jeshi la Zimamoto. Jeshi la Zimamoto jambo kubwa na la msingi ambalo tunaliwekea kipaumbele ni kuhakikisha kwamba tunapata kwanza vifaa vya kutosha ili tuweze kudhibiti majanga ya moto yanapotokea, pia vifaa hivi viweze kuenea katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu hasa katika Wilaya ambapo huduma hii haijafika. Hivi sasa kuna huduma ya Zimamoto katika mikoa yote lakini kuna wilaya nyingi ambazo bado huduma hii haijafika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii katika kipindi cha mwaka mmoja tunajivunia mafanikio makubwa kwamba, tumeweza kuanzisha Zimamoto katika Ofisi za Wilaya takribani nne ikiwemo Ruangwa, Ukerewe, Ileje na Rungwe. Nilipokwenda Ruangwa na Rungwe tuliwaahidi kwamba tutawapatia gari. Bahati mbaya zile gari tulizoahidi zimepata changamoto lakini hii ahadi iko palepale, gari nyingine zitakapofika kipaumbele kitaelekea katika maeneo ambayo tumetoa ahadi ili yaweze kusogeza nguvu na jitihada ambazo tayari zimeoneshwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi wakati mkakati huu wa kueneza huduma ya Zimamoto Wilayani unaendelea, tunaanza kupeleka huduma ya elimu katika wilaya zetu, kuhakikisha kwamba tunatafuta Askari kwa ajili ya kupeleka elimu ya kinga na tahadhari ya moto. Hilo jambo limekuwa likifanyika kwa mafanikio makubwa katika maeneo mbalimbali nchini na tunaomba Waheshimiwa Wabunge watuunge mkono.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli ni kwamba katika bajeti hii tumetenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa magari manne, kuna mkakati kabambe utakapofanikiwa wa kupata mkopo wa fedha zitakazosaidia kupata vifaa vya kisasa kupitia mkopo wa Benki ya KBC chini ya kampuni ya Smart ambayo mazungumzo yanaendelea vizuri. Tunatarajia katika mpango huu kununua magari 21 pamoja na vituo vitatu vya kisasa vya zimamoto na uokoaji katika Jiji la Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunatarajia kuingia mkopo mwingine waEuro milioni tano ambapo unatarajia kutolewa na Serikali ya Austria kupitia Raiffeisen Bank ambapo tunatarajia kununua magari pamoja na vitendea kazi vingine. Kwa hiyo, utaona kwamba kuna jitihada kubwa ambazo tumezichukua katika kuhakikisha kwamba tunaimarisha vitendea kazi katika Jeshi la Zimamoto pamoja na kuweza kusogeza huduma hizi karibu na wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nizungumzie Mamlaka ya Vitambulisho (NIDA). Kabla sijazungumzia Mamlaka ya Vitambulisho (NIDA), kabla kengele yangu haijalia, naomba nichukue fursa hii kuwatambua kwa haraka, maana niwatendee haki Waheshimiwa Wabunge wametoa michango mizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumzia hoja ya usalama barabarani ambayo Mheshimiwa Lucy Owenya, Mheshimiwa Mbaraka Dau, Mheshimiwa Balozi Adadi Rajab, Mheshimiwa Maulid Mtulia, Mheshimiwa Dkt. Immaculate Semesi, Mheshimiwa Leah Komanya, Mheshimiwa Mwita Waitara, Mheshimiwa Oscar R. Mukasa, Mheshimiwa Raza, Mheshimiwa Risala Kabongo, Mheshimiwa Zainab Mussa Bakar, hawa walichangia wengine kwa maandishi na wengine kwa kuzungumza hii hoja ya usalama barabarani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa hoja ya hali ya kisiasa, Mheshimiwa Katani Katani, Mheshimiwa Khatib Said Haji, Mheshimiwa Makilagi, Mheshimiwa Bobali, Mheshimiwa Faida, Mheshimiwa Khalifa Mohamed Issa, Mheshimiwa Maftaha, Mheshimiwa Sofia Mwakagenda, Mheshimiwa Mnyika, Mheshimiwa Mtolea, Mheshimiwa Rhoda Kunchela na Mheshimiwa Mwantakaje pamoja na Mheshimiwa Ali King walichangia kwa kiasi fulani kwa maandishi na kwa kuzungumza hoja ya hali ya kisiasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya Magereza wachangiaji walikuwa ni wengi vilevile; Mheshimiwa Japhet Hasunga, Mheshimiwa Rashid Shangazi, Mheshimiwa Risala Kabongo, Mheshimiwa Esther Matiko, Mheshimiwa Gekul, Mheshimiwa Mkuchika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika hii hoja ambayo nimemaliza nayo muda huu mfupi uliopita ya zimamoto; Mheshimiwa Sophia Mwakagenda, Mheshimiwa Japhet Hasunga, Mheshimiwa Maftaha Nachuma, Mheshimiwa Juliana Shonza, Mheshimiwa Shaabani Shekilindi, wote hawa walichangia hii hoja ya zimamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa hii hoja ambayo namalizia sasa hivi ya NIDA, kuna wachangiaji wawili ambao walichangia kwa maandishi, Mheshimiwa Magdalena Sakaya na Mheshimiwa Bobali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuwatambua Waheshimiwa Wabunge kutokana na michango yao mizuri, naomba sasa nimalizie kwa haraka hoja ya Mamlaka ya Vitambulisho (NIDA). Kuna hoja mbili kubwa ambazo zilizungumzwa. Moja, ni kwamba malengo hayajafikiwa, tulikuwa tuna target ya kufikia malengo ya kusajili watu zaidi ya milioni 22, mpaka mwezi wa Machi tumesajili zaidi ya watu milioni nane, wakasema kwamba inakuwaje hali hii inajitokeza wakati tayari tumeshapata BVR kutoka Tume ya Uchaguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli ni kwamba BVR za Tume ya Uchaguzi zina changamoto zake. Kwanza BVR za Tume ya Uchaguzi zinatambua taarifa zisizozidi 40 wakati taarifa ambazo zinahitajika kutumika na mfumo wa NIDA ni taarifa 72, hilo moja. Hata quality ya picha nafingerprints kwa upande wa mfumo huu wa BVR…
(Hapa muda kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.