Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Ajali Rashid Akibar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Newala Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naomba kuchukua nafasi hii kwanza tumshukuru Mheshimiwa Rais, maana tusipomshukuru tutakuwa ni wezi wa fadhila. Mheshimiwa Rais katika Wizara hii ametoa mchango mkubwa sana kwa kuchukua jitihada zake za dhati kabisa kutafuta fedha na kuweza kununua ndege ambazo kwa kweli umekuwa mchango mkubwa sana kwa Wizara hii ya Utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata Mheshimiwa Gibson pale rafiki yangu naye ameona kwamba mchango wa Mheshimiwa Rais katika kununua ndege ni mchango mkubwa sana kwake yeye binafsi amesaidia sana kufanya contribution ili Wizara hii na yenyewe kwenye utalii ionekane machoni kwetu na watalii wa nje moja kwa moja na ndege nyingine zinakuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mchango huu ningemwomba rafiki yangu Maghembe ambaye ndiye Waziri, atambue mchango wa Mheshimiwa Rais, vilevile atengeneze nishani ya kumtambua Mheshimiwa kama Mr. Utalii namba moja baada ya hapo kila mwaka atakuwa anatengeneza nishani moja moja hii itakuwa nafasi mojawapo ya kumtangaza Mheshimiwa Rais na kuwatangaza wale wengine wote ambao watakuwa wanashiriki katika kutangaza utalii katika nchi yetu, yatakuwa ni mashindano makubwa ambapo tutakuwa tunatambua vyanzo vipya, hapo itakuwa ni sehemu ya matangazo, atashirikisha wanafunzi, atashirikisha wanavyuo na wanahabari vilevile. Mheshimiwa Maghembe asiogope, atumie jitihada zake kutangaza utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo za Mheshimiwa Rais, kama Wabunge wenzangu walivyosema sekta ya utalii ni sekta ambayo ni pana sana, ili sekta hii iweze kufahamika au kama unataka kuanzia kwenye sekta ambayo ni mpya ni lazima azitambue maliasili zilizopo katika ardhi hii na akishatambua maliasili ardhi zilizopo katika ardhi hii ni lazima afanye tafiti. Akishafanya hizo tafiti hana jinsi nyingine ni lazima aingie gharama kubwa sana ya kutangaza vivutio hivyo, ukishatangaza hivyo vivutio hapo ndipo utapata rasilimali na atapata fedha Mheshimiwa Maghembe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Maghembe juzi wakati tunatoa mchango hapa mimi nilitoa mfano mmoja mdogo sana kuhusu kisiwa cha Kilwa. Katika mchango wangu mkubwa sana nitazungumzia Kisiwa cha Kilwa. Inawezekana watu wengi hawajui Kilwa maana yake nini, wanasikia tu kwamba kuna Kilwa Kipatimu, Kilwa Masoko, Kilwa Pande. Hayo maeneo yote yalikuwa ni kisiwa kimoja na kisiwa hiki kina maajabu sana. Kisiwa hiki kilinunuliwa na tajiri mmoja ambaye inasadikika kwamba alinunua kwa kipande cha nguo ambacho kilifunika kwenye vijiji vyote hivi na kile ambacho kilifunika paliitwa Kilwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kilwa zote saba au nane ni maeneo ambapo yule mfalme alikuwa anamiliki, hiyo historia ni nani ambaye anayeifahamu kwa kweli, watu wengi hawaifahamu historia hiyo na kuna majengo katika hivyo visiwa pamoja na hayo maeneo kuna majengo ya Wajerumani ambayo namwomba Mheshimiwa Waziri akafanye tafiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu nilizungumzia kwamba kuna magofu na visiwa zaidi ya 1000 ambavyo hata Waheshimiwa Wabunge humu ndani tukisema tugawane kila mmoja atapata viwili viwili, haya ni maeneo mapya ya utalii, Mheshimiwa Maghembe aende kule akafanye tafiti hayo maajabu watu wayaone. Siyo ajabu hata Waheshimiwa Wabunge humu ndani wengine hawajui. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, Watalam wake wafanye tafiti za kina ili imsaidie yeye mwenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ukienda Lindi Mjini, kuna eneo linaitwa Kitunda. Bahati nzuri nilikuwa nimekwenda kule kulikuwa na watu ambao wapo kule chini inasemekana kwamba wanatafuta fedha ya Wajerumani, na inasemekana kwamba kuna handaki ambalo liko ndani kama kilomita mbili ambapo Wajerumani walikuwa wanatembea chini kwa chini. Mheshimiwa sisi ambao tulikwenda kule tuliweza kuogopa, lakini Mheshimiwa Waziri nadhani akitumia watalaam wake ataangalia lile handaki lina nini ni sehemu moja ambayo ni nzuri sana ya kiutalii ya vivutio, lakini kwa kuwa havijatambuliwa haviwezi kufahamika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitoka hapo nenda Mtwara moja kwa moja kule kuna maeneo ambako Stanley alikaa siku saba kule kuna nyumba, bahati nzuri nimeiona leo katika maandishi ya Mheshimiwa Waziri, lakini yale magofu yaliyopo pale Mtwara ni mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri kwamba yale magofu ambayo au na vile visiwa ambavyo vipo kule Kilwa ambavyo watu wanaweza wakavirekebisha, tuwavutie wao hata kama wakitengeneza basi wakae navyo kwa muda mrefu na siyo kwenda kuwanyang’anya na kuwabugudhi wale. Kwa mfano, kulikuwa na yule Mama ambaye alikuwa amekuja pale akatengeneza kile kisiwa na akajenga hoteli akawa analeta watalii wake wasiopungua 70 hadi 80 na akawasomesha wanakijiji pale tusim-discourage sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yeye anamiliki lakini maana yake baada ya hapo ile ardhi hawezi kuondoka nayo hebu Wizara ifanye utaratibu wa kuhakikisha kwamba hawa watu ambao wanafufua au wanarekebisha hayo magofu, hayo magofu yanaendelea kubaki katika structure ya asili, provided hawachukui hatuna sababu ya kufunga biashara zao. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri wa Utalii kama kuna mtu anaweza kutambua hivyo na anaweza akavitangaza hivyo na kuna watu wanafanya hizo renovation basi watambue.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwangu pale kuna shimo linaitwa shimo la Mungu, shimo la Mungu hilo ukiangalia liko chini ni kama kilomita mbili hivi. Kwa hiyo, maana yake ukienda ukiangalia mara moja kama siyo mzoefu lazima mtu aje akushike mkono. Vilevile kuna njia ambayo walipita Wajerumani na kuvuka kwenda Msumbiji. Hawa Wajerumani walikuwa wametokea Msumbiji wakati wanafanya research wakafika pale na ndiyo maana waka- establish Wilaya ya kwanza Tanzania ambayo ni ya Newala, lakini walikuwa wanafanyia research katika lile shimo la Mungu. Namwomba Mheshimiwa Waziri aende akalibainishe hilo shimo la Mungu ili watu walifahamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nani anayejua kwamba leo ukienda Zanzibar kuna Kisiwa cha Chumbe ambacho kuna kobe wakubwa ambapo watu wawili tunaweza tukapanda kama ngamia tukazunguka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Rais aliyepita alizungumza kitu kimoja ‘ukitaka kula lazima uliwe’ asiogope kuliwa Mheshimiwa Maghembe! Aingize fedha, apeleke proposal mbona makusanyo ni makubwa? Ili hii sekta tuweze kuvuna fedha za kutosha ni lazima tuwekeze kwa kiasi kikubwa. Alikuwa ana maana ya kwamba tusiogope hasara ili tuje kupata faida na ndiyo maana alisema kwamba ukitaka kula ni lazima uliwe, maana yake wekeza mtaji mkubwa then utapata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haingii akillini leo maeneo ya uwekezaji ya maajabu saba ya dunia yako Tanzania, nenda Ngorongoro crater nenda Serengeti. Serengeti kuna maajabu pale kutokana na movement ya wale wanyama ambao wana-move kutoka eneo moja la juu kwenda sehemu nyingine, lakini ile kwa kweli ni maajabu lakini tunayatangaza kwa kiasi gani? Mheshimiwa Waziri apeleke habari kote Tanzania ili watu wazijue, duniani kote tusiogope hizo gharama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyabiashara huwa kwanza tuna-risk, tunaingiza fedha kwa kiasi kikubwa ndiyo baadaye tunakuja kupata, usitegemee kupata bila kuwekeza haiwezekani, hayo maajabu hayapo duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna bodi pale kama tatu au nne, kuna fees anazozipata Mheshimiwa Waziri, kwa nini anatumia shilingi bilioni mbili kutangaza, kwa nini asichukue bilioni 20 tukapata bilioni 300. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri na niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge katika Wizara ambazo tunaweza tukapata fedha ni Wizara ya Maliasili na Utalii, fedha ipo nje, haihitaji kutumia gharama kubwa. Kwa hiyo, nimwombe sana, zile bodi tatu kwa nini zinakuwa nyingi vile? Kwa nini asiziunganishe kama vile tunavyofikiria kuunganisha mifuko? Aunganishe zile bodi apate bodi moja ambayo itakuwa inafanya kazi kwa ufanisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kwa kumalizia niongelee kuhusu utalii wa ndani. Kama vile ambavyo tumezungumza, haiwezekani utalii wa ndani Mheshimiwa Waziri akafanya peke yake. Suala la utalii ni kubwa. Naomba aunganishe nguvu na Wizara ya Habari vilevile na Wizara ya...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana.