Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Naibu Spika. Awali ya yote, nachukua nafasi hii kuwapongeza kwa dhati sana Mawaziri wetu wawili hawa; Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara ya Maji kwa ufuatiliaji wao wa karibu na kutenda kazi kwao kwa umakini katika kusaidia Taifa letu kuondokana na shida ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ni moja kati ya nchi tano za Afrika zenye wingi wa maji na maji yanayofaa kwa matumizi ya binadamu. Tatizo letu labda ni kwenye changamoto za utaalam na rasilimali fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nijielekeze kwenye hii taasisi ya Wakala wa Uchimbaji Visima na Mabwawa (DDCA). Hii ni taasisi ya Serikali, unapokuja ushindani mara nyingi wanashindwa kwa sababu wana bei zao ambazo zimewekwa kwa kiwango.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachoshauri ni kwamba Halmashauri zetu zitumie hii Mamlaka ya DDCA katika uchimbaji wa visima na mabwawa, kwa sababu hawa wana utaalam wa kutosha na pindi wamechimba kwa bahati mbaya maji hayakutoka, huwa hawadai malipo. Taasisi binafsi wanatuchimbia visima na mabwawa na baadaye wanadai malipo na maji huwa hayatoki. Nashauri iongezewe nguvu na vifaa vya kisasa kabisa ili zile kanda ambazo wameweka ziweze kufanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakwenda kwenye mfuko wa maji. Nami nakubaliana na waliotangulia kwamba ile shilingi 50 sasa iongezeke kwenye bei ya mafuta, ya kukatwa kwenye mafuta, ile tozo ili ifikie shilingi 100.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naishauri Serikali iangalie zaidi kwenye simu. Kwenye simu kuna fedha nyingi sana, tuangalie vyanzo vingine vya kuongeza huu mfuko na tuangalie haya Mashirika ya Simu. Mashirika ya Simu yanaingiza fedha nyingi, lakini wanavyowekeza kwenye maendeleo ya wananchi ni kidogo. Katika huu Mfuko wa Maji nashauri kwamba vijijini wapewe asilimia kubwa ili kuimarisha miundombinu ya maji huko Vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ninaloliona hapa kwenye VAT ni katika madawa ya kutibu maji. Kwenye madawa ya kutibu maji hii VAT inapelekea sasa maji yawe bei kubwa ambapo kuna baadhi ya mamlaka wanashindwa kujiendesha hata kulipa bill za umeme. Naomba liangaliwe suala hilo kwenye madawa ya kutibu maji ili kumshushia mwananchi mzigo wa kulipa bill kubwa ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kwenye mikoa yetu, mkoa wa chini zaidi unaolipa bei ndogo ni 640 Moshi, na DAWASCO wanalipa 1,663 kwa unit, lakini bei hizi bado kwa Tanzania ukilinganisha na nchi za nje, mfano Denmark kwa unit ile ile inayolipwa Moshi shilingi 650 wao wanalipa shilingi 7,658. Ukienda nchi ndogo ambayo inalipa bei ndogo na ina utaalam wa kutosha, ni China; inalipa shilingi 902, lakini Moshi tunalipa shilingi 640. Hili nataka kutoa mchanganuo mdogo zipo nchi mbalimbali na bei zake.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuchangia Chuo cha Maji. Chuo hiki kiongezewe nguvu na vifaa vya kutosha ili tupate wataalam wa maji huko vijijini na kwenye Manispaa zetu. Kikiimarishwa Chuo hiki tutapata wataalam watakaosaidia kwenye Mikoa yetu na Wilaya zetu; mfano kwenye kitengo cha drill cha uchimbaji wa Visima, hiki kipewe msukumo mkubwa wa wataalam ili tuweze kuwatumia.
Mheshimiwa Naibu Spika, nami niongezee kuchangia kwenye uvunaji wa maji ya mvua ambapo suala hili liwe ndiyo kauli mbiu yetu. Tuanze na sisi Wabunge humu ndani kwenye majumba yetu na maeneo yetu tujiwekee akiba ya maji ya mvua. Nafahamu kuna nchi baadhi ya maeneo maisha yao yote wanaishi kwa maji ya mvua tu, hawana maji mengine yanayotumia, kwa sababu wapo juu ya milima, milima ni jiwe hawapati maji, maji yao ni ya mvua tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, maji ni afya. Kwa kuwa maji ni afya tukiwekeza zaidi kwenye maji, tutapunguza hata ununuaji wa madawa ya kutibu binadamu na hasa watoto wadogo ambao wanaathirika sana na maradhi mbalimbali ya maambukizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tukipata maji tutamsaidia mwanamama au mwanamke kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi, atapata muda wa kutosha wa kulea familia, atapata muda wa kutosha wa kujiajiri na kuinua kipato chake, badala ya kutumia muda mrefu kuhangaika kutafuta maji. Kwa hiyo, nashauri tuwekeze zaidi kwenye Mfuko huu wa Maji ili tuweze kumsaidia mwananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiendelea, naamini kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi ikiongozwa na Rais wake, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu na Mawaziri wote, wana nia na dhamira ya dhati kabisa katika kuhakikisha wananchi wa Tanzania wanaondokana na shida ya maji na shida mbalimbali zinazotukabili. Mambo huenda kwa awamu, awamu baada ya awamu, hatua baada ya hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini Wizara imejipanga vizuri katika kutekeleza mpango kazi wao waliotuandikia katika bajeti yao. Naishauri Serikali zile pesa walizoomba zitoke na zitoke kwa wakati...
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.