Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muheza
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuwa mchangiaji wa kwanza mchana huu. Kwanza napenda kuwashukuru sana Waziri na Naibu wake kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya ya kuweza kutuletea watalii wengi. Wizara hii ni muhimu sana ambayo inaingiza pato la Taifa kama alivyosema mwenyewe Mheshimiwa Waziri kwenye asilimia 21; asilimia 17.5 ikiwa utalii na misitu asilimia 3.9. Nitakuja kuongelea suala hilo baadaye lakini ningependa kuanza mchango wangu na Hifadhi ya Amani (Amani Natural Reserve). (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Misitu ya Amani ni mikubwa sana na kama nilivyoongea kwenye mchango wangu mwaka jana ni misitu ambayo ina mambo mengi ndani yake. Ukiacha mambo ya miti yenyewe ambayo ipo pale pamoja na vivutio mbalimbali au scenario ambayo ipo au pamoja na vipepeo, maua na kila kitu ambavyo viko pale lakini ni reserve ambayo inatakiwa iangaliwe kwa uangalifu. Ni reserve ambayo inatupa chanzo cha maji kutoka Mto Zigi. Kwa hiyo, reserve hii sasa hivi ina hatari ya kuharibiwa na ina hatari ya hata chanzo cha maji kuharibiwa kabisa kwa sababu hivi karibuni tu maji ya Tanga yote yalikuwa ni tope. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juhudi zimefanyika kimkoa, Mkuu wa Mkoa amejaribu kupeleka watu kule kwa ajili ya kuzuia ukataji wa miti kwenye hifadhi hiyo. Mkuu wa Wilaya pamoja na Halmashauri tumekuwa tukipeleka Askari wa Field Force lakini nguvu inakuwa ni ndogo. Ningeshauri ili kuweza ku-preserve Amani Nature Reserve, Mheshimiwa Waziri hawa Askari wa Wanyamapori ambao wapo kwa ajili ya kuangalia nafikiri wako pia kwa ajili ya kuangalia hifadhi zetu, tafadhali ahamishe hata unit moja immediately vinginevyo hii reserve itapotea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, reserve hii ni ya maana sana na iliwahi kulinganishwa kama ni moja ya maajabu ya dunia na mwanahistoria mmoja ambaye alikwenda kwenye Kisiwa cha Galapagos kule Ecuador Pacific. Sasa tutakapoachia reserve hii iweze kuharibika tutakuwa tumefanya makosa makubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu wakulima wangu wa Derema 1,128. Wakulima hawa wameshapewa maeneo kwenye shamba la Kibaranga lakini bado hawajahama. Kama nilivyosema kwamba bado wanahitaji kifuta jasho ambacho Mheshimiwa Waziri aliahidi kwamba atakiangalia, naomba akiangalie ili wakulima hawa waweze kuhama mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu ni kuhusu Mnada wa Miti ya Tiki. Mheshimiwa Waziri alikuja kuhudhuria Mnada wa Tiki pale Lunguza. Mnada huu umekuwa na malalamiko mengi sana kwani umekuwa ni kilio kwa wafanyabiashara na wenye viwanda pale Muheza kwa sababu tangu hii system ya mnada imekuwa introduced kuna viwanda karibu kumi vimefungwa pale Muheza. Hii ni kwa sababu matajiri wanakuja pale na hawa wenye viwanda vidogo vidogo hawawezi kushindana na hawa matajiri, utakumbuka kwenye mnada uliopita tajiri mmoja alichukua karibu vitalu vyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka Mheshimiwa Waziri aangalie system hii ya mnada ijaribu kuboreshwa na kuangalia watu ambao wapo wanazunguka wanaangalia hizi hifadhi. Tiki zinapandwa vizuri sana, huyu Meneja wa Shamba la Lunguza Abdallah anafanya kazi nzuri sana na kila tiki inapokatwa unakuta amekwishapanda. Sasa wafanyakazi na wakulima wanafanya kazi nzuri, itakuwa siyo busara wao kuwanyang’anya sasa kwa sababu hawa matajiri wanaponunua hivi vitalu wanapakia magogo yote wanakwenda kupasulia Dar es salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka Waziri aangalie ili hawa wazawa ambao wamefungua hivi viwanda pale waweze na wao kupata hizi tenda za kuweza kupasua haya magogo, vinginevyo itakuwa shida. Kwa sasa viwanda karibu kumi vimefungwa, wafanyakazi karibu 1,000 wale wanaokaa pale wamepoteza kazi. Kwa hiyo, ni lazima kuwawekea masharti, kama hao matajiri lazima wafungue viwanda pale ili wafanyakazi wa pale waweze kupata kazi ya kufanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nilikwishamwomba Katibu Mkuu ni kwamba tunategemea barabara ile sasa hivi kuiweka lami, lakini pale kuna malighafi (moram) ambayo ipo kwenye msitu huu lakini ipo pembeni. TANROAD wameomba sana kutumia hiyo malighafi kwa ajili ya kutengenezea hiyo barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ombi hili liweze kuzingatiwa kwa sababu kipindi kijacho tumeshaingizwa kwenye mpango kwa ajili ya kuwekewa lami kipande kidogo. Naomba kabisa mfikirie tutumie hiyo moram ambayo ipo pale iweze kutengeneza barabara hiyo ya Amani. Barabara hii itasaidia sana kuleta watalii ambao wataongezeka ili kupanda kwenye Milima ya Amani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la Mbuga ya Saadan ambayo ina upungufu sana wa wanyama. Mbuga hii sisi Muheza tuna interest nayo kwa sababu inapita Bagamoyo, Pangani na inatoboa mpaka Muheza inakwenda mpaka Amani. Sasa tulikuwa tunaomba waongezwe wanyama pale iweze kusaidia ili siku zijazo watalii watatoka Sadaan wanakwenda Pangani, Amani wanarudi Pangani kupumzika. Ni suala la muhimu sana ambalo naomba mzingatie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nakuja kwenye utalii. Kama nilivyosema, utalii unaingiza pato kubwa la Taifa lakini ukiangalia idadi ya watalii wanaoingia hapa nchini sasa hivi imeongezeka tuna milioni 1.2 ukilinganisha na mwaka jana ambayo ilikuwa milioni 1. Hata hivyo, bado idadi hii haitoshi kabisa ukiilinganisha na nchi nyingine. Kwa mfano, Victoria Falls Zimbabwe, pale ni hizo falls tu zenyewe lakini watalii ambao wanaingizwa pale ni wengi kuliko hawa wa kwetu, ni zaidi ya milioni 2.5 kama sikosei.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna umuhimu wa kujaribu kuongeza vivutio vya kuwafanya watalii waweze kuja kwa wingi na tumeona katika Afrika tupo kwenye namba 10 au
11. Kwa hiyo, bado tupo nyuma na tunahitaji kuongeza juhudi ili kuongeza watalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watalii hawa unawaongeza namna gani? Kuna masuala ya matangazo (advertisements). Suala hili ni muhimu sana na ukiangalia hapa hela ambazo zimetolewa kwa ajili ya advertisement ni ndogo sana. Nakumbuka kuna wakati mimi nilikuwa Denver kule Marekani na nilifarijika sana nilipoona kwenye TV moja ya Fox wanaonesha migration Serengeti na baada ya ule mkutano Wazungu wengi sana walionesha interest ya kuja kuangalia hii migration huku Tanzania. Sasa advertisement kama zile zinasaidia sana, ni lazima tuweke umuhimu sana kwenye mambo ya advertisements. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na advertisements kuna masuala ya tour operators. Tour operators wamesahauliwa sana na sijaona wakitajwa kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri. Hawa ndiyo watu wanaleta watalii, hawa ndiyo wanafanya mipango, tour operators ni watu muhimu sana. Ukiangalia kwa mfano hao Victoria Falls ambao wanaletewa watalii wengi sana, wengi wanatoka South Africa na Zimbabwe wamefungua Ofisi kule (tour operator), wengi wanawachukua wanawaleta mpaka wanajaa, ni vizuri sana tukawapa umuhimu watu hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tu nilikuwa naangalia kwenye gazeti moja la wananchi kwamba Kenya Airways inatoa ndege mara tatu sasa hivi kutoka Cape Town - Victoria Falls – Nairobi. Ni muhimu sana kuangalia tour operators ambao tukijumuisha pamoja na direct flights ambazo ni muhimu sana Mheshimiwa Waziri azipate, Wizara hii ina uwezo wa kununua au kukopa ndege yake ili kuwatoa watalii direct, watalii wanapenda direct flights.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwa mfano kama Zanzibar, Zanzibar wanapata watalii wengi sana, lakini tatizo la Zanzibar sikumbuki sasa hivi kama wamesharekebisha ile mikataba yao ya zamani ambayo…
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Balozi.