Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kahama Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza natoa shukrani nyingi kwa kunipatia nafasi hii ya kuchangia katika Wizara ya Elimu.
Kwanza napenda kutoa shukrani nyingi kwa Serikali kwa kutoa elimu ya bure kutoka darasa la kwanza mpaka la kumi na kbili. Mpango huu wa elimu bure umetusaidia sana kupunguza kero nyingi majimboni kwetu pia Serikali kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ya Tanzania kama haitafanyiwa mabadiliko makubwa itaendelea kuwa chanzo cha mateso, umaskini kwa wazazi, watoto na kurudisha nyuma maendeleo ya nchi yetu. Wakati wakoloni walipoleta elimu zaidi ya miaka 100 iliyopita walikuwa na maana nzuri sana, leo baada ya mabadiliko makubwa ya dunia, uchumi na teknolojia kwa ujumla wake ni vigumu sana kuendelea na mfumo wetu wa elimu hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano kwa nchi ya Uingereza; wanapomaliza wanafunzi mfano, milioni moja kutakuwa na retirement ya wafanyakazi karibu laki tisa au laki tisa na nusu ambao ni asilimia 90 mpaka 95. Kwa hiyo, wale wanafunzi laki moja ambao watakuwa hawana ajira watakuwa chini ya Serikali wanaweza kulipwa na kutafutiwa kazi polepole.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wetu, wakimaliza wanafunzi milioni moja kutoka chuo na shule zote watakaopata kazi ni wanafunzi 50,000. Kwa maana hiyo ajira yetu ni asilimia tano peke yake ya wanafunzi. Kwa tofauti hii ya uwiano wa ajira kati ya waliotuletea mfumo huu wa elimu na waletewa, hata ikitokea miujiza hatuwezi kutengeneza ajira hata kwa asilimia 20. Ni jukumu la Wizara kuchukua mawazo ya Wabunge yanayoweza kufanyiwa maboresho ili kulitatua hili tatizo ambalo ni kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tunaotoka Mikoa ya Kanda ya Ziwa tungeomba kutoka darasa la kwanza mpaka kidato cha nne kwa shule za kutwa tupewe elimu ya kawaida na tupewe elimu ya mazingira yetu. Kanda ya Ziwa tuna shughuli zetu za kawaida kama ufugaji, uvuvi, biashara, madini, tungeomba Wizara ya Elimu itupatie elimu hii kutoka darasa la kwanza ili mtu anapomaliza form four awe ana-balance ya elimu mbili. Kwa hiyo, ataamua mwenyewe aendelee kwenda kwenye ajira ya Serikalini au sehemu nyingine au arudi akajiajiri kuliko mtindo wa sasa hivi baada ya mtu kumaliza university anarudishwa nyumbani. Akirudi nyumbani anakukuta wewe mzee umezeeka, huna kitu cha kufanya anakuja na karatasi inayoitwa degree. Tatizo hili ni tatizo la Watanzania wote, kila mtu ni mwathirika wa hili tatizo.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunamuomba Waziri ajaribu kuangalia upya muda wa kukaa shuleni. Kama hatuna ajira ingekuwa vizuri mtoto amalize university akiwa na miaka 15 au 17 ili awakute baba na mama yake at least wana nguvu kwa maana hakuna kazi ili waendelee pamoja akiwa bado mdogo ni rahisi kufanya naye kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna tatizo la watu wa vyuo vikuu; vyuo vikuu vinaendesha nitaita kama aina ya utapeli mamboleo. Wanachukua pesa kwa wananchi, wanalazimisha wananchi kukopa, wanachukua pesa, shilingi milioni 10 mpaka shilingi milioni 30, baada ya miaka mitatu wanakurudishia mtoto ana karatasi inaitwa degree. Wao ndiyo kiwanda pekee kilichobaki duniani ambacho hakiwezi ku-suffer, viwanda vyote vinateseka sasa hivi lakini vyuo vikuu hakuna mahali vinateseka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Wizara ilete sheria hapa ili wanapotaka kusajili hao wanafunzi waeleze kazi walizonazo ili wao waende kwa waajiri waende wakatafute hizo kazi kabla hawajasajili wanafunzi. Waeleze mshahara ndiyo waseme sasa lipa kiasi hiki mtoto wako atakwenda kufanya kazi hapa. Hii itasaidia ndugu zetu maprofesa na wamiliki wa vyuo kulijua soko la ajira, itabidi wakakutane na waajiri. Kwa sasa hawakutani na waajiri, wao wanatayarisha wanafunzi wanaacha wazazi na wazee wote nyumbani wanakuwa maskini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, usukumani tunakaribia kumaliza ng’ombe, tunalipia vyuo tunabaki na karatasi inayoitwa degree, lakini ukienda kwa mwajiri akiikataa ina maana hiyo degree ni valueless (haina thamani yoyote). Kwa hiyo, tungemuomba Waziri alete sheria hapa Bungeni ili vyuo vikuu viweze kubanwa na vyenyewe viende vikatafute ajira, badala ya mtindo wa sasa hivi wa vyuo kutumia nguvu ya Serikali na mawazo ya kusema elimu ni ufunguo wa maisha, matokeo yake sasa elimu ni kibano cha maisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongelea kidogo suala la VETA; humu ndani wote tuna magari, lakini sijasikia mtu yeyote anasema anapeleka gari yake VETA, wote tunauliza wapi ambapo kuna garage nzuri ya Toyota tunaambiwa ipo Mwembeni, tukifika pale Mwembeni hatuulizi cheti chochote, ningemuomba Waziri awafikirie sana watu wa garage maana yake ndio wanaofanya kazi kubwa kwa sasa hivi. Kama wao anaweza kuwa-indicate kama VETA ili wanafunzi wetu wakaenda kwenye garage za Miembeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, uzuri ni kwamba garage hizo hazina masharti yoyote ya kusoma, unaweza kusoma miezi sita kama umeshaelewa unaweza kuendelea na shughuli zako. Tofauti na sasa hivi unapeleka mtoto VETA kujifunza kupaka rangi miaka mitatu, fundi bomba miaka mitatu akirudi anakuta teknolojia ya bomba imeshamalizika inakuwa hakuna chochote. Hawa wakiona ametoka VETA wote huku mtaani hawamtaki, wanasema huyu ni soft, lakini anayetoka kwenye garage anapokelewa vizuri sana maana yake ni practical. Tunaweza kuwapeleka kwenye maeneo ya sofa, maeneo mengi sana ambayo yapo sasa hivi, yanatosha kabisa kuweza kusaidia VETA badala ya mtindo wa sasa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, namuomba Waziri, pamoja na yote hayo, anisaidie kwenye Jimbo langu la Kahama shule Nne za sekondari ambazo zimekuwepo kwa muda mrefu kuwa High School.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu ni huo kwa leo, nashukuru sana.