Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Fatma Hassan Toufiq

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa nami nichangie hoja iliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii kwanza kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na Watendaji wote kwa kuandaa bajeti hii ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya mwaka 2017/2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze moja kwa moja kwenye biashara ya uwindaji. Inabidi ikumbukwe kwamba biashara hii ni biashara tofauti sana na biashara nyingine. Uwindaji wa kitalii ni shughuli ambayo ni starehe kwa watalii husika, hivyo basi ni dhahiri kwamba Watalii hawa wanapokuwa wamekuja kwa ajili ya uwindaji wa kitalii wanahitaji kuwa na mazingira ambayo yametunzwa vizuri na yako vema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa kuna tishio kubwa sana la uvamizi wa mifugo katika mapori yetu mbalimbali au mapori ya akiba na hii imekuwa ni kikwazo sana kwa uwindaji wa kitalii na hata hii imesababisha asilimia 34 ya uwindaji wa kitalii ukaporomoka kati ya 2013 na 2017. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri aone kwamba hii tunapoteza pato la Taifa, kwa hiyo ipo sababu ya msingi kabisa kwa Serikali kuona inafanya mkakati wa kuhakikisha kwamba mifugo haikai katika haya mapori ya akiba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirejee kwamba kupoteza hii asilimia 34 ya vitalu kwa kweli Taifa linakosa mapato makubwa sana. Kwa mfano, Serikali inakosa mapato kwenye ile daraja la kwanza kabisa la vitalu US$ 60,000, hii ni pesa ya kutosha sana. Sambamba na hilo kwenye grade ya pili tunakosa US$ 30,000 na kadhalika na kadhalika mpaka grade ya tano ni US$ 5,000. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla ione kwamba kweli hapa Serikali inakosa mapato kwa sababu tu ya mifugo kuingia katika mapori haya. Naomba nitoe shime kwamba lazima uwepo mkakati wa uhakika wa kuhakikisha kwamba mifugo haiingii katika mapori haya.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nibainishe kwamba kwa kuwa sekta ya utalii inaingiza asilimia 25 ya fedha za kigeni na kuchangia asilimia 17 ya pato la Taifa, hivyo naendelea kusisitiza kwamba ni budi Serikali ikawa na mkakati endelevu wa kuhakikisha kwamba tunaweza kupata pato zaidi kwa kuboresha miundombinu iliyopo katika maeneo yote ya hifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia nizungumzie sekta hiyo ya utalii hasa nishauri kwamba, sekta ya mifugo pamoja na Halmashauri zijitahidi sana kusimamia Sera ya Mifugo kwa kutenga maeneo ili kusudi wafugaji waweze kupata maeneo yao waweze kuweka mifugo yao kule. Hii pengine inaweza ikasaidia mifugo isiingie katika hifadhi zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, ni budi tuwe na takwimu sahihi za mifugo iliyopo katika nchi hii na kila mfugaji abainike kwamba ana mifugo mingapi. Pia wafugaji lazima wahamasishwe tu wafuge kwa tija ili mwisho wa siku Serikali iweze kupata mapato kwa kutokana na utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia nizungumzie suala la misitu katika mabonde na mito. Haina shaka kwamba tatizo la uharibifu wa mazingira binadamu ndiyo wahusika wakuu. Kwa hiyo, maeneo mengi sana yameharibiwa, maeneo mengi sana yamekatwa miti na kadhalika hasa kwenye maeneo ya mabonde. Nashauri kwamba, Serikali pia ije na mkakati wa nguvu wa kuhakikisha kwamba maeneo yale ambayo ni ya mabonde yahifadhiwe na yapandwe miti mingi sana kwa sababu ile mito na maziwa ambayo yanakauka inatokana na ukataji miti, hivyo nilikuwa nashauri Serikali ilisimamie hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo naomba nisisitize tena suala la upandaji wa miti ili tuweze kukilinda kizazi hiki na kizazi kijacho, watoto wetu na wajukuu zetu na vitukuu wasije wakatulaumu kwamba sisi tulishindwa, kwa hiyo suala la udhibiti wa mazingira ni lazima lifanyike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo naomba pia nichangie idara ya utalii ya mambo ya kale. Kuna mwenzangu mmoja ameshalizungumzia hili lakini nami naomba niongezee. Ili Taifa liweze kupata kipato ni budi Serikali yetu iendelee kutangaza vivutio vya utalii pamoja na malikale. Kwa mfano, katika maeneo ya fukwe, mapango, kuna miongoni mwetu ambao pia wamezungumzia kuhusu suala la mila na desturi za makabila mbalimbali, historia za viongozi, pamoja na mila za makabila na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, hapa kwetu Mkoani Dodoma Wilaya ya Kondoa kuna mapango ambayo michoro yake iko katika historia ya dunia. Je, Serikali imetangaza kiasi gani Wilaya hii ya Kondoa ili kusudi nayo iwe ni mojawapo ya kivutio cha watalii? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wa Afrika ya Kusini, kuna utalii wa mila na desturi ambao unaendelezwa kule, sisi tuna zaidi ya makabila 120. Je, tumejiandaaje makabila haya nayo yaweze kuwa kivutio cha watalii? Tuna makabila mbalimbali, tuna Wamasai, tuna Wayao, tuna Wanyakyusa na mengine ambayo sikuyataja, wote hawa wana mila zao na desturi, hebu nasi tuone ni kwamba tunafanyaje kuhusu hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo naomba pia niishauri Serikali ifanye utaratibu wa kutuma wataalam wetu katika maeneo mbalimbali ya Afrika na nje ya Afrika, kuona wenzetu wamewezaje kufanikiwa katika hili suala zima la utalii. Sisi tuna vivutio vingi sana sana duniani, lakini bado hatujaweza kuwavutia watalii kiasi hicho. Nashauri Serikali ingefanya utaratibu wa kuwapeleka wataalam mbalimbali ili kusudi waje walete ujuzi kutoka maeneo hayo angalau na sisi itusaidie kupaisha sekta yetu ya utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba nichukue fursa hii kushukuru sana na kuunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.