Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Prof. Norman Adamson Sigalla King

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji

MHE. PROF. NORMAN A. S. KING: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Kabla sijaendelea na mchango wangu, ni vizuri nitambue kama Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu kazi kubwa inayofanywa na Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ya kuimarisha miundombinu Tanzania. Wananchi wa Makete wamenituma niseme ahsante kwa sababu anashughulika na barabara yao ya kutoka Njombe, Makete kwenda Mbeya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, pia nitumie nafasi hii kupongeza uteuzi wa rafiki yangu na mdogo wangu Profesa Kitila Mkumbo kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maji. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilipokuwa nasoma kitabu hiki, nimerudia chote mara mbili, mara tatu nilishindwa kuamini. Nimeshindwa kuelewa kama Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya Maji na Naibu na Wasaidizi wake wanaifahamu Wilaya ya Makete vizuri na mchango wake wa maji kwenye nchi hii. Labda nimkumbushe Mheshimiwa Waziri. Wilaya ya Makete ndiyo inayotoa mto unaoelekea au kumwaga maji Mbarali katika mashamba ya Kapunga yanayolima mpunga pamoja na bonde la Usangu. Ni mto ambao chanzo chake kiko Wilaya ya Makete, Tarafa ya Matamba na Ikuwo. Ni maji hayo hayo yanayokwenda kwenye Hifadhi ya Ruaha, yanatoka Makete.

Mhedhimiwa Naibu Spika, ni maji hayo hayo yana kwenda kwenye bwawa la Mtera. Umeme wa Tanzania unategemea Makete. Ni maji hayo hayo yanabadilishwa jina lake yanaitwa Ruaha Mkuu ambapo eneo la Ruaha Mbuyuni wanalima vitunguu na nyanya, yanatoka Makete. Ni maji hayo hayo yanayotoka Makete yanayokwenda Kilombero na kuzalisha miwa, sukari wanayotumia Watanzania, yanatoka Makete.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile ni maji hayo hayo yanayotoka Makete yanakwenda Rufiji na kubalishwa jina na kuitwa Mto Rufiji. Pamoja na kazi kubwa ya wananchi wa Makete kuachia eneo la kilometa za mraba 465.4 ili angalau Watanzania milioni 8.9 waweze kupata na kutumia maji kutoka Makete, lakini Makete yenyewe haina maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nilihudhuria kikao cha Makamu wa Rais, pale Iringa ilikuwa bayana kwamba maji yanayotoka Makete yanNufaisha Watanzania milioni 8.9, lakini Tarafa ya Matamba na Ikuwo haina maji. Mheshimiwa Waziri ana ugomvi gani na wananchi wa Makete? Wanafanya kosa kuhama kilometa 465.4 ili waachie vyanzo vya maji ili Watanzania wapone, lakini wao wasipewe maji. Je, ni kosa lao wananchi hawa kuwahurumia Watanzania wengine? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo unachokiona chote kwenye bonde hili ninalolisema mpaka Rufiji, maji yake yanatoka Makete. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri, hebu awe na jicho la huruma. Ni vizuri bajeti yake itambue ya kwamba wananchi wa Makete na hasa Tarafa ya Matamba na Ikuwo wanahitaji maji na ndiyo zawadi pekee atakayowapa. Haiwezekani wao waachie eneo kwa ajili ya maji ya Watanzania wengine, lakini wao wenyewe wasipewe maji. Hivi ni dhambi gani wamefanya wananchi hawa wa Makete? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Tarafa ya Bulongwa, ukiongelea Kata ya Kipagalo, Luhumbu na Bulongwa yenyewe, nenda Kata ya Vijiji vya Tanala, Mang’oto, Mbarache, Kigala na Mfumbi maji hakuna, lakini wameachia eneo.

Mheshimiwa Naibu Spika, unafahamu kilometa hizi ninazozisema sehemu nyingine ni Jimbo zima. Kilometa za mraba 465 Makete halikaliwi na mtu wameacha ili Tanzania ipate kuneemeka, Tanzania iwe na maji mengi. Juzi wakati Waziri Mkuu alipofanya ziara pale Makete, aliambiwa kwamba tatizo, kuna mradi wa maji ambao Wizara ya Maji ilisimamia pale na ikaufanya vibaya mradi ule. Kwa hiyo, umepelekea Vijiji vya Kinyika, Matamba, Mlondwe na Itundu kukosa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, huo ni mradi uliosimamiwa na Wizara siyo wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete. Waziri Mkuu aliahidi wananchi wa Makete ya kwamba atamtuma Waziri mwenye dhamana aende autembelee mradi ule ili asahihishe makosa ambao Wizara yake ilifanya. Mpaka hivi ninavyoongea, rafiki yangu, kaka yangu Mheshimiwa Engineer Lwenge, Mheshimiwa Waziri hajafika Makete. Naamini ujasiri wake, natambua uwezo wake, najua ataitembelea Makete.

Naomba sana, awakumbuke wananchi wa Makete kwa sababu ya kazi yao nzuri ya kutunza vyanzo vya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unafahamu, leo hii tunapoongelea vyanzo vya maji, ni vigumu sana kupata eneo ambalo linazalisha maji kwa wingi kama Makete, sijui kama lipo. Ndiyo maana marefu ya mto wote huu angalau leo Watanzania mnajua sasa kwamba kimsingi mto huo asili yake ni Makete.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja za wenzangu ambao wanasisitiza umuhimu wa bajeti hii kuongezwa na hasa shilingi 50 inayosemwa kwa lita ya mafuta, ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vitu vingine vyote siyo watu wote wanavitaka, lakini unapoongelea maji ni kila mtu. Ndiyo maana tukaja na sentensi inayosema, “maji ni uhai” kwa sababu bila maji, hakuna uhai. Huwezi kula bila maji, huwezi kufanya chochote bila maji, ndiyo maana ni muhimu sana bajeti ya maji ipate kuongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu Mheshimiwa Waziri atakaposimama atalijulisha Bunge Tukufu kwamba hitimisho lake kwenye bajeti yake anaonesha shilingi bilioni 672, lakini ni vizuri asome pia ukurasa wa 173 katika hotuba yake, unaoeleza fedha za kutoka India dola milioni 103 ambazo ni sawa na trilioni 1.1 kwamba: Je, zimo kwenye bajeti au la! Kama zimo, basi bajeti ya maji itakuwa ni shilingi trilioni 1.762 na siyo bilioni 672.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri atakaposimama ni vizuri kutoa ufafanuzi ili kulifanya Bunge lielewe kwa usahihi kwamba shilingi milioni 503.04 iliyopo ukurasa wa 173 kwenye hotuba yake, je, imejumuishwa kwenye bajeti au la.

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.