Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami nichangie kwenye Wizara hii muhimu ya Maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii Wizara ni ya muhimu sana kwa sababu inagusa uhai wa binadamu. Binadamu ili aweze kutembea, miili yetu lazima itumie maji. Kwa hiyo, tukitamka maji ni muhimu kwa kila mtu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitabu cha Mheshimiwa Waziri nimekisoma vizuri sana. Tunaposema maji, kuna wengine wanasema kwamba maji yanaenda kumkomboa mama. Maji tunaenda kukomboa binadamu wote pamoja na wanyama.
Mheshimiwa Naibu Spika, akinamama wakiamka asubuhi saa 12.00 wanamwacha baba nyumbani na familia, wanatembea kilometa nne mpaka tano wanatafuta maji; na baba pale nyumbani anahangaika; kuna akinamama wengine wananyonyesha, anahangaika kuangalia watoto pale nyumbani. Ni shida kubwa! Kuna sehemu nyingine watu wanachota maji kilometa karibu nne kwa kufuata maji mbali na punda. Wakitoka saa 12.00 wanarudi saa 4.00 mpaka saa 5.00 asubuhi. Kwa hiyo, suala la maji ni suala la msingi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kusoma kitabu hiki, mimi kwenye Jimbo langu la Mufindi Kusini, kwa kweli wakati nasoma kitabu hiki nimesikitika sana. Mwaka 2016/2017, kwenye bajeti Wilaya yetu ya Mufindi tulipangiwa shilingi bilioni
2.5 na bajeti ile ya mwaka 2016 imerudi kama ilivyo. Mwaka 2016 hatukupata hela yoyote. Kwa hiyo, imerudi ile ile shilingi bilioni 2.5. Kwa Wilaya nzima shilingi bilioni 2.5 tukagawanya Majimbo mawili, ni sawasawa na sifuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Jimbo langu la Mufindi Kusini kuna miradi ambayo ina miaka mitano, mpaka leo tunavyoongea haijakwisha. Mheshimiwa Naibu Waziri na Mheshimiwa Waziri niliwaambia kwamba kwenye Jimbo langu tatizo kubwa, Serikali ilijitahidi sana kujenga matenki ya maji, miaka ya nyuma kama miaka kumi iliyopita. Yale matenki ya maji, yanahitaji ukarabati. Bahati Mheshimiwa Naibu Waziri na Mheshimiwa Waziri waliniahidi, wakasema watatafuta fedha. Sasa leo nimesoma kwenye bajeti humu, bajeti hii hawajatenga kukarabati miundombinu ya maji katika Jimbo la Mufindi Kusini. Kwa kweli hii ni hatari sana. Kama tutakuwa tunakuja hapa tunatoa ahadi kwa wananchi kwamba miundombinu tutakarabati, lakini tusifanye hivyo, ni hatari.
Mheshimiwa Naibu spika, wanafunzi kwenye Shule za Sekondari na Msingi wanapata shida sana, hakuna maji. Watoto wanatoka na vidumu kutoka nyumbani wanapeleka maji shuleni. Badala ya kwenda kusoma, wanaanza kufuata masuala ya maji. Ukienda kwenye zahanati, kwenye hospitali hata Hospitali ya Mafinga pale mjini, maji ni shida kubwa. Namwomba Mheshimiwa Waziri, matenki yale ambayo aliahidi kwamba atakarabati, wananchi waanze kupata maji, naomba hiyo kazi aifanye.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitaje matenki ambayo yalitengenezwa na Serikali na miundombinu yake imeharibika. Ukienda Nyororo kuna tenki moja, Igowole kuna tenki la pili, Ihomasa, Mkangwe, Ikangamwani, Kibao, Sawala, Kasanga, Ihawaga, Nanyigwe; sehemu hizi zote matenki yapo lakini maji hamna, miundombinu imeharibika. Kama kweli tuko serious na wananchi tumewaahidi, naomba matenki yale yaweze kutengenezwa wananchi waanze kutumia maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna vijiji vya Mufindi Kusini havina maji kabisa. Bahati nzuri mimi Mbunge nimechimba visima pale, lakini Serikali kwenye gravity system bado haijapeleka. Kwa mfano, ukienda Mninga pale hakuna maji, Mkalala, Ihawaga, Luhunga, Lugema, Kiyowela, Idete, Iholo, Itika, Kitasengwa, Itulituli, Kisasa, Ibatu, Mtambuka, hakuna maji vijiji hivi. Halafu napewa shilingi bilioni mbili ambayo ni ya mradi mmoja wa mwaka 2016 au mradi wa kijiji wa Kata ya Mtwanga. Mwaka huu sijapewa hela yoyote. Sasa mimi Mbunge ninayewakilisha wananchi nakuja hapa, naona sijapewa hela yoyote. Hii inakuwaje? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri Mheshimiwa Waziri nimeshamwambia, kwamba kwenye Jimbo langu hujapanga bajeti yoyote na ameniagiza, amesema nimwambie Mkurugenzi waandike proposal waweze kuleta. Ninavyoongea hivi, kama Mkurugenzi ananisikia, kesho aandike proposal hiyo, kesho kutwa nimpe afanye amendment. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna sehemu nyingine ukiangalia kwenye kitabu hiki, unaweza ukaona kuna maeneo matano, Wilaya moja imepewa fedha shilingi bilioni 200; mimi napewa shilingi shilingi bilioni mbili. Kweli hiyo inakuja hiyo? Yaani Wilaya moja ukijumlisha hela za wafadhili, ukijumlisha hela za ndani, ukijumlisha na hela nyingine sijui miradi maalum wanapewa wilaya moja shilingi bilioni 200, sisi kule hatujapewa hela. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama kweli tunakuja ndani ya Bunge, tunataka usawa tujadili vizuri, tunaomba miradi ya maji ifuate utaratibu. Hilo litakuwa ni suala la msingi sana, kila wilaya iweze kupewa fedha. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais; alisema kwamba ikifika mwaka 2020 masuala ya maji, asilimia kubwa atakuwa ametatua. Sasa atatatuaje kama wilaya moja ndiyo inapewa fedha nyingi, Wilaya nyingine hazipewi? Hii italeta tatizo kubwa. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, katika kugawa fedha afanye analysis vizuri, agawe sawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, tulisema kila kijiji kitapewa shilingi milioni 50, kwa nini asiseme kila kijiji kitapewa shilingi milioni 200 kwa ajili ya kutatua masuala ya maji ili tuwe sawa? Kuna watu wengine hapa wanashingilia wamepewa hela nyingi sana; anafika hapa anaanza kushangilia. Mimi nitashangiliaje kama Wilaya yangu hatujapewa fedha? Mimi nitakuwa Mbunge mwenye akili kweli! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja lakini lazima nitamletea Mheshimiwa Waziri proposal ili Jimbo langu la Mufindi Kusini liweze kupewa maji. Kama halitapewa maji, basi nitamwandikia Mheshimiwa Rais, nimwambie mimi hapa nitafanyeje? Sasa katika kuongoza, nitafanyeje mikutano pale kama hakuna maji? Haiwezekani! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi kusema kwamba Serikali yetu inafanya vibaya. Serikali ina malengo mazuri safi kabisa, lakini Watendaji wanatuangusha katika kugawa mahesabu. Kama wanashindwa, sisi Wabunge tugawe mahesabu kwa kila Wilaya. Haiwezekani wilaya moja ikapewa shilingi bilioni 600, shilingi bilioni 200, shilingi bilioni 100 na wengine wanapewa shilingi bilioni moja au shilingi milioni 500. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pale Mafinga nimesoma wamepewa shilingi milioni 500. Sasa mwingine anapewa shilingi bilioni 200, hii haiwezekani jamani! Hata kama kiasi ni kidogo, tunajua sawa ni ndogo, tugawane sawa basi! Tunajua kama fedha ni ndogo, hiyo ni collection ya revenue kwa mwaka, hatuwezi kupinga, lakini kile tunachokipata tugawanye sawa kila mmoja aridhike.