Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia kidogo kwenye Wizara hii ambayo ni muhimu sana katika maendeleo ya nchi.

Kwanza napenda nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri ambayo ameitoa na mambo ambayo wanayafanya katika hii Wizara, kwa kweli nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli mchango unaotolewa na sekta hii ni mchango ambao hautoshelezi, haulingani na vivutio tulivyonavyo katika nchi hii. Nchi yetu ni nchi pekee duniani na nchi ya pili kwa kuwa na vivutio vya utalii duniani baada ya Brazil, ni nchi ambayo ina mlima mrefu katika Afrika na mlima wa pili duniani hicho ni kivutio kizuri sana. Ni nchi ambayo kwa mujibu wa wanasayansi mwanadamu wa kwanza duniani inasadikika aliishi hapa, hicho kivutio peke yake ni kikubwa sana katika nchi hii, wanasayansi wamegundua hilo, wameliona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii ni nchi yenye mbuga nyingi sana za wanyama, ni nchi ina maziwa marefu, tuna maziwa mengi, tuna bahari tuna ziwa lenye kina kirefu duniani Ziwa Tanganyika, ni nchi ambayo kule kwenye Jimbo langu la Mbozi kuna kimondo ambacho ni cha aina yake hakipo duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni nchi ambayo watalii wanakuja kuangalia nyayo za watu waliopita miaka mingi walipo kanyanga tunapata hela nyingi sana. Ni nchi ambayo tumebahatika ambayo Mwenyezi Mungu kweli ametupatia kila kitu, lakini ukiangalia mchango wake kwenye Pato la Taifa haulingani na haya yote tulionayo, mikakati tuliyonayo hailingani na hali halisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali sasa hivi kweli tumeanza kuchukua hatua za kuimarisha utalii, kwa mfano kwa sababu tumenunua ndege sasa za kusaidia kuimarisha utalii, hiyo peke yake haitoshi, yapo mambo mengi yanayotakiwa kufanyika ili kufufua utalii wetu. Kwanza lazima tuangalie kodi mbalimbali, tozo mbalimbali zinazotozwa kwenye sekta ya utalii, concession fees lazima ziangaliwe, ukilinganisha na wenzetu, ukilinganisha na Kenya, ukilinganisha na nchi zingine lazima tuangalie ni namna gani hizi kodi zinakuwa ni vivutio kwa watalii badala ya kuwa discourage, bila kufanya hivyo nchi hatuwezi kwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya kitu cha muhimu sana katika sekta ya utalii ni kuimarisha miundombinu ya utalii, miundombinu hiyo ni pamoja na kujenga viwanja vya ndege kwenye maeneo mengi ambayo hiyo nadhani Serikali imeanza kufanya, tumenunua ndege, lakini hiyo haitoshi, tunahitaji barabara nzuri zinazoelekea kwenye vivutio mbalimbali, barabara zinazopitika ili watalii waweze kupita, lazima hayo yote yafanyike kwenda kule kwenye Jimbo langu kule kwenye kimondo barabara ni mbaya, tunahitaji hoteli za maana kwenye maeneo yale. Kule kwenye kimondo hakuna hoteli, hakuna barabara, hakuna nini, ni mtalii gani atakwenda? Sasa haya yote lazima tuyafanye ili kuhakikisha kwamba tunaimarisha sekta hii ya utalii ili iweze kutoa mchango mzuri na unaokubalika katika nchi. (Makofi)

Jambo la pili, hatujafanya jitihada za kutosha za kutangaza utalii. Ukiangalia matangazo yetu mengi ambayo tunayafanya hayatoshelezi, ukiangalia bajeti yetu tunayotumia kuitangaza bado ni ndogo, vivutio viko vingi lakini hatujavitangaza kama inavyotakiwa, bila kufanya hivyo hatuwezi kufika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tulikuwa tunachangia hapa tukawa tunasema angalia tulikuwa na Serengeti Boys, vijana wetu wameenda kule wanatutangaza, lakini hebu angalia mashindano mengi yamefanyika kwenye nchi hii, kuna Olympic huwa tunakwenda, kuna mashindano ya Jumuiya ya Madola huwa tunakwenda, kuna Kilimanjaro pale huwa tunakwenda yale mashindano yalikuwa na watu wengi sana, mwaka jana nafikiri walikuwa watu 11,000 walishiriki kwenye yale mashindano, Mount Kilimanjaro Marathon walishiriki, lakini angalia jezi ambazo wanavaa watu wetu, angalia jezi wanazokuwa wamevaa hazitangazi utalii, makampuni yetu yapo wapi kutangaza huo utalii? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kuna wachezaji, kuna mmoja ameenda kule ameshiriki Uingereza ameshinda, lakini alikuwa na jezi anatangaza bia, jezi yake ile inatangaza Multi Choice ya South Africa na ametoka Tanzania, hiyo lazima tusikitike, lazima tuhakikishe tunakuwa very strategic tufanye maamuzi ambayo kweli yataisaidia katika kuimarisha nchi hii (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna michezo mingi inafanyika sasa hivi, najua tunajiandaa kwenda Japan, wenzetu Wakenya wanapoenda kwenye michezo kama hiyo huwa wanaomba mpaka space wanakuwa na space kule ya kutangaza, Ethiopia wanakuwa na space ya kutangaza wanakuwa na banda wanatangaza vituo vyao vya utalii pamoja na michezo, Watanzania tunagawa business card kwenye mabanda yetu, hatuna hata maeneo ya kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji kuimarisha ili kuhakikisha kwamba kwa kweli mambo yaende vizuri, bila kufanya hivyo tutashindwa. Sekta hii ina mchango mkubwa sana ambao ninaamini kabisa unaweza kuchangia sana katika maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tuangalie Ngorongoro, Serengeti na makampuni mengine yajaribu kudhamini michezo mbalimbali, tuna michezo mingi sana Tanzania, ikidhaminiwa tukawapa vifaa vizuri vya michezo kwa ajili ya kutangaza utalii, ninaamini tutajitahidi sana na tutaweza kufufua na kuisukuma mbele sekta yetu hii ya utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika mbuga zetu huku watalii wanapokwenda, zile huduma za msingi zinakuwa bado ni kidogo sana. Nimeangalia juzi walikuwa wanalalamika wanapopanda Mlima wa Kilimanjaro, wanapopanda wanasema kuna watalii wengine wanashindwa, wakishindwa kule hakuna hata helicopter ya kuwapa msaada, hakuna nini, hiyo inatuaharibia. Vifaa vya dharura vya kuweza kuwasaidia watalii wetu wanapokuwa wamepata dharura tuviimarishe katika maeneo yetu ili tuweze kusaidia katika hii sekta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia vyuo vya utalii nimeangalia hapa na mambo mengine mengi, ushiriki wa sekta binafsi yote ni mambo ya msingi sana, suala la msingi zaidi ili kuweza kuvutia watalii ni ulinzi na usalama ndani ya nchi yetu, bila kuwepo na usalama wa kutosha watalii wanaogopa hawawezi kuja.

Naiomba Serikali iweke utaratibu mahsusi, iweke mikakati ya kutosha kuhakikisha kwamba tunaimarisha ulinzi na usalama katika maeneo ya vivutio vyetu vya utalii na hiyo itasaidia sana kuweza kuleta mchango mkubwa na kuimarisha sekta yetu hii ya utalii ili iweze kutoa mchango mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni mambo ya msingi sana katika hii Wizara na ni Wizara ambayo inaweza ikatubeba, tukichanganya hii na ya Madini kama leo tumesikia taarifa zingine za madini tukichanganya zinaweza kusukuma maendeleo kwa kiwango kikubwa sana katika nchi yetu. Kwa hiyo, lazima mikakati ya kutosha kabisa iwekwe hapo ili kuhakikisha hii sekta inaimarika.

Suala la pili ambalo ningependa kuchangia katika hii Wizara ni suala la misitu na utunzaji wa misifu. Hifadhi ya misitu iko maeneo mengi, kule Jimboni kwetu sasa hivi imekuwa ni kero kubwa sana katika utunzaji wa misitu, ile misitu miaka ya nyuma tulikuwa na machifu walikuwa wanalinda sana ile hifadhi, wananchi walikuwa hawakati kati ovyo, sasa hivi Serikali ikaja kuanza kushughulikia inawakamata watu ovyo hadi misitu ile imeanza kuharibika. Ninaamini kabisa kama tukiwatumia na tukiwashirikisha wananchi katika kulinda ile misitu inaweza ikalindwa vizuri kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo ambalo limejitokeza sana kule Jimboni hii Wizara inatoa vibali kwa wakata mkaa, baadhi wanakata magogo, wanakata mkaa, wanauza lakini wananchi wakikutwa na mkaa wananyang’anywa na wanapigwa, wakati tayari hao wamepewa vibali, najua kuna wengine ambao wanakuwa hawana vibali lakini wapo wengine wana vibali, sasa inakuwaje wananchi wale wanaotumia mkaa wakati hawajaambiwa nishati mbadala hasa wanatumia mkaa wanakamatwa na bahati mbaya wanapokamatwa, wanaponyang’anywa ule mkaa haupelekwi Serikali. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. JAPHET N. HASUNGA Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana.