Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuweza kunipatia fursa na mimi nichangie kwenye Wizara hii muhimu sana kwa maisha ya Watanzania na hasa kwa sisi wahanga ambao ni wanawake ambao tunatembea kilomita nyingi kutafuta maji licha ya Sera ya Maji kusema kwamba tutakuwa tunapata maji ndani ya mita 400.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhahiri kabisa zaidi ya asilimia 80 ya Wabunge waliopo humu ndani watakubaliana na ukweli kwamba maji imekuwa ni tatizo na inapelekea tunakuwa na vifo vingi. Mwanamke akienda hospitalini kujifungua bila maji kwa kweli sidhani hata kama zoezi litaweza kukamilika kama inavyotakiwa na katika hali ya usafi na afya. Zaidi mtakubaliana na mimi kwamba watoto wetu wa kike wengine wanarudi majumbani kutoka shuleni au hawaendi kabisa kwa sababu ya kukosa maji hasa wakiwa kwenye zile siku zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na kulaani wale Wabunge waliosema kwamba tusiongeze fedha. Ni ajabu sana kuona kwamba fedha za maendeleo zilizokwenda kwenye sekta hii ya maji ni asilimia 19 tu ilhali kwenye sekta ya ujenzi fedha zilienda zaidi ya asilimia 100 tulizozipanga kwenye bajeti iliyopita. Kwa hiyo, naomba sana Serikali kwa mapendekezo ambayo tumeyatoa hapa Bungeni tuongeze kutoka shilingi 50 mpaka shilingi 100 kwa sababu hizi fedha zipo ring-fenced, tuziongeze zifikie hapo tuweze kutatua matatizo ya maji vijijini na mijini pia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nirudi sasa kwenye Jimbo langu la Tarime. Tarime tuna Hospitali ya Wilaya na kuna kipindi tunakosa maji kabisa, wagonjwa wakienda pale inakuwa shida na mtafutano. Tuna Gereza la Tarime linahitaji maji na lina shida kubwa sana, tuna taasisi zingine mbalimbali zahanati na vitu kama hivyo vina tatizo hili la maji. Katika Mji wangu wa Tarime licha ya kwamba ni mjini ni chini ya asilimia kumi tu ya wakazi wa Tarime ndio wanapata maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati najaribu kupitia hiki kitabu kwa kweli nimesikitika sana. Nimekisoma na kugundua katika miji mikuu ambayo imepata maji Tarime haipo licha ya kwamba nilishauliza maswali mengi sana hapa ndani na Waziri akaniahidi kabisa kwenye bajeti hii atakwenda kutenga fedha na kuhakikisha kwamba anatatua tatizo la maji Tarime. Nikasema kwa mfano mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda mpaka Tarime na Sirari tayari mwaka 2012 walishafanya upembuzi yakinifu na Benki ya Maendeleo ya Ufaransa ilishajitolea kufadhili mradi huu na Waziri akaniahidi kwamba watatenga bajeti, nimeangalia sijaona.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Tarime wanateseka na maji. Wanapoteza muda mwingi ambao wangeenda kufanya shughuli za kimaendeleo kutafuta maji.Akinamama wajawazito wanatembea kilomita nyingi kutafuta maji. Kwa hiyo, naomba sana mnisaidie kwa kuweka fedha ili kutatua tatizo la maji katika Mji wa Tarime. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Tarime pia tuna Bwawa la Nyanduruma, lile bwawa ni la enzi za Mjerumani lakini mpaka leo hii halijaboreshwa. Napenda sana Serikali muwekeze fedha pale kwani bwawa lile tukiliboresha zaidi litakwenda kutoa mtandao wa maji ambayo yataenea kwenye Mji wa Tarime na kusaidia kutatua tatizo la maji wakati tukisubiria maji ambayo yatatoka Ziwa Viktoria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, linguine, kuna mradi ambao ulikuwa ni msaada kwenye Kata ya Nyandoto, mradi wa Kemangeumekamilika lakini bado hamjaleta fedha kuweza kuweka sasa mtandao wa maji kuwafikia wananchi. Tenki limeshajengwa, tunahitaji kupata fedha ili kuweka network ili wananchi wa Tarime waweze kupata maji. Nishauri hii sio kwa Tarime tu hata huko kingine unakuta wakati mwingine tuna visima vya asili ambavyo tukiviboresha vinaweza kusaidia kutatua tatizo la maji kwa muda mfupi wakati tukisubiria mjipange kwa mipango ambayo inatekelezeka kwa kutumika kwa muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana Wabunge tukatae hii bajeti...
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Muda wako umekwisha Mheshimiwa Esther Matiko.