Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Desderius John Mipata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa mchango kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni Serikali imefuta shule ya sekondari ya Milundikwa ikiwa na kidato cha kwanza hadi cha sita na kuua kabisa matarajio ya watoto katika ngazi zao mbalimbali walizokuwa wamefikia bila kuangalia performance nzuri sana ya shule hii. Ikiwa na miundombinu yenye thamani ya shilingi milioni 871. Naitaka Wizara inisaidie kurudisha miundombinu mbalimbali iliyokuwa imejengwa na wazazi ikiwemo madarasa, mabweni, maabara, vyoo, maji na mambo kadhaa ambayo sasa wanafunzi wameyakosa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishauri Wizara itafute wadau mbalimbali kokote wanaoweza kupatikana ioneni kwa jicho la huruma, Mheshimiwa Waziri mpaka sasa sijaona mchango wa Wizara yako, kazi zinazoendelea kwa sasa ni kiduchu tu, bado kazi ni kubwa kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni miundombinu ya elimu Wilayani Nkasi (Nkasi Kusini kwa upekee) ni hatari na pamoja na mchango huu, naomba kuambatanisha na hali ilivyo mbaya kwa takwimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule za msingi idadi ya watoto darasa la awali hadi darasa la saba ni watoto 80,604. Idadi ya walimu mahitaji ni 1,791; waliopo 1,089 na upungufu ni asilimia 39. Takwimu za vyumba vya madarasa mahitaji ni 1,791; vilivyopo 655; upungufu ni 1,136 ambao ni sawa na asilimia 63.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wamejenga maboma 273 vya vyumba vya madarasa ili kukabiliana na hilo tatizo, tunaomba tupanue kupunguza kero hiyo, kadhalika takwimu za nyumba za walimu, mahitaji 1,089 zilizopo ni 392 upungufu 697 upungufu asilimia 64. Wananchi tumejenga maboma mengi bado kupauliwa, tunaomba mtusaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu sekondari; idadi ya shule ni 23 na 22 ni za Serikali moja tu ni ya binafsi. Jumla ya wanafunzi waliosajiliwa mwaka 2017 wanaume ni 1,345 na wanawake 1,174 jumla ni 2, 519. Idadi ya kutoka kidato cha kwanza hadi cha sita wanaume ni 3,854 na wanawake ni 3,141 na jumla ni 6,995.

Mheshimiwa Mwenyekiti, walimu wa sayansi waliopo kwa sasa ni 14 tu wanahitajika walimu 95 tusaidie. Takwimu za nyumba za walimu, mahitaji ni 366, zilizopo 89, upungufu 277, sawa na asilimia 75.6. Tuna maboma 36 tunaomba tusaidie kupaua. Maabara mahitaji ni 66 zilizopo ni tano upungufu 61. Kila sekondari kuna ujenzi wa maabara wameshindwa kumalizia tunaomba msaada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtoto wa kike kushindwa kumaliza shule kwa tatizo la mimba tulishughulikie kama Zanzibar, tusiwahukumu watoto wa kike mbona watoto wa kiume wanawapa mimba na wanaendelea na kusoma nani atamsaidia binti wetu asome? Pia walemavu wasaidiwe.

Jimbo la Nkasi Kusini linapakana na Ziwa Tanganyika kwa upande wa Magharibi ambapo kata zilizoko kando kando ya ziwa zina changamoto nyingi zikiwemo, mawasiliano ya simu (kata ya Kala).

Mheshimiwa Mwenyekiti, mawasiliano ya barabara ambazo siyo nzuri, nyumba za walimu na madarasa; mambo haya yote yamekuwa yakifanya watumishi wengi kutokupendelea kwenda kufanya kazi maeneo hayo. Hivyo ni eneo lenye uwiano wa walimu usiolingana na maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mchango huu, tunaomba kupata walimu zaidi hasa katika shule za maeneo haya, sekondari na msingi pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vipo vijiji visivyofikika kwa gari, mfano, Kijiji cha Kasanga - Kata ya Ninde; Kijiji cha Msamba - Kata ya Ninde; Kijiji cha Izinga - Kata ya Wampembe na Kijiji cha Mwinza - Kata ya Wampembe. Vijiji hivi pamoja na vingine hulazimika kwenda kufanya mitihani ya darasa la saba katika shule nyingine kwa sababu wasimamizi hawako tayari kwa usafiri wa majini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali itafute ufumbuzi ikiwa ni pamoja na kusidia wananchi katika jitihada zao za kilimo na kufungua barabara za maeneo ya wananchi hawa. Tusikubali jambo hili liendelee siku zote, tutafute suluhu kwani itawezekana pia watoto wanaosafirishwa majini mara kwa mara wakapata shida japo hatuombei jambo hilo; tahadhari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanafunzi wamekuwa wakisafirishwa kwa makundi makubwa/idadi kubwa kwenda kufanya mitihani maeneo yanayoruhusiwa au basi, shule zote zipate fursa ya kufanya mitihani kwa kupata vyombo vya usafiri kwa usimamizi ili shule zote ziweze kufikika wakati wa mitihani, watoto wafanye mitihani kwa utulivu shuleni kwao walikozoea.

Maeneo ya pembezoni kama Jimbo langu naomba yapewe upendeleo kwa nyumba za walimu na madarasa ili kuwakomboa wananchi hawa ambao wanatakiwa kushikwa mkono ili wasogee. Watoto yatima waruhusiwe kusomeshwa kama watakuwa wamefaulu vizuri, maana wengi wao wamekuwa wakirudi nyumbani kwa kukosa msaada zaidi au vinginevyo ianzishwe taasisi itakayoiangalia changamoto hii kwa umahiri mkubwa (yatima kusoma).

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nashukuru kupokea shilingi 259,000,000 Kasu sekondari ili kuendeleza miundombinu ya shule mpya kufuatia kufutwa kwa Mihudikwa sekondari na watoto kuhamishiwa Kasu.

Tunaomba Chuo cha Chala kiboreshwe kiwe VETA kamili ili wananchi wa Nkasi wapate ujuzi hasa wale wanaofuzu darasa la saba na sekondari pia. Ahsante.