Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi naomba nitoe mchango wangu katika hoja iliyoko mezani kwenye Bunge lako tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri ambayo inaendelea kufanyika katika mbuga yetu ya Hifadhi ya Mkomazi. Kuna wataalam kule wameenda kutatua matatizo yale ya mgogoro, kwa hiyo tunaamini kwamba kwa upande wa Lushoto, Korogwe na Mkinga, sasa maeneo yale ambayo wananchi walikuwa wanasigana na hifadhi majawabu yatakwenda kupatikana kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala lingine nilizungumza juzi kwenye semina naomba nilirudie kwamba Msitu wa Shagayu ambao ndiyo unatiririsha maji yanayokwenda kwenye Hifadhi ya Mkomazi uliungua mwaka 2012 takribani hekta 49 na zilizopandwa miti ni hekta 11 tu. Kwa hiyo, ikolojia ya msitu ule imeharibika. Niombe sana kwamba tukapande miti katika eneo lile ili angalau maji yaendelee kutiririka na kufaidisha Mbuga hii ya Mkomazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nimezungumza katika Bunge lililopita kuhusu usawa katika rasilimali za Taifa. Katika Halmashauri ya Lushoto hatuna mlango wa kuingia hifadhi ya Mkomazi, lakini hali kadhalika kwa Korogwe na Mkinga. Eneo pekee ambalo mtalii anaweza akaingia Hifadhi ya Mkomazi ni kupitia Wilaya ya Same. Sasa naomba na sisi wa Mkoa wa Tanga tupate mlango katika eneo lile la Kamakota ambayo iko katika kata ya Lunguza. Tumeshazungumza mwaka jana lakini mpaka ssa hakuna utekelezaji.

Sasa naomba sana kwamba sisi Lushoto tuna utalii wa misitu, tuna utalii wa mazingira na utalii wa miamba. Kwa hiyo ili mtalii aweze kuacha pesa ni lazima awe na siku nyingi za kukaa katika eneo fulani. Lakini anapotumia siku moja na kuondoka ina maana wananchi wa maeneo yale hawafaidiki na kuwepo kwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba sana kuwa tuongeze itinery ya matukio ambayo watalii watakuwa wanayaona katika maeneo yetu. Kwa hiyo naomba suala hili la kupata geti katika eneo la Kamakota lifanyiwe kazi ili na sisi tuweze kuchangia uchumi wa Taifa.

Lakini suala lingine ni suala hili la uhifadhi na ujirani kwamba kumekuwa na matatizo kati ya wafugaji, lakini pia na maeneo haya ya hifadhi. Sisi kule tunajitahidi angalau kujenga malambo nje ya hifadhi kwenye zile kata ambazo zinapakana na hifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawaomba TANAPA watuunge mkono katika majaribio haya ya kujenga haya malambo na majosho ili tupunguze kasi ya mifugo kuingia katika hifadhi kwa sababu kama tunavyojua hizi hifadhi zimeanza kuhifadhiwa tangu wakati wa ukoloni. Ina maana wakoloni waliona thamani zaidi kuliko labda hata sisi Tanzania huru sasa hivi tunataka kwamba kila mahali tufanye kuwa ni sehemu ya kuchungia wanyama. Ni vizuri tukaweka mipango yetu mizuri. Sisi tumepewa maarifa ya kuweza kutatua na kupanga rasilimali ardhi vizuri, lakini bila kuathiri nia njema kabisa ya kuhifadhi na kutunza rasilimali hizi za Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la concession fees kwenye mbuga zetu. Hili nalo lazima liangaliwe na kuleta pia hamasa sio tu kwa watalii wa nje lakini kwa watalii hawa wa ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na ahsante sana kwa kunipa dakika hizi tano.