Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Abdallah Ally Mtolea

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Temeke

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona dakika hizi za lala salama nami niweze kuchangia mawili matatu katika Wizara hii inayoshughulika na mambo ya elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapotokea mjadala hapa wa kuitaka Serikali ibadilishe Sheria ya Ndoa ili ukomo au mwanzo wa umri wa kuolewa uwe kuanzia miaka 18 na kwenda juu kuna kundi huwa linapinga sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya kundi hilo linalopinga kupandisha ukomo wa kuolewa watoto wa kike ndiyo hilo linapinga watoto wanaopata ujauzito kurudishwa tena shuleni. Tafsiri tunayoipata hapa ni kwamba kumbe wabakaji na wanaotutilia mimba watoto wetu inawezekana wengine wapo humu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge kama wazazi, mtu kuanza kupinga kumpa fursa mtoto wa kike ambaye pengine alifanya kosa kupata mimba au ilitokea bahati mbaya amebakwa, unasimama mapovu yanakutoka hapa eti hutaki mtoto huyu kurudi tena shuleni ni jambo la aibu sana.

TAARIFA...

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza unaposema Bunge lililopita maana yake una-refer Bunge la Kumi, Bunge la Kumi Mheshimiwa Mchengerwa hakuwa Mwenyekiti na wala hakuwa Bungeni.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika haya maisha tunayoishi hatushindani kutokufanya makosa, tunashindana kwa namna gani unajifunza kutokana na makosa ambayo umeyafanya. Hivi ni nani amefanya kosa la makusudi kati ya aliyebakwa akapata au kijana anayejifunza kuvuta dawa za kulevya? Serikali hii juzi tumepitisha hapa bajeti ya Wizara ya Afya, Serikali inatenga pesa kwa ajili ya vituo vya methadone, inatumia mamilioni ya fedha kwa ajili ya kuwapa fursa vijana ambao wametumia dawa za kulevya sasa wanatafuta nafasi ya kujifunza kutokana na makosa yao, wanatafuta nafasi ya kujirekebisha ili wawe raia wema. Ndiyo kazi ya Serilkali kuwajengea miundombinu wananchi ili waweze kuwa wananchi bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mtoto aliyepata mimba ama kwa kubakwa au kwa kurubuniwa unamnyimaje fursa ya kurudi shuleni?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusimalize maneno kwa sababu tu mtoto wako anasoma shule nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusiwe wageni wa nchi hii, Waziri wa Elimu anafahamu, moja ya changamoto kubwa za elimu katika nchi hii ni kwamba hizo shule ziko mbali na watoto wetu wanakoishi. Watoto wanatembea umbali mrefu kuzifuata shule, hakuna hostel za kutosha kwamba hawa watoto wakae hostel wasome huko mpaka wamalize shule zao. Mtoto anapewa lift ya bodaboda mwaka mzima, hivi mtoto huyu kweli ana ujasiri gani atakataa kutongozwa na dereva wa bodaboda anayempa lift kwa mwaka mzima? Wewe mtu mzima pamoja na Ubunge wako hapa ukipewa lift mfululizo siku 30 tu lazima mtakuwa bwana na bibi. Leo mtoto mdogo, watoto hawa wadogo wanarubuniwa, wanapata mimba, tunashindwa kweli kuwa na huruma kweli?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukru sana na ukijiona unanyeshewa wewe ingia ndani, ujue upo nje, ndiyo maana manyunyu yanakukuta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira ambayo watoto wetu wanakwenda shuleni siyo rafiki kiasi hicho, kwamba unaweza ukadhibiti wasipate mimba. Wakati Serikali inaendelea na jitihada zingine za kuhakikisha watoto watakuwa wanapata hostel, shule zitakuwa karibu na makazi yao, pia tuwape fursa wale ambao tayari wameshapatwa na matatizo. Inatugharimu kiasi gani...(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.