Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Omari Mohamed Kigua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu wake na timu nzima ya Wizara kwa hotuba yao ambayo imeonesha matumaini ya dhati kabisa ya kuinua sekta ya utalii, wanyamapori pamoja na misitu. Nichukue fursa hii kuchangia maeneo machache katika hotuba hii, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 59 unazungumzia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania. Kwa mujibu wa Sheria ya Misitu ambayo ilianzisha Wakala wa Misitu, lengo kubwa la uanzishaji wa TFS lilikuwa ni kusimamia na kuhifadhi rasilimali za misitu na ufugaji wa nyuki. Wakala wanatekeleza wajibu wao vema, ila yapo baadhi ya meneo nchini utendaji wa wakala unagubikwa na baadhi ya watumishi wachache kuwa sehemu ya uharibifu wa misitu na kutosimamia uharibifu wa misitu, hili ni tatizo kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano katika Wilaya ya Kilindi ambako ndiko liliko jimbo langu kuna uharibifu mkubwa wa uvunaji wa misitu ambao haufuati utaratibu. Katika Kata za Kilwa, Kilindi Asilia, Kata za Msanja na Kata za Mswaki, maeneo haya kuna uvunaji wa mbao ambao si rasmi. Wakala yupo Wilaya ya Handeni, lakini cha kushangaza mbao zinasafirishwa usiku. Hivi Wizara na Mkurugenzi wa Wakala taarifa hizi mnazo? Nimuombe Mheshimiwa Waziri na timu yake wafuatilie suala hili kwa karibu sana na ningependa kupata maelezo ya kutosha kwenye eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni Mbuga Tengefu ya Wanyama ya Saunyi. Serikali ina dhamira ya kuongeza Pato la Taifa kupitia utalii wa wanyama na kadhalika, lakini bado kuna maeneo ambayo Wizara haijayapa kipaumbele, mfano katika eneo la kitalii la Mbuga Tengefu ya Saunyi iliyopo Kata ya Saunyi, Wilaya ya Kilindi, eneo hili kuna wanyama mbalimbali, lakini sijaona jitihada za Wizara. Hivi Wizara haijui kama eneo hili lingesaidia kuinua Pato la Taifa? Wapo wawindaji wengi wanawinda isivyo rasmi, naomba Wizara itupie jicho eneo hili kwani Wizara isipofanya haya ni kuvunja moyo wananchi wa Saunyi ambao kwa muda mrefu ni wafugaji na ambao wamekuwa sehemu ya kulinda hifadhi ya mbuga hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie eneo lingine katika ukurasa wa 79 kuhusu Wakala wa Mbegu. Wakala huyu ni muhimu sana katika kuhakikisha mbegu zinapatikana za kutosha. Mbegu hizi ndizo ambazo zinatumika katika kuhakikisha maeneo ambako kuna ukataji wa miti kwa wingi ambayo husababisha kuleta jangwa. Mbegu hizi zinasaidia kupunguza athari, lakini naona jitihada za Wakala katika eneo hili ni ndogo sana. Niombe sana jitihada ziongezwe kuhakikisha mbegu zinapatikana kwa wingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo la mara kwa mara la wafugaji kuvamia misitu. Hivi kweli dhamira ya Wizara na Serikali kulinda misitu itafanikiwa kweli?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano katika Kata ya Msanja, Kijiji cha Mswaki, kuna msitu wa Bondo. Msitu huu ni wa Serikali, lakini viongozi wa Serikali katika kata hii wameruhusu wafugaji kufanya shughuli za ufugaji katika eneo hili, hivi hili ni sahihi kweli? Naomba Wizara ichukue hatua haraka ili kuhakikisha kuwa misitu hii inalindwa kwa gharama kubwa. Aidha, Wizara iweke utaratibu wa kuwa na timu katika Wizara ya kufuatilia watendaji wao ambao wana dhamana ya kusimamia misitu ya nchi yetu. Vilevile kwa wale wanaovamia misitu watozwe faini kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uvunaji wa Asali na Ufugaji wa Nyuki. Tanzania ina misitu mingi na maeneo ambayo kama ufugaji wa nyuki utasimamiwa kwa dhati tunaweza kuzalisha kiasi kikubwa cha asali. Miongoni mwa mikoa ambayo ni wafugaji wa nyuki na kurina asali ni Mkoa wa Tanga na sisi wa Wilaya ya Kilindi. Tunafuga nyuki na kurina asali pia, ila kuna tatizo moja ambalo ningependa Wizara ilifanyie kazi, nalo ni kutuletea Wataalam wa kutosha ambao watatoa elimu ya utengenezaji wa mizinga pamoja na njia za kisasa za kufuga nyuki kwa sababu, Kilindi kuna nyuki na misitu mingi sana ambayo kama jitihada za kuwekeza zitafanywa basi, tutawapa wananchi wetu fursa ya kupata mapato katika eneo la ufugaji wa nyuki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.