Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa

Hon. Martha Moses Mlata

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa

MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatambua umuhimu wa Wizara hii na kazi kubwa sana na nzuri inayofanyika. Aidha, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa namna anavyoongoza Wizara hii kwa hekima na utulivu mkubwa . Pamoja na pongezi hizi naomba nimpongeze pia Jenerali Venance Salvatory Mabeyo kwa heshima kubwa aliyopewa na Mheshimiwa Rais, kwa kumteua kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, hongera sana. Kwa imani kubwa aliyonayo Rais wetu kwake ndivyo na sisi Watanzania tuna imani sana na yeye. Tunaamini ataendelea kushirikiana na viongozi wote walio chini yake na walio juu yake ili kuendelea kuwa na utulivu na amani tuliyo nayo nchini pamoja na usalama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizi pia niwapongeze wanajeshi wote kwa kazi nzuri ya kulinda mipaka ya nchi yetu, hakika tunawapongeza kwani tunatambua kazi kubwa waliyonayo. Wakati wengine tunaendelea na shughuli zetu wao wakiwa katika shughuli nzito ya kutulinda wakati wengine tukiwa tumelala, wao wakiwa macho kutulinda. Hakika tunawashukuru sana. Tuna imani na Jeshi letu, Mungu awabariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizi naomba nitoe maoni yangu kwa ufupi kama ifuatavyo:-

Kwa kuwa hapa Tanzania vijana walioko sekondari na hasa wanaohitimu kidato cha nne, mitihani yao huwa inafanyika mwishoni mwa mwezi wa kumi kila mwaka. Hivyo watoto hawa wanaotajarajia kuendelea na masomo ya kidato cha tano husubiri kwa takribani miezi minane na zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo hali hiyo huwa ni kipindi cha mpito mgumu sana kwa wazazi na hata watoto pia kwani mazingira yanaweza kumuathiri mtoto na kujikuta anabadili nia yake ya kuendelea na masomo yake ya kidato cha tano ama wengine kuangukia kwenye tabia za ama kupata mimba au dawa za kulevya au ulevi na tabia nyingine zitakazokwamisha ndoto yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo kutokana na hali hiyo, naomba nishauri kuwa watoto hawa wanaomaliza kidato cha nne, mara baada ya matokeo yao ya mitihani Wizara iandae namna ya kuwachukua watoto hawa kujiunga na JKT kwa miezi kati ya sita na mitatu ili wasipoteze muda bure na pia kutunza uadilifu na nia yao njema ya kuendelea na shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Jeshi la Kujenga Taifa ya mwaka 1964 (na marekebisho yake) kifungu cha 5(2) kinatoa nafasi kwa kijana mwenye umri wa miaka 16 kujiunga na Jeshi hilo; hivyo haitakuwa tatizo kuwachukua wanafunzi hawa. Kwa sheria hiyo Wizara iongee/ishirikiane na Wizara ya Elimu ili kubadili mfumo wa kuwapeleka JKT vijana wanaomaliza kidato cha sita badala yake tunaanza na wanaosubiri kwenda kidato cha tano kwani hawa wana muda wa kutosha sana kuliko wa kidato cha sita wanaosubiri kwenda vyuo vikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, vijana watakaofaulu kuanzia division one hadi division three ndio waweze kupata nafasi ya kujiunga na JKT. Pia itaweza kurahisisha kuwapata wanaotaka kujiunga na Majeshi yetu kama Polisi, Magereza, Uhamiaji, Jeshi la Wananchi na kadhalika kuliko utaratibu wa sasa unaotumika kuwasaka mitaani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho najua jambo hili linaweza kuonekana ni gumu sana, lakini ninaona manufaa yake ni makubwa zaidi, kwani tunaokoa Taifa letu na nguvu kazi pamoja na wasomi na tunapata waadilifu zaidi kwani watoto hawasahau.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa naunga mkono hoja asilimia mia moja.