Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Welezo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SAADA SALUM MKUYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mimi pia nachukua fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa ambayo anaifanya. Nadhani hatuna budi vile ile kulipongeza Jeshi letu la Wananchi wa Tanzania, hususan kwa upande wetu wa Zanzibar nadhani limejitahidi sana kurejesha discipline ambayo ilikuwa imeanza kutetereka, kwa hivyo tunalipongeza sana Jeshi letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja atueleze, kuna hospitali abazo zinaendeshwa na Jeshi. Ni Hospitali za Kijeshi ambazo wananchi wamekuwa na confidence nazo kwa kiasi kikubwa. Mwananchi ukimwambia aende katika hospitali ya kawaida na Hospitali ya Jeshi anakwenda katika Hospitali ya Jeshi kutokana na confidence kubwa aliyokuwanayo juu ya utendaji wa wanajeshi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hospitali hizi ziko katika hali mbaya sana, dawa hakuna, hakuna vifaa, lakini hata wale madaktari ambao si wanajeshi ambao wanapangiwa katika vituo vile wanakuwa hawakai kutokana na mazingira duni ambayo yapo katika vituo vile. Sasa tunaomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha atuambie ni mkakati gani hasa umewekwa kuhakikisha kwamba hivi vituo ambavyo vinatoa huduma kwa wananchi vinaimarishwa ili viwe na ufanisi zaidi kwa watendaji lakini vilevile kwa vifaa na dawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inafika hadi kwa mwezi vituo kama vile vinapata OC ya shilingi 100,000, haviwezi kuendesheka kwa namna kama ile. Jimboni kwangu kipo kituo cha namna hiyo, inafika hadi hata panadol ya kuwapa wale wananchi wanaowatibu hawana. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nadhani hili lichukuliwe special consideration na utuambie mkakati ambao unatarajia kufanya katika bajeti hii ya mwaka 2017/2018. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia kuhusiana na wanajeshi wastaafu. Wanajeshi wetu wastaafu Mheshimiwa Waziri wanahangaika sana kufuata mafao yao. Once wanapostaafu tu ile connection baina yao na yule aliyekuwa mwajiri wao inakatika. Kwa hiyo, anapostaafu huyu
mwanajeshi, na hii ni kwa sababu ya experience ninayo, anakuwa hana msaada wowote zaidi ya kuanza kuhangaika kwenda kurudi, kwenda Hazina kudai mafao yao. Pengine wale ambao walikuwa wakihangaika katika kudai mafao yao kwa muda mrefu huenda taarifa zao zimepotea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kule jimboni kwangu kuna mwanajeshi amestaafu muda mrefu, ni mtu mzima, amenipa namba yake ya file nimekwenda Hazina, namba ya file ndio, lakini jina silo kabisa. Hii inaashiria kwamba, wale wanajeshi wetu wakistaafu inakuwa ile connection hata zile taarifa zao zinakuwa hazipo, zinapotea, hakuna mtu wa kuwafuatilia. Kwa hiyo, tunaomba sana Mheshimiwa Waziri hawa wanajeshi wetu kuwe kuna mkakati maalum wa kutunza taarifa zao wakati ambapo wapo kwenye ajira, lakini wanapostaafu lazima kuwe kuna usaidizi kutoka katika taasisi zao walizokuwa ili wasiende kule kupata taabu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa ni watu ambao wamefanya kazi nzuri kwa Taifa hili, ni watu ambao wameweza kulinda mali pamoja na roho za raia kwa kipindi kirefu na katika wakati mgumu. Haiwi vyema na haiwi busara kuona kwamba wakistaafu ndiyo sasa waanze wao wenyewe kuhangaika, waende Hazina, wapande ngazi warudi; na mara nyingine, hususan familia zile zinazoathirika. Wakati mwingine mwanajeshi anakuwa amefariki na familia ile kuanza kufuatilia mafao ya marehemu inakuwa ni kazi kubwa sana, wanakuwa hawapati usaidizi wowote kutoka katika jeshi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, kama walivyosema wengi kwamba sasa hivi kumekuwa kuna mchanganyiko baina ya makazi ya raia na Kambi zetu za Jeshi. Tunapata taabu sana sisi ambao tuna majimbo na tukiwa tunataka kukarabati miundombinu ambayo raia wao wenyewe pia wanatumia, lakini zimepita katika maeneo ya Jeshi, tunapata tabu sana. Sasa Mheshimiwa Waziri tunaomba hili nalo liangaliwe vizuri, jinsi gani sasa kama tukitaka kukarabati miundombinu katika sehemu ambazo Kambi za Jeshi zinapita lakini na raia wanatumia, tunafanya nini? Kwa sababu hii imekuwa ni changamoto kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la mwisho ni kuhusiana na mafunzo haya ya JKT. Upande wetu kule Zanzibar hizi nafasi zinakuja…
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.