Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Mwenyekiti,naipongeza Serikali kuja na Mpango wa Pili mzuri wa Maendeleo, ambao utagusa maeneo mengi, ikiwemo Ilani ya uchaguzi tulioinadi mwaka jana 2015. Pia napongeza Hotuba ya Waziri Mkuu ambayo inaonesha commitment ya Serikali kwa wananchi wake. Hatua hii na hatua nyingine mbalimbali ambazo Serikali imeendelea kuchukua, imesaidia kuwapa Watanzania mtazamo mpya wa kufanya mabadiliko kuanzia kwenye ngazi ya familia.
Mheshimiwa Mwenyekiti,rasilimali watu, naomba na kuishauri Serikali iangalie kuboresha maslahi ya watumishi ili waweze kushiriki kikamilifu katika kuchangia ukuaji wa uchumi. Na-declare interest mimi ni mhasibu, mkulima na mfanyabiashara pia.
Naishauri Serikali iwatazame kwa jicho kuu watumishi wa Idara ya Takwimu, kwani ikiboreshewa vifaa na huduma wataisaidia Serikali kupata taarifa muhimu zinazohusu hali ya uchumi, changamoto, pamoja na namna ya ufafanuzi wa changamoto kwa wakati. Pia kada ya uhasibu itazamwe, itumike kuisaidia Serikali, kada hii inatumika zaidi kwa sasa kuandaa taarifa tu na hawatumiki kwenye maamuzi, kwani hawaonekani kama viongozi kwenye idara na agency za Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti,huduma za jamii katika Jimbo la Ushetu; maeneo ya Majimbo, Halmashauri za Wilaya zilizopo nje ya Makao Makuu ya Wilaya zimesahaulika na Serikali kuendelea kuamini huduma zikifika Makao Makuu ya Wilaya mwonekano unakuwa huduma imewafikia wananchi wengi, hivyo naomba yafuatayo Ofisi ya Waziri Mkuu iyazingatie:-
(a) Kwanza, afya, tunahitaji tupatiwe hospitali ya Wilaya katika Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, katika Kituo cha Afya cha Mbika, Kata ya Ushetu. Kituo hiki hivi sasa kinahudumia Jimbo la Ushetu na Majimbo jirani ya Ulyankulu na Urambo. Hospitali ya Wilaya ya Kahama pekee imezidiwa kwani inahudumia Wilaya za Mbogwe, Bukombe, yaani wagonjwa wa nje na ndani ni 600 kwa siku.
(b) Huduma ya utawala; tunaomba kupewa Wilaya ya Ushetu ili usimamizi na uratibu wa shughuli za huduma na maendeleo zisimamiwe vizuri. Tuliahidiwa kupewa Wilaya baada ya kupewa Halmashauri ya Wilaya na Jimbo, jambo ambalo limekamilika (rejea hotuba wa Waziri Mkuu ya 2010/2011).
(c) Ujenzi wa barabara kutoka Mpanda- Ulyankulu- Ushetu - Kahama kwa kiwango cha lami; kama ilivyo kwenye Mpango wa Maendeleo na Ilani ya Uchaguzi, barabara hii itajengwa. Hata hivyo, inaonesha usimamizi wa barabara hii itakayohusu mikoa mitatu, yaani Katavi, Tabora na Shinyanga, inaonesha usimamizi unasimamiwa na Meneja TANROAD Katavi.
Mheshimiwa Mwenyekiti,nashauri ifuatavyo:-
(i) Usimamizi ufanywe na mameneja wote, kila mmoja eneo la mkoa wake na kuwe na project tatu ili usimamizi na uwajibikaji upimwe kimkoa.
(ii) Ujenzi uanze kwenye kila Mkoa husika ili huduma kwa wananchi iende kwa uwiano.
(d) Ushirika; suala la ushirika litazamwe, tuwe na ushirika kwenye sekta zote, wafugaji hawana ushirika madhubuti, hivyo wasaidiwe kikamilifu.
(e) Maji; maji yaliyotoka Ziwa Victoria yamefikishwa Wilayani Kahama, kwa nini yasisambazwe kwa wananchi wa Jimbo la Ushetu.
Mwisho, naunga mkono hoja. Taarifa yangu iingizwe kwenye Kumbukumbu Rasmi za Bunge.