Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Kiteto Zawadi Koshuma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia katika hotuba ya Wizara hii ya Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi ya Utalii Tanzania bado inalo jukumu la kuutangaza utalii ndani na nje ya Tanzania. Katika ukurasa wa 100 - 107 katika hotuba ya Waziri imeeleza kwa kirefu namna ambavyo bodi imefanya kazi kuutangaza utalii wa Tanzania ndani na nje kupitia matamasha makubwa yaliyofanyika ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Mwanza ni Jiji ambalo limepewa jina la Rock City, hii ni kutokana na mkoa huo kuwa na vivutio vingi vya mawe na majabali yanayoufanya mji huo kupendeza na kuvutia kijiografia. Bismarck Rock ni jiwe kubwa linalopatikana ndani ya maji ya Ziwa Victoria, jiwe hili lilipewa jina la Counselor maarufu wa Ujerumani. Kivutio kingine ni mawe yenye maumbile tofauti tofauti yaliyobebana yanayopatikana katika Milima ya Miama, Wilayani Ilemela, Mkoani Mwanza. Huko pia kuna beach nzuri zilizotulia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kivutio kingine ni mawe yanayocheza yanayopatikana katika Kisiwa cha Ukara, Wilaya ya Ukerewe. Mawe hayo yanavutia kwa kuwa hucheza mara yanapoimbiwa nyimbo za kimila na wazee wa kimila. Kivutio kingine ni Nyumba ya Makumbusho ya Bujora. Nyumba hii inaonesha maonesho ya mila na desturi za kabila kubwa Mkoani Mwanza ambalo ni Wasukuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vivutio vingine ni Saanane Island na Kirejeshi Game Reserve ambapo wanyama mbalimbali kama vile swala, chui, twiga na simba huonekana kwa urahisi. Serengeti National Park pia inapatikana kwa umbali wa saa mbili tu kutoka Uwanja wa Ndege wa Mwanza, hivyo, kuwa rahisi kufika. Kivutio kingine ni Mnara wa MV Bukoba ambapo watu hutembelea na kutoa heshima zao kwa victims waliozama na kupoteza maisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mwanza katikati ya mji kuna mti uliotumiwa na Wakoloni wa Kijerumani kuwanyongea wahalifu. Hivyo basi, niishauri Serikali kupitia Bodi ya Utalii Tanzania kwa kushirikiana na television zote nchini pamoja na majarida ya mashirika ya ndege hapa nchini kutangaza Mji wa Mwanza kama mji wa kitalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo yote, naunga mkono hoja ya Wizara ya Maliasili na Utalii.