Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa

Hon. Rhoda Edward Kunchela

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Katavi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa

MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nilitaka nichangie machache kuhusiana na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Kwanza nataka niunge hoja asilimia 100 hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani kutokana na hotuba hii kuonesha mwelekeo wa namna gani Wizara inaweza kutatua kero ambazo zinalikabili Jeshi letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia suala la usalama wa nchi kama wapinzani lakini pia kama Watanzania ambao tuna haki ya kuzungumza na kuikosoa Serikali hatuna maana mbaya, tunathamini kabisa michango ya Jeshi, tunaelewa kabisa kazi ambazo zinafanywa na Jeshi letu, kwa hiyo, si kwamba tunapinga kila kitu. Tunachotaka ni kuikosoa Serikali katika yale mapungufu ambayo tunaona kabisa kupitia Jeshi hili basi linaweza likafanya marekebisho katika baadhi ya sehemu ili tukaenda sawa na wananchi wakawa na amani hiyo ambayo mnaisema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nataka nizungumzie kidogo kuhusiana na migogoro ya ardhi kati ya wananchi na Jeshi. Kumekuwa na changamoto kubwa kwenye maeneo mengi ya Jeshi ambayo sasa wananchi wamekuwa wanayalalamikia, kwamba Jeshi limeingilia kwenye makazi ya watu, lakini unakuta tena Jeshi hilo hilo linasema wananachi wamevamia maeneo ya Jeshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunaiomba Serikali na Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha aeleze ni mkakati gani ambao sasa Wizara au Serikali hii imepanga ili kutatua migogoro hii ya ardhi ambayo imesababishwa na Jeshi, aidha, wananchi kuvamia maeneo ya Jeshi au Jeshi kuvamia maeneo ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nilitaka niseme kidogo, katika Mkoa wangu wa Katavi kuna kata ya Misunkumilo pamoja na Kata ya Mpanda Hoteli. Katika maeneo haya kuna wananchi wako pale wamejenga wana miaka zaidi ya 60 mpaka leo. Vilevile kuna viwanda pale na pia kuna wananchi wana mashamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii wamezuiliwa kuendelea kufanya shughuli za kiuchumi kwenye maeneo yale, wameshindwa kulima, wananchi wanakufa na njaa katika kata zile. Eneo lile lina mgogoro lakini Serikali mpaka sasa haijawahi kusema ni lini sasa mgogoro huu utakwisha ili hawa wananchi sasa waache kupigwa, waache kunyanyaswa na Serikali ambayo mnasema ni Serikali ya amani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la malipo ya wanajeshi. Hivi tunavyoongea kuna wanajeshi zaidi ya 250 ambao wamehamishwa kutoka Makao Makuu kuja Dodoma hapa katika Mji wa Dodoma, hawajalipwa na wengine wako humu ndani. Serikali ina mkakati gani wa kuwalipa hawa wanajeshi? Mmewahamisha, mmewaleta hapa watu wameacha familia zao. Tunaomba sasa katika bajeti hii itengwe fedha kwa ajili ya kuwalipa hawa wanajeshi, wanateseka na familia zao zinateseka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niongelee pia suala la mwisho linalohusu utawala bora. Tunathamini kabisa kazi zinazofanywa na Jeshi, lakini tunaomba hawa wanajeshi bajeti hii sasa ilenge maana ya kuwajengea nyumba ili watoke katika makazi ya watu, maana imekuwa ni kero; wananchi wanakuwa wanaogopa, lakini na Jeshi nalo zile kambi zake zinashindwa kufanya yale majukumu kama Jeshi kwenye maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na migogoro mingi. Ni kweli, wanajeshi wana haki kabisa endapo mwananchi anakuwa amekosea, lakini kero nyingine inapokuja kuna makosa madogo madogo, unakuta mwananchi amemuudhi huyu mwanajeshi basi hicho kipigo atakachokipata, wengine ni vilema. Ukiangalia katika fukwe zetu unakuta mwanajeshi anamlazimisha mwananchi kula samaki mbichi, leo hii tumefikia hapa! Wananchi wetu wanateseka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaliomba Jeshi, ni kweli wananchi wanakosea, sasa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.