Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TAUHIDA CASSIAN GALOSS NYIMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii kwa kuchangia Wizara ya Elimu. Kwanza kabisa nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa kazi kubwa na jitihada yao wanayoifanya, kwa kweli sisi kama Watanzania tunaiona wenyewe kwa macho. Kinachonifurahisha na kuniridhisha zaidi ni kwamba Mawaziri wote wawili ni wanawake. Mara nyingi wanapofanya kazi wanawake mimi kama Tauhida huwa najisikia ufahari mkubwa lakini hatuachi kusema mambo madogo madogo ili waweze kuyafanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mimba kwa watoto wa kike linahitaji umakini kwenye kutoa uamuzi. Ukiangalia suala hili kwa pande zote mbili kwa hoja zinazojengwa basi kila mmoja ana tafsiri yake. Naamini kwamba Waheshimiwa Wabunge ni watu makini na watatoa maamuzi sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye ukurasa wa 28 na 29 wa Taarifa ya Kamati, kuna sheria zinazomhusu mtoto wa kike, naomba ziangaliwe na zifanyiwe kazi. Nasema zifanyiwe kazi kwa sababu sheria ambayo ilitakiwa iletwe ni anayempa mimba mtoto wa kike kuwekwa ndani. Imani yangu ni kwamba atakayempa mimba mtoto wa kike akiwekwa ndani nina uhakika kwamba suala la mimba kwa wanafunzi litakoma au suala la mimba kwa watoto wa kike litakoma kwa sababu mtiaji mimba ataogopa kuwekwa ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niseme kwamba ifike wakati kama wananchi na Watanzania tukubaliane kwamba mtoto wa kike anatakiwa apewe elimu ya kutosha, tusiwe watu wa kufumba maneno. Suala la kufumba maneno ndiyo limetufikisha hapa leo kutokubaliana.
TAARIFA...
MHE. TAUHIDA CASSIAN GALOSS NYIMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Mchengerwa kwa ufafanuzi na maelezo mazuri, nayakubali kwa kuwa mwanasheria ametoa jambo la ziada zaidi kutukumbusha, naikubali taarifa yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri Mheshimiwa Waziri amesikia kwa sehemu, naomba aweke mkazo kwenye maeneo hayo, yeye ni mama, ni mwanamke, hatupendi kuwa na Taifa wanawake wakakosa fursa ya kufanya kazi, kwa sababu tu ya hali ambayo wao hawakupendezewa nayo na wala hawakukubaliana nayo. Umri mtoto anaopata mimba ni mdogo, anarubuniwa, nafikiri ni wakati wa kulishawishi Bunge hususan wanawake wenzangu tuliotoka kwenye Viti Maalum kwamba tuje na mikakati ya makusudi na sheria za makusudi, mtoto mwanamke atafutiwe jinsi ya kulindwa aendelee na masomo yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tusiamue kwa utashi tu, tusifikie wakati tukaamua bila kujua nini athari yake mbele. Ningeridhia sana kama ingekuwa bakora hii na sisi tuliokuwemo ndani ingetukamata. Nazungumza kama ingetukamata kwa sababu watoto wengi wanaothiriwa na hili ni watoto wa vijijini, watoto wa kimaskini. Nazungumza hivi Mheshimiwa Waziri kwa kuwa tunaishi mitaani tunaelewa nini kinachoendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mtoto yeyote wa mtu aliyepo humu ndani, tena namshangaa baba yeyote anayesimama humu ndani akadhani kwamba hakielewi kinachoendelea kule nje. Mtoto anayepata fursa ya kusoma ni mtoto wa mwenye pesa, ndio anayepata fursa ya kusoma, tufikie wakati tuwafikirie na walioko chini. Nazungumza mtoto yoyote wa mwenye pesa akishika ujauzito, ikifika mwezi mmoja au miwili anaenda kutolewa mimba kimya kimya inapita, baba ndani ya nyumba yake haelewi mtoto wake kama katolewa mimba maana haugui lakini isitoshe mtoto huyo huyo atatafutiwa shule ya mbadala kwenda kusoma. Inaniwia vigumu kutokuitendea nafsi yangu haki, nataka apewe fursa mtoto wa kike kuendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, kwangu mimi ni kigezo Wabunge wangapi wa kike humu mnaendelea kusoma. Wabunge mmebeba mimba zaidi ya tano ya sita mmezaa na mnakaa na waume zenu. Tuwatafutie mustakabali watoto wa kike tunawafanyaje, tunawasaidiaje? Huwezi kuwa Mbunge wa Viti Maalum uliyeteuliwa na wanawake wenzio… (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.