Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Hamadi Salim Maalim

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Kojani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. HAMAD SALIM MAALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala kwa kutujalia asubuhi hii tukaamka tukiwa wazima. Pia nikishukuru chama changu kwa kunipa nafasi hii na kuniamini kwamba nitaweza kuwawakilisha vizuri katika Bunge hili al Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya shukrani hizo, naomba nianze mchango wangu moja kwa moja katika suala zima la elimu. Tunaelewa fika kwamba elimu ndiyo msingi wa maendeleo ya mwanadamu na elimu ndiyo kioo cha maisha ya mwanadamu. Ndani ya Tanzania yetu niseme kwamba kuna sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ni Zanzibar ambapo ni mdau mkubwa katika elimu ya juu Tanzania. Pia katika sekondari ya kati ambapo tunakuwa na kidato cha tatu na kidato cha nne Zanzibar pia ni mdau katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo kubwa ambalo linatukumba Zanzibar katika suala zima la sekondari ya kati ni kwamba mara nyingi inapotokea mabadiliko ya mitaala huwa yanatuathiri sana Tanzania Zanzibar kiasi kwamba wanafunzi wetu inafika kufanya mtihani wakati mwingine hatujapata yale mabadiliko yaliyotokea. Wakati mwingine mabadiliko yanatokea wenzetu wanaanza kuyafanyia kazi kutoka Januari sisi tunayapa kuanzia mwezi wa nane. Inaonekana kwamba hapa kuna daraja kubwa sana baina ya Tanzania Bara na Tanzania Visiwani katika suala hili la elimu katika sekondari ya kati.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naishauri Wizara husika kwamba katika kufanya mabadiliko haya ni vyema wadau wenzao wa Tanzania Zanzibar wawashirikishe vizuri ili kuondoa hili daraja lililopo baina ya pande mbili kwani kufanikiwa kwa vijana wetu katika suala zima la elimu ndio kufanikiwa kwa Taifa letu. Hatutegemei kwamba vijana wetu tuwaone wanafeli kila baada ya mitihani. Hii inatuathiri sana walimu ambao tunajitayarisha kwa kiasi kikubwa sana lakini ikafikia mahali tukakuta matokeo ya wanafunzi wetu yanakuwa ni mabaya kutokana na dosari ndogo ndogo kama hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naenda kipengele cha pili cha TASAF. Niipongeze Wizara husika ya Utumishi na Utawala Bora katika suala zima la Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF). Wamejitahidi sana katika suala la kusaidia kaya maskini. Tumeona katika maeneo mengi tuliyopita nadhani hata katika ziara yetu ya Kigoma. Hata hivyo, kuna dosari ambazo zimetokea kwamba mbali ya kusaidia kaya maskini tumekuta kuna vijana wadogo ambao wanamudu kufanya kazi ndiyo wameingizwa katika mfuko huu wa kusaidia kaya maskini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tulipofika pale Kigoma tulimkuta mama mmoja wa miaka karibu 120 hakuingizwa katika mfuko wa kaya maskini lakini kuna vijana wa miaka 25 wameingizwa. Imani ilitujia Wabunge kama watano tukamchangia yule mama shilingi 50,000/=. Kwa kweli naomba suala hili liangaliwe vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kupitia Mfuko huu wa Maendeleo wa TASAF mbali ya kuhudumia kaya masikini unatengeneza barabara. Naomba mfuko wa TASAF uangalie kwamba kule Pemba kuna barabara mbili ambazo zinazozalisha sana. Katika kipindi cha mvua kama hiki barabara zile huwa hazipitiki hata kidogo. Barabara hiyo ni ya Mgelema na barabara ya Mjini Kiuyu. Kwa hivyo kwa kuangalia imani yao Mfuko wa TASAF, naomba kwa kutumia njia hii ya kaya maskini basi barabara zile wazipatie msaada wa kuzitengeneza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipengele cha tatu ni suala zima la vyombo vya habari. Na mimi pia naomba nigusie suala la vyombo vya habari kwamba wenzetu wanaonyesha wanaongopa. Jamani Serikali ya CCM msiogope. Ukiwa na mtoto nyumbani ikiwa siku zote unampiga yule mtoto unamchonga ukali. Itafikia mahali itakuwa baba hakuogopi tena na mama hakuogopi. (Makofi)
Mheshimwia Naibu Spika, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 18(d) inaeleza kwamba haki ya kupata taarifa ni haki ya kila mtu tena kila wakati siyo saa nne za usiku mpaka saa tano za usiku. Hivi jamani Bunge la Jamhuri ya Muugano wa Tanzania linaendesha mijadala kwa saa saba kila siku kuanzia saa nne mpaka saa saba na kuanzia saa kumi mpaka saa mbili za usiku. Tunachukua kipindi cha saa moja tunakionyesha kwenye vyombo vya habari, uhalali uko wapi? Hivi kweli watu wetu watapata zile taarifa ambazo wanazitegemea kuzipata kutoka kwetu? (Makofi)
Mheshimwia Naibu Spika, naomba CCM msiogope acheni vyombo vya habari binafsi kama ninyi mmenyima chombo chenu cha habari, viingie Bungeni, vichukue taarifa, vipeleke kwa jamii. Naomba mfanye tathmini ndani ya Dodoma muangalie je, hata hao wana-CCM wenzenu kwa ninyi kuzuia vyombo vya habari wanawaunga mkono kwa suala hili? Nina imani kwamba kama kuna watu 100 basi 60% watakuwa hawaungi mkono suala hili. Wana-CCM msiogope jamani viacheni vyombo vya habari vifanye kazi vizuri na watu wote waweze kupata taarifa kwa wakati unaostahiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya suala hilo, naomba niende kwenye suala zima la madaraka na mamlaka kwa Serikali za Mitaa. Dhana ya Serikali za Mitaa ni pana na hii inapatikana kutokana na ushiriki mkubwa wa wananchi yaani wananchi wenyewe kushirikishwa vizuri ndiyo inapatikana ile dhana ya Serikali za Mitaa. Leo tuone Meya, Naibu Meya, Wenyeviti wa Vijiji wanaonekana hawana hadhi ndani ya Serikali za Mitaa wenye hadhi ni Wakurugenzi, Makatibu Tawala na Wakuu wa Wilaya. Hivi kweli jamani ile dhana ya kwamba wananchi ndiyo wanaotoa mamlaka kwa Serikali iko wapi? (Makofi)
Mheshimwia Naibu Spika, naomba Waziri husika kama kuna kubadilisha sheria basi wabadilishe, Wakurugenzi, Makatibu Tawala na viongozi wengine wa Halmashauri wachaguliwe kwa kura kama ambavyo anachaguliwa Meya, Naibu Meya na Wenyeviti ili kutoa mamlaka zaidi kwa viongozi hawa. Tukifanya hivi, ule utata wa kwa nini Meya, Naibu Meya, na Wenyeviti hawana ile hadhi utaondoka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata jana kuna Mbunge mmoja wa CCM alisema hapa kwamba wao wanaonekana kwenye Serikali za Mitaa si chochote si lolote. Watu wanapitisha bajeti zao, wanajenga majengo, wao wanakuja kuambiwa tu kwamba kuna jengo limejengwa kwa shilingi milioni 90 pengine jengo lile ni shilingi milioni 45. Hii inaonyesha kudhalauriwa kwamba hata kudhalauriwa Wabunge wetu waliomo kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano hawana hadhi kwenye Serikali za Mitaa. Jamani naomba Serikali iwe wazi katika suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ni suala zima la mipango mibovu ya Wizara za Ofisi ya Rais. Nadhani katika ziara zetu tulizopita tulipitia taasisi mbalimbali zilizoko chini ya Ofisi ya Rais, Utawala Bora. Kitu cha kusikitisha tulikuta kuna taasisi moja imepangisha jengo kwa mwezi wanalipa shilingi 80,000,000, kuna taasisi nyingine mbili zinalipa shilingi 40,000,000, hivi tuangalie kwa mwezi mmoja taasisi hizi zinalipa shilingi 120,000,000 kwa mwaka wanalipa shilingi 144,000,000,000.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha
muda wa mzungumzaji)
MHE. HAMAD SALIM MAALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba nikae.