Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tabora Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami pia nakushukuru sana kwa kuniruhusu nichangie Wizara hii ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambayo kwa kweli ndiyo msingi wa maisha ya Watanzania wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kuendelea kuchangia napenda pia nitoe shukrani nyingi kwa Mheshimiwa Rais na Mawaziri wote wa Wizara hii ya Elimu. Vile vile nijikite kwenye mambo haya manne ambayo nitayaongelea, moja shule za ufundi lakini mambo ya VETA, tozo ya SDL na mimba za utotoni. Naomba nianze na suala hili la mimba za utotoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge hili limekuwa linaomba tuletewe sheria itakayozuia watoto kuolewa wakiwa wadogo. Bunge hili limepitisha sheria kali sana kwamba mtu ambaye atampachika mimba mtoto wa shule, afungwe miaka 30.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshangaa, watu wanachangia tena Bunge hili linaruhusu watoto kupata mimba wakiwa mashuleni. Hii ni kinyume! Bunge linaomba tulete Sheria ya Kuzuia Watoto Kupata Mimba lakini Bunge hili hili leo linataka tupitishe kanuni au ruhusa watoto wapate mimba shuleni. Tunajikanyaga! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ku-declare interest kwamba mimi ni Muislamu na niko wazi kabisa na nina hakika dini zote zinakataza mambo ya zinaa kabla ya ndoa. Kwa hiyo, ni vigumu sana mimi kwa imani yangu ya dini kuruhusu watoto hawa watiwe mimba halafu warudi shuleni. Ina maana niwaruhusu wapate mimba kabla ya kuolewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaunga mkono kama Bunge hili litaruhusu watoto wa shule waolewe, wazae ndipo warudi shuleni. Kinyume chake ni kosa kubwa sana. Pia nimepitia takwimu; wanasema kama huku-research usiseme; tatizo la mimba shuleni mwaka 2015 jumla ya watoto wote wa primary and secondary school 3,937 ndio waoliacha shule kwa sababu ya kupata mimba, lakini watoto walioacha shule kwa makosa mengine ya utoro 139,866. Hili ndiyo tatizo kubwa sana, siyo la mimba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuruhusu watoto wapate mimba warudi shuleni, itaharibu nidhamu ya shule kabisa. Watoto sasa hivi wanaogopa kupata mimba kwa sababu wanajua watafukuzwa shule, sasa tukiruhusu wapate mimba wakasome, itakuwaje? Serikali imeshaweka muundo wa watoto wanaopata mimba wakarudi nyumbani kama mama watoto, wasome elimu ya watu wazima ambayo inaanzia Shule ya Msingi mpaka Chuo Kikuu, wanakosa nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kuruhusu watoto walioitwa mama, wanajua mambo yote ya kulea mtoto wakakae darasa la saba tena, haiwezekani!
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kidini nakataa, lakini Bunge hili limelaumiwa kutunga sheria zinazokanganyana zenyewe; huku tunakataza watoto wasifanyiwe zinaa wakiwa wadogo chini ya miaka 18 na mtu akifanya kosa afungwe miaka 30. Huku tunaruhusu hiyo tena ifanyike kuwa watoto wapate mimba warudi shuleni. Hii sheria itatukanyaga wenyewe, haiwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa maoni yangu ni kwamba watoto hao wanaoacha shule kwa kupata mimba wafukuzwe kabisa. Waliowatia mimba wafungwe miaka 30 na watoto wasirudi shuleni kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ni la kwanza. Naomba sasa niongelee mambo ya Elimu ya Ufundi. Mfumo wa elimu unaotolewa sasa hauwezi kulingana na matakwa ya Mheshimiwa Rais ya kujenga nchi ya viwanda na hili naomba lisikilizwe vizuri sana. Mimi ni zao la Elimu ya Ufundi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka iliyopita kulikuwa na Shule ya Ufundi, Moshi; kulikuwa na Shule ya Ufundi, Ifunda. Shule zote zilikuwa zikipeleka wanafunzi waliotoka Form Four kwenda Chuo cha Ufundi (Technical College) na hao walichagua ufundi tangu mwanzo, walikuwa kama Fundi Umeme miaka minne ya Sekondari, inaitwa Trade School, baadaye kama wewe ni Civil Engineer, utaanzia mambo ya engineering kuanzia form one.
Mheshimiwa Mwenyekiti, michoro wanayochora Chuo Kikuu leo ya technical drawing niliichora nikiwa Form One. Tulikwenda pia Chuo Kikuu cha Ufundi (Technical College) tukachukua miaka mitatu, tukajaliwa watoto wanaoitwa Mafundi Sadifu (Technicians).
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, tumefanya kazi nje, tukarudi tena Chuoni, tukasoma Diploma ya Engineering. Kwa hiyo, tuna miaka 10 katika ufundi uliochagua ukiwa form one. Kama ni electrical, ni miaka minne form one mpaka form four, kama ni Civil, ni miaka minne form one mpaka form four, lakini miaka mitatu ya ufundi inakuwa jumla saba. Ukirudi kuchukua Diploma, una miaka kumi katika ufundi. Tulizalisha mafundi kama mimi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na mifumo miwili ambayo ilikuwa inajulikana waziwazi. Mfumo wa Academicians form one mpaka form four, form five, form six na Chuo Kikuu cha Engineering au cha Udaktari. Ufundi tulianzia Sekondari ya Ufundi, Chuo cha Ufundi, unarudi unapata fundi anaitwa Diploma Engineer, hawa ndio ambao wanaendesha kampuni nyingi mnazoziona leo, ndiyo wako viwandani. Mfumo huu ulifutika kwenye Awamu ya Pili ya Uongozi wakati Mheshimiwa Mungai (Marehemu) alipofuta shule za ufundi zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi suala hili haliwezekani tena. Tuna Artisan kutoka VETA. Hawa watu wa VETA ni wa chini kabisa katika Elimu ya Ufundi, lakini baadaye kutoka hapa mpaka hapa, hakuna ma-technician, mafundi sadifu hawapo.
Mheshimiwa Rais anaongelea ufundi, viwanda vya ufundi, viwanda vya kuzalisha mali; wanaoendesha viwanda hivi ni mafundi sadifu. Mafundi VETA wana-repair mashine zikiharibika na kadhalika. Namwomba Mheshimiwa Rais afikirie kuendeleza elimu ya viwanda, afikirie kurudisha mfumo wa zamani wa Diploma Engineers ambao walifanya kazi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, sisi waajiri tunaona kwamba VETA kuwekwa chini ya Wizara ya Elimu ni kosa. Kufanya kosa siyo kosa, kujisahihisha ni bora. Tunapenda VETA iwe chini ya Wizara ya Kazi na Ajira ambako ndiko tunafanya uendelezaji wa stadi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu Kenya Polytechnic walilinda mambo hayo na matokeo yake, hela tunayochanga sisi kama SDL inakwenda kusomesha watoto High Learning Institution, tungependa sisi hela yote iende VETA, lakini vile vile tungeomba pia VETA yote katika mfumo mpya wa kuanzisha Mfumo wa Elimu ya Ufundi irudi tena katika Wizara ya Kazi ambako ndiko tunaendeleza stadi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi waajiri tunapata taabu sana katika suala hili, tunaona kwamba VETA imewekwa sehemu ambayo labda kwa makosa ambayo hatuyajui, lakini tunaomba sasa VETA irudishwe tena Wizara Kazi ili iweze kuendeleza ujuzi wa wafanyakazi lakini vile vile ujuzi wa wanafunzi wapya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, mimi bado naumia na tozo. Najua tunaongelea tozo ya SDL ambayo iko chini ya Wizara ya Elimu. Napata ukakasi! Ningependa kuongelea tozo ikiwa chini ya Wizara ya Kazi, lakini iko Wizara ya Elimu. Hii inatupa tabu sisi waajiri kuchangia kwa sababu tunaona tozo hii inakwenda kwingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, lakini vile vile naomba sana Serikali ichukue ushauri ambao nimeutoa. Ahsante sana kwa kuniruhusu niongee.