Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Kavuu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kuchangia katika hotuba ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji ambayo ni muhimu sana katika maendeleo ya binadamu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba niwaaminishe ndugu zangu wa Kambi ya Upinzani kwamba CCM haijachoka kubeba mzigo, CCM ni kama tembo, tembo hachoki kubeba mkonga wake na wale wanaofikiri itatoka madarakani ni ndoto za mchana. Sasa niwaombe tu kwamba tuwe wavumilivu na Serikali hii makini inayotekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili naomba niendele kuwaomba ndugu zangu wa Kata ya Kasansa na Mamba wawe wavumilivu kwa mvua zinazoendelea na pili waweze kuchukua tahadhari kwa ajili ya kujinusuru na maafa yanayoweza kutokana na mafuriko; na mafuriko yale niliwahidi nayashughulikia na niko mbioni kukamilisha ili nikawatembelee.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishukuru Serikali yangu na niishukuru Wizara hii ya Maji, katika bajeti ya mwaka uliopita imeweza kunisaidia angalau nusu ya jimbo langu kupata maji. Vijiji vya Kashishi, Chamalendi, Mwamapulu, Ukigwamizi, Msadya, Maimba, Ikulwe, Kaunyala, Minyoso, Ntompola, Mkwajuni, Lichima, Kibaoni, Nyambwe, Lunguya, Ilalangulu, Mawiti karibu kote huko nimepata visima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo nililonalo gari la kuchimbia liko moja, kwa hiyo, naomba mniongezee magari angalau mawili ili tuweze kumaliza tatizo hili mara moja. Nirudi pale pale kwenye kata yangu ya Kibaoni, tuna mradi mkubwa na kisima kikubwa pale cha maji. Niliomba mnitafutie wataalam kuja kuangalia kisima pale tatizo ni nini sijapata taarifa, naomba nipate taarifa na nijue status ya pale kwa sababu kile kisima ndicho kinachosambaza maji katika kata ya Kibaoni nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niungane na wenzangu wote waliotanguliza kusema sasa tuongeze tozo kutoka ile shilingi 50 tupate shilingi 100 na ikiwezekana 150 ili wananchi vijijini wapate maji safi na salama, maji ya kutosha na yawe endelevu isiwe kwamba yakifika kipindi cha kiangazi maji yanakuwa yanakauka hapana, tunaomba namna ambavyo tutafanya miradi yetu hii iwe endelevu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nirudi tena kwenye mradi wangu wa umwagiliaji wa kata ya Mwamapuli, humu sijaona umetengewa fedha yoyote. Skimu ya Mwamapuli naomba nipate status yake. Katika bajeti iliyopita mliniambia mmenitengea karibu shilingi bilioni moja kwa ajili ya upembuzi yakinifu.
Kwa hiyo, ninaomba sasa kama upembuzi yakinifu mmeshafanya mniambie, kama ni pesa mtanipa kutoka kwenye hiyo asilimia tutakayoongeza ndiyo yenye uhakika zaidi naomba mnifikirie katika mradi huu, ni mradi wa Kitaifa kwa hiyo naomba muutafutie pesa ili tuweze kupata.
Mheshimiwa Naibu Spika, pale tumeshakufungua maghala manne na tuna mashine ya kisasa ya kuchambulia Mpunga. Sasa ile mashine inakaa bure pamoja na yale maghala yanakaa pale bure. Sasa naomba mradi huu uanze mara moja ili wananchi wanufaike na kazi walizojitolea za asilimia 20 za kuchangia maendeleo katika kujenga miradi ile. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niseme neno moja. Wapo wenzangu waliotangulia kuzungumza kwa kusema kwamba tupunguze tutoe hela kwenye REA, hapana. Si vijiji vyote vimekwishapata umeme, naomba ile tozo ya kwenye REA ibaki vilevile, tuhakikishe vijiji vinapata umeme. Nimekuwa nikilia kila siku na Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini, kata zote zilizoko Jimbo la Kavuu pamoja na kata zote zilizoko Jimbo la Kwela kwa Mheshimiwa Malocha hakuna umeme hata kijiji kimoja. Jimbo la Kavuu lina umeme kata ya Kibaoni na Usevya center tu, Usevya ni nyumba kumi.
Kwa hiyo, ninaomba sana kwa sisi tunaotoka majimbo ya vijijini hii hela tusikubali ipunguzwe. Lazima tuhakikishe inapatikana tena kwa wingi na wananchi kule vijijini wana enjoy haya matunda ndugu zangu. Tusiwe wachoyo watu wa mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vijijini ndio kwenye nguvu kazi kubwa, ndiko tunakotoa chakula na nimewaomba hata ndugu zangu wa Jimbo la Kavuu, tukivuna mazao yetu hakuna kupunguza bei, tulinunua kwa shilingi 25,000 kwa debe na wao wauze shilingi 25,000 na kuendelea ili mjini yapande zaidi na wakulima waone sasa wanapata chochote kidogo na kukuza maisha yao kwa sababu pembejeo walijinunulia wenyewe. Leo tunataka tuanze ooh, chakula kule kimefanya hivi, hapana, tuwaache wauze kwa bei zile zile walizonunua ili na wao waweze kubadilisha maisha yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niongelee mradi wangu wa umwagiliaji wa Kilida. Mradi huu ulikula hela nyingi sana na ni mkubwa, umeharibika kutokana na mvua na mafuriko yaliyopita pale. Sasa sababu mvua bado zinaendelea niiombe sasa Wizara na nimekwishaleta maombi yangu maalum, mabanio na mifereji na magati pale yavunjika. Kwa hiyo, zile mvua zinavyoendelea maji yale sasa yanahama kwenye ile kata yanaenda kujaa kwenye Mto Msadya ambao umefurika sasa kwenye kata ya Usevya. Kwa hiyo, niwaombe mshughulikie lile banio, Naibu Katibu Mkuu yupo hapa ananifahamu na hilo banio analifahamu, Mr. Kalobelo unalifahamu vizuri. Naomba mlisimamie sasa ili ile scheme irudi kwenye miundo yake ili tuokoe kata zingine zisipate mafuriko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naishukuru sana Serikali yangu, nawashukuru sana Wizara ninaomba magari mawili ya nyongeza yaje kunisaidia kuchimba vile visima, tena nashukuru ni visima virefu vitakaa muda wa mwaka mzima ili wananchi wangu wapate maji safi na salama, na shule zangu zote za msingi na sekondari zipate maji safi na salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi na ninaunga mkono hoja ninaomba ile tozo iongezewe asante sana.