Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Nianze kwa kuwapa pole wananchi wangu wa Jimbo la Geita Vijijini ambao watoto wao wamefariki kwa ajali ya kuzama kwenye Ziwa Victoria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anazozifanya, lakini pia nimpongeze sana kwa kumteua Profesa Maghembe kwenda kushika Wizara ya Maliasili na Utalii. Lakini sitakaa nimpongeze Maghembe hata siku moja kama hajabadilika, aliyemteua nampongeza, lakini Profesa Maghembe sitakaa nimpongeze hata siku moja.

Waheshimiwa Wabunge, sisi tunaotoka kwenye majimbo ya vijijini kuna matatizo makubwa hata ya Ikwiriri nikwa sababu yanaandikwa kila siku kwenye magazeti. Lakini kwa sisi ambao tunaishi pembeni mwa mapori tuna matatizo makubwa na ndio maana nasema siwezi kumpongeza Profesa Maghembe kwa yafuatayo; kwanza kwenye Halmashauri zetu tumepitisha sheria, mwananchi akiwa na nusu debe, gunia moja tu la mkaa haruhusiwi kukamatwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hebu nenda Ofisi za Maliasili, kumejaa baskeli tunasubiri sijui hata hiyo minada mtamuuzia nani hizo scrapers za baiskeli, watu wameshikwa na gunia moja au madebe mawili anakamatwa na ananyang’anywa baskeli, ananyang’anywa pikipiki yake. Sasa hivi sisi kwetu Kijijini ukiona gari ya Maliasili bora ukajitundike hata kwenye mti kuliko kusubiri kile kipigo utakachokipata.

Mheshimwia Mwenyekiti, lakini mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Maghembe ya Maliasili, napata shida sana kujiuliza labda sisi Kanda ya Ziwa tulikuja kwa bahati mbaya kwenye hii Tanzania. Mbona yanayofanyika Kanda ya Ziwa, kule Kanda ya Kaskazini mbona hayafanyiki wakati na wao wana mapori. Waziri ametoa siku tatu tukamatiwe ng’ombe kwa kisingizio ng’ombe ni za Wanyarwanda. Wakati huo huo watumishi wake wanaowaingiza Wanyarwanda wanawaambia toeni ng’ombe wale Wanyarwanda, mnaenda kukamata ng’ombe za Wasukuma, halafu mnazipiga mnada, na Wabunge mnada wenyewe unavyopigwa ni wa deal.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ng’ombe 600 unaambiwa lete shilingi milioni tatu wanatoa watu wao Ubungo, halafu nakupongeza kwa sababu gani. Na mimi nataka nikwambie Profesa Maghembe kama Mwenyekiti King, tunajua mipango inayofanyika kwenye Wizara yako na nimewapigia kabisa watumishi wako, mtumishi mmoja anaitwa Masaro mwingine anaitwa Kidika, ananiambia mliipenda wenyewe, kwa kauli yake kama Mwenyekiti wa Chama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kesho yake akapiga ng’ombe za watu mnada, ng’ombe 500 zinauzwa shilingi milioni tatu, kwa nini msituite sisi ambao wenye ng’ombe tunashindwa kutoa milioni tano. Halafu mnasimama humu mnaipongeza Wizara kwa sababu gani, nataka nikuambie Profesa inawezekana ninyi mmesoma na Mungu amewasaidia hamjui uchungu wa kufuga ng’ombe kuanzia moja mpaka kumi. Hamjui watu tumeshindwa kwenda shule kwa sababu ya kuchunga ng’ombe tukawasomesha ninyi mkawa Maprofesa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na sisi Wasukuma sasa tumeamua, na nimezungumza uelewe, tutaziroga hizo ng’ombe mtavimba matumbo mnaozila huko Dar es Salaam. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani kwa nini wanunuzi watoke Dar es Salaam peke yake, yaani leo siku ya mnada watu wametoka na malori Pugu, wanajuaje kama wanakuja kushinda kwenye mnada! (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnatukamatia ng’ombe hivi hii Serikali imekosa sehemu ya kukusanya hela mpaka mkanyang’anye ng’ombe za wafugaji, haiwezekani Mheshimiwa Maghembe hata kama utanielewa vibaya lakini huo ndio ukweli. Kuna manyanyaso makubwa, mwananchi wangu wa Bukombe amepigwa risasi ya jicho hakuna fidia, aliyempiga yupo, halafu mimi nakusifu kwa sababu gani! Haiwezekani na ninaomba sana haya maneno yaingie hivo hivo nilivyoyaongea.

T A A R I F A...

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea kwa mikono miwili, nasubiri na nyingine kama hiyo. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumwambia tu Profesa kwamba ingekuwa ni mimi nateua yaani katika Mawaziri walio-fail wewe ni namba moja. Sijui ni wewe ama ni watu wanaokuzunguka ni mfumo wa hiyo Wizara sielewi. Inawezekana vipi Mheshimiwa Waziri mtumishi wako kabisa anayelipwa mshahara na Serikali unampigia simu mimi kama Mwenyekiti wa Chama namwambia kuna tatizo gani kwa nini msikae na hawa watu mkawapa ng’ombe hata wiki moja wauze watoke. Anasema hili ni agizo la Rais, hivi Rais kabisa huyu tunayemjua mwenye upendo na maskini anaewajengea watoto wa Dar es Salaam maghorofa, anayewapa watu hela, anaetoa misaada, anatuuzia ng’ombe sisi kwa sababu gani, kwa nini wasiseme watumishi wako kuwa wewe ndo umewaagiza. Na kwa nini yafanyike Kanda ya Ziwa tu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeenda Loliondo na Kamati, unataka kuwatoa wafugaji kwenye Pori la Loliondo kwa kisingizio wanaharibu ili umpe Mwarabu tukakutalia mbona hujaenda kuwanyang’anya kule, haiwezekani na hiki kitu haitawezekana. Kwa mara ya kwanza nitatoa shilingi hata kama ziko nne zote nitaondoka nazo. Nitatoka shilingi lazima uje na majibu ya msingi ni kwa nini mnatudhulumu mali zetu. Hivi kwa nini msingetupa hata kipaumbele kwama mnataka kukusanya hela za kuuza ng’ombe za watu, kwa nini msitupe kipaumbele mkatuambie njoo tarehe fulani saa fulani wote tukapambana kwenye mnada, kwa nini wanunuzi watoke Dar es Salaam?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vitu vingine vinauzi potelea mbali hata kama tutatoka humu tumenuniana lakini message imeenda inauma sana. Kwa wale waliozaliwa kwenye ufugaji mmesomea ng’ombe, ng’ombe inalelewa kama binadamu, kwa nini ng’ombe wa Tanzania anageuka kuwa adui. Akiingia Serengeti mnakamata, hivi mlishawahi kuona ng’ombe amekula Simba, kwanza ng’ombe ni chakula cha wanyama hata digidigi ng’ombe hali. Ana madhara gani ananyanyasika ng’ombe wa Kisukuma?

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua sheria pengine zinamlinda Mzee Maghembe lakini hivi vitu vinauma sana, wewe leo ukienda ku-draw hela kwenye akaunti yako ukakuta hakuna hela kuna zero, utachanganyikiwa utawekaje hata mafuta kwenye gari. Ukituuzia ng’ombe ndo benki yetu sisi ambao hatukusoma tuliishia darasa la saba, ukilima pombe una nunua ng’ombe halafu tena ng’ombe unakuja mna- deal na watu wa Dar es Salaam. Sisi tumefuga ng’ombe ili wakale watu wa Dar es Salaam, sitaunga mkono hoja yako kabisa Mheshimiwa Maghembe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, mimi nina Hifadhi kwenye Jimbo langu la Geita inaitwa Rubondo, ina Sokwe Mtu wameletwa miaka ya 1962 wanafundishwa kukutana na binadamu. Na kuna watu wanakula posho kila siku na Wizara inatoa hela. Umri wa sokwe kuzeeka yaani maisha yake niliwahi kuuliza wataalamu wakasema miaka 45 mpaka 50. Leo sokwe hawa bado wanafundishwa yaani umri wao umezidi na bado wanaishi kwa huruma ya Mungu lakini sokwe bado hawajaanza kutizamwa. Lakini kingine Maghembe, hifadhi yetu na yenyewe ni ya miaka mingi, tunahamasisha watalii wanaenda kule, kuna gari moja tu juzi umepeleka mbili haitoshi, watalii wakienda 30 mpaka wasubiriane na wakati wamekuja timu moja. Kwa nini msiongeze gari kama zilivyo kule kwenye mbuga zingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Ngorongoro huko Kilimanjaro zimejaa, kwa nini usipunguze ukaleta kwenye mbuga zetu hizo ambazo hazina usafiri na watalii wanataka kwenda huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine uwekaji wa mipaka wamezungumza na wenzangu, Mheshimiwa Waziri toka Dar es Salaam zunguka huko vijijini uje uone beacon za watu wako walivyoziweka. Sijui mna huruma ya design gani au mnataka kuipanga Tanzania kwa style nyingine. Haiwezekani vijiji vipo toka mwaka 1974 watu wamezeekea hapo wametoka maprofesa hapo na wengine ma-king kama mimi halafu unakuja kuniwekea kigingi katikati ya kijiji changu. Halafu na simama hapa nakuunga mkono, sitaunga mkono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine Profesa kuna Tume ya Wizara sita, mbona majibu yake hayatoki? Sisi tunasubiri hiyo Tume ambayo imezunguka kisanii sanii wala haijatuhoji mmeulizana wenyewe na Wakuu wa Wilaya hatujapata majibu, umeleta kutuuzia ng’ombe. Tuelekeze wapi tuzipeleke ng’ombe zetu kama unataka tuziue tununueli kwa bei tuliyofuga nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, nikiendelea hapa naweza kutoa machozi halafu huyu Mzee akapata laana. Ahsante sana.