Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza kabisa niwapongeze Wabunge wa Afrika Mashariki wanawake waliochaguliwa jana, na bila kujali itikadi zetu tukiungana katika mambo ya msingi, tutakuwa tunaitendea haki nchi yetu. Pili, nipongeze kabisa jitihada zinazofanywa na Jiji la Dar es Salaam kwa kudhibiti huo wizi ambao umesemwa na aliyenitangulia chini ya UKAWA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa kama ambavyo tumeungana jana na kuweka historia ya kuwapeleka Wabunge wanawake wengi kwenye Bunge la Afrika Mashariki, ninaamini tutaungana tena kuibana Serikali kuhakikisha tunaitendea haki bajeti hii ya maji ambayo ukizungumzia watu ambao wanaumia katika suala zima la kutafuta maji ni mwanamke. Ninaamini tutaacha itikadi zetu pembeni ili tulitendee haki Taifa letu na tuwatendee haki wanawake wa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina sababu kubwa za kusema hivi. Waheshimiwa Wabunge mwaka jana zilitengwa shilingi bilioni 937 fedha za maendeleo ni shilingi bilioni 915, zilizotoka ni asilimia 19 tu ya zaidi ya shilingi bilioni 900. Sasa tujiulize tupo kwenye kipindi hiki ambacho leo hii Waziri na Naibu wake shemeji yangu wanaomba tupitishie hapa bajeti. Hiyo asilimia 81 mtaileta lini kuwatendea haki watanzania na wanawake wa Taifa hili? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaposema tunaikataa bajeti naunga mkono hoja ya Kambi Rasmi ya Upinzani si kwamba tunawachukia, si kwamba hatutaki maji, no, tunaitaka Serikali na tunamtaka Waziri wa Fedha aende afanye anavyofanya mkae mjipange upya mjue sasa mtakapopata fedha mtuletee ili sasa sisi wanawake na wanaume wote na Waheshimiwa Wabunge wote ndio tuungane kuipitisha bajeti yenu. Haiwezekani tunasema tuna mkakati wa kuhakikisha tunamtua mwanamke ndoo ya maji kichwani mijini na vijijini, halafu mpaka leo zaidi ya asilimia 81 haijaenda kwenye Wizara ya Maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nilishasema nitasema ukweli, fitina kwangu mwiko. Nakupenda shemeji yangu na nakupenda mzee wa site, katika hili kwa sababu ninawapenda ninahitaji asilimia 81 mpate Serikali iende ikakae, ikatafute pesa iwape. Kuunga mkono hapa siwezi nikawapaka mafuta kwa mgongo wa chupa, hiyo si desturi yangu mimi. Si desturi yangu na kama mama, kama mwanamke na kama Mbunge wa Jimbo ambaye Jimboni kwangu..., nimesoma kitabu chako umeweka, umetenga hela. Mwaka jana ulitenga na miaka kumi iliyopita huo mradi ulikuwepo yaani leo wana Bunda kama ni birthday ni birthday ya kuanzishwa mradi wa maji kwa miaka kumi bila kupata maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa biashara ya kutenga pesa ambazo hazifiki na kila siku nimekuwa nikisema mkandarasi huyo ni mwizi, amekataliwa Kigoma na Rorya. Mimi nilisema simtaki alienitangulia akawa ananibishia, wananchi wa Bunda wakasema mwana Bulaya jaga, nimekuja.

Mheshimiwa Naibu Spika, wizi sitaki jimboni kwangu; wizi jimboni kwangu sitaki, silindi wezi, ninachotaka mimi ni maslahi ya wananchi wangu kwanza.

Mheshimiwa Waziri huyo mkandarasi ana madeni mengi, mkiweka hela kidogo badala ya kwenda kufanya shughuli za kukamilisha ule mradi wa maji ambao sasa hivi una miaka kumi haukamiliki, halafu mimi leo nije hapa hata kama nakupenda kiasi gani siwezi kukubali kuja kuunga
mkono wakati wananchi wangu wanaona tu mwaka wa kumi sasa hivi mradi wa maji haujakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri yetu ni changa lakini Mamlaka ya Maji Bunda ni class c, inapaswa kupata ruzuku Serikalini na ndiyo maana wanashindwa kulipa bili ya maji kwa sababu hampeleki fedha kwa mujibu wa taratibu anahitaji kupata ruzuku. Kwa sababu kuna neno kata, wanakata! Nilimuomba kaka yangu nashukuru umenisaidia na baba yangu Muhongo. Neno kata linatumiwa vibaya. Mnashindwa kupeleka fedha wakisikia kata wanakata bila kujua wanaathiri mamia ya wanawake na maelfu ya watanzania kwa kukosa huduma ya maji hicho kidogo ambacho kinapatikana, please! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine nadhani kwenye Hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani mmeambiwa kuna miradi hewa, nendeni mkaishughulikie kule, mkichelewa mimi nitawaumbua. Nilishasema kule kwa kaka yangu Mheshimiwa Bonny, mradi ule wa Mgeta – Nyangalanga amepewa mtoto wa mpigakura wangu senior, kala milioni 800 haujakamilika wakawa wanalazimisha apokelewe kinguvu, Makalla alikataa wakataka kumtumia DC nikamwambia wewe utaondoka wewe mradi hautapokelewa, haukupokelewa. Shughulikieni hawa wezi, msipowashughulikia nitawaumbua hapa, sicheki na mtu mimi.

Mheshimiwa Naibu Spika, wizi Jimboni kwangu sitaki. Mradi wa Mgeta, shughulikieni. Wizi, conflict of interest, unatoa tender kwa mtoto wako, hana vigezo, kakataliwa maeneo kibao mpaka Mtwara kule, ondoeni wizi, nimesafisha mtu sitaki na mtoto wake, nataka mambo yangu yaende vizuri ili wananchi wangu wapate maendeleo kupitia binti yao, Ester ngw’ana Bulaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, naomba sana Mheshimiwa Waziri, mzee wa site na shemeji yangu wa Kantalamba, sana, mbali ya kwamba kuna hii miradi mingine imeanzishwa kama kule Rwabu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Muda wako umekwisha Mheshimiwa Ester Bulaya.