Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MAKAME MASHAKA FOUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuchaguliwa kwa kura nyingi na kuwa Rais wa Tanzania. Pia namshukuru Mungu na wananchi wa Jimbo la Kijini kwa kunichagua kuwa Mbunge wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo ni uti wa mgongo wa wananchi wa Tanzania. Serikali ikipe kipaumbele zaidi kwani zaidi ya 60% ya Watanzania wamejiajiri katika kilimo. Kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, naishauri Serikali kuweka kipaumbele kwenye kilimo cha umwagiliaji pia kutenga maeneo maalum hasa yenye ukosefu mkubwa wa mvua ili vijana wa maeneo hayo wapate kilimo chenye tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana ni nguvu kazi kubwa ya Taifa. Wako vijana wengi waliomaliza kusoma hawana kazi. Naishauri Serikali iweke utaratibu au mkakati wa kuhakikisha vijana wote wenye uwezo wa kufanya kazi wanafanya kazi na mkakati uanze vijijini hadi Taifa. Hali hii itasaidia vijana wengi kutokuhamia mjini na kuzurura hovyo mitaani. Naishauri Serikali iweke utaratibu maalum kwa kuwapatia taaluma nzuri ya uvuvi wa kisasa vijana wetu wanaoishi Ukanda wa Pwani ili wavue uvuvi wenye tija. Kwani uvuvi wa kizamani hauna tija kubwa kwa hivi sasa, mfano uvuvi wa madawa, kuchokoa kwa miguu umepitwa na wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, imefika wakati sasa kuchukua hatua kali kwa wafanyabiashara wa madawa ya kulevya kwani vijana wengi hivi sasa wanaathirika kiakili, wanakuwa wezi, wabakaji kutokana na kutumia madawa haya ya kulevya. Hivyo, naiomba Serikali isiwe na muhali kwa wasafirishaji na wasambazaji, wote wachukuliwe hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kuanzia Serikali ya Mitaa hadi Taifa ifanyie kazi kauli mbiu ya Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli isemayo Hapa Kazi Tu inayoenda sambamba na kutumbua majipu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja.