Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafinga Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mchango wangu wa kuzungumza, ninayo yafuatayo; TDL - Sekta ya Utalii kutoza 1.5 USD Bed Night Levy siyo nzuri kimapato. Utaratibu ungewekwa tozo hii iwe kwa asilimia kwa sababu it is unfair kwa anayelaza kwa shilingi 30,000/= anatozwa 1.5 USD sawa naye anayelaza kwa dola 50 na kuendelea, hata kiuchumi siyo sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeambiwa takwimu za watalii ni 1.2 million na kwa kuwa utalii wetu ni ule tunaitwa Low Volume High Yield. Hivi hata kwa hesabu za common citizen, kwa mfano, kwa mujibu wa takwimu katika kitabu cha bajeti ukurasa wa 136 jedwali Na. 9 wastani wa siku za kukaa watalii hotelini ni siku 10. Sasa kwa mahesabu ya haraka tuchukulie wageni 1.2 million wamelala siku tano, maana yake hizo ni a total of 6,000,000 nights ambazo ukifanya ile Bed Night Levy ya USD 1.5 per bed ambayo ni kama shilingi 3,000/=; maana yake ni 6,000,000 x 3000 = 18 billion ambayo ingeweza kabisa kutusaidia katika kuutangaza utalii, kuimarisha mafunzo hasa kupitia Chuo cha Utalii na hata kutoa ruzuku kwa wajasiriamali wa miradi ya utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba tuanzishe chombo maalum cha kuratibu TDL, chombo hiki kitabainisha njia mbalimbali za namna ya kuimarisha makusanyo kupitia TDL.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ushirikishwaji wa sekta binafsi sambamba na kuanzisha One Stop Centre, ni wazi kuwa Serikali haiwezi kujenga mahoteli zaidi ya kujishirikisha na ujenzi wa miundombinu ya barabara na viwanja vya ndege. Kwa sababu hiyo, ushirikishwaji wa sekta binafsi haukwepeki. Tufike wakati sekta binafsi tuione kama mdau na siyo adui/mwizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 23 wa kitabu, umeelezea kuhusu VAT, kuna confusion. Wadau wanasema imeathiri Sekta ya Utalii, lakini Serikali inaonesha kuwa hakuna athari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kama ilivyoshauriwa na Kamati, Wizara ikae na wadau kupitia na kujiridhisha kuhusu suala hili. Nasisitiza pia pawepo na One Stop Centre kwa ajili ya masuala ya ku-facilitate masuala ya utafiti kama ambavyo TIC; ukifika unakutana na Idara zote kuanzia BRELA, TRA na kadhalika. Tufanye hivyo katika utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati fulani nikiwa Afisa Mambo ya Nje, Mama Blandina Nyoni akiwa Katibu Mkuu Maliasili alitoa USD 10,000 (dola 10,000) kwa baadhi ya Balozi zetu kutumia kutangaza utalii, na ilisaidia sana. Kila Balozi ilitumia kadri ya mazingira. Wapo walionunua TV na kila mgeni akija kufuatilia visa, wakati anasubiri anaangalia filamu mbalimbali kuhusu utalii wa Tanzania. Nashauri tupanue wigo wa kutangaza utalii kwa kuendelea kuhusisha taasisi nje ya Wizara kulingana na mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kweli kama tunasema katika sera kuwa jamii zinazozunguka mbuga na hifadhi zitakuwa sehemu ya kunufaika, mbona hii single entry inaenda kuua kuliko kunufaika? Hoja kwamba kuna ukwepaji wa mapato bado inaweza kutazamwa hasa katika baadhi ya maeneo. Hili suala ni kama vile kuwalinda wawekezaji wakubwa na kuwamaliza wawekezaji wadogo na hasa wanavijiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya Mheshimiwa Ryoba ni ya msingi na muitazame. Leo hii ufugaji unaongezeka badala ya ng’ombe 500 kama ilivyokuwa awali. Kuna ng’ombe 8,000 matokeo yake ni nini? Wataanza kuingia kwenye hifadhi, dhana ya conservation kama matokeo ya WMA. Hii itazamwe upya, tuwe open minded, tufikirie zaidi namna bora ya kudhibiti upotevu wa mapato lakini kwa kuzingatia ustawi wa jamii zinazozunguka hifadhi.
Kuhusu misitu vs vibali; kwanza nashukuru ushirikiano ambao Mafinga tunapata kutoka Sao Hill na TFS. Tumepokea madawati na Halmashauri yetu iko tayari kutoa eneo kwa ajili ya Ofisi ndogo na parking kama sehemu ya ushirikiano. Nimesoma kijitabu na niliitwa na Kamati kuhusu utaratibu wa upatikanaji malighafi Sao Hill, hata hivyo nashauri kuwa pamoja na utaratibu huo, usawa na uwazi (fairness na transparency) ni muhimu sana. Siyo sawa mtu mmoja (sitamtaja) alijidai kuwa eti ana mkataba na Serikali (TFS) apewe ujazo mkubwa kisha awauzie wengine tena kwa majigambo makubwa kwamba wataendelea kumtegemea yeye. Hili halikubaliki! Ni vizuri mgao wa malighafi uzingatie uwezo wa kiwanda na sio umaarufu wa mtu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kutotoa mgao kwa vikundi, pamoja na kuwa ni sheria/kanuni, nashauri suala hili litizamwe upya. Ni muhimu sana kutenga kiasi kidogo kwa ajili ya makundi ya mahitaji maalum kama wenye ualbino na vikundi vya wajane as CSR (Corporate Social Responsibility).
Suala la wanachi kupata vibali ndipo wavune miti yao sio sawa na litatuletea mgogoro na wananchi bila sababu yoyote. Nimechangia kwa kuzungumza, lakini nasisitiza maamuzi kama haya yawe shirikishi kuliko ku-impose tu. Mtu ana shida, anataka kuuza msitu wake atatue shida yake, why tumwekee mlololongo? Je, capacity hiyo mnayo? Tutafakari upya na nakuletea tangazo hilo, barua Na. TFS/ SH2/MUF/MSC/VOL.1/113 ya tarehe 9 Mei, 2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi kuwa hatuwezi kumrejesha mjusi aliyeko Ujerumani. Ushauri wangu ni kwamba shirikianeni na Wizara ya Mambo ya Nje, Wajerumani walishaonesha nia kwamba pale kwenye shimo alipotoka yule mjusi pajengwe reception na hoteli ambayo itatumika na wageni watakaopenda kuona lile shimo alipotoka mjusi. Jambo hili linataka utashi tu na linawezekana na litaongeza idadi ya watalii na hivyo kuongeza mapato.
Pili, Wajerumani pia wako tayari kutoa funds lakini specifically kwa ajili ya kuimarisha masuala ya archeology na conservation. Yote hayo ni in connection na huyu mjusi. Aidha, Mheshimiwa Dkt. Mwekyembe anaweza kuwa msaada katika suala hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, iwe ni kwenye misitu, uwindaji au utalii kwa ujumla ni vizuri viongozi wa kuchaguliwa kuanzia Wenyeviti wa Vijiji/Mitaa, Madiwani na Wabunge washirikishwe ipasavyo hasa katika maamuzi yanayokusudiwa kufanywa, yanaathiri maisha ya wananchi kwa asilimia 50. Mfano, suala la mkaa, vinyungu, single entry na kadhalika. Naomba kuwasilisha.