Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Sebastian Simon Kapufi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpanda Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi kwa kuchangia naomba nianze na maneno yafuatayo; mtu mmoja aliwahi kusema hivi; “hata nikifa nisije nikatafutwa makaburini, nikasomeke kwa kazi nilizozifanya wakati wa uhai wangu na wale niliowatendea.” (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tafsiri yangu ni nini? Hapa tulipo katika jengo hili Tukufu watu wetu kule katika Majimbo yetu, kama kuna mambo mazuri tunayoendelea kuwatendea, umeonekana kwenye tv (television), haujaonekana lakini utasomeka kwenye nyoyo zao na yale uliowatendea. Ndiyo maana leo hii Baba wa Taifa ana muda mrefu amefariki, wengine hata kaburi lake hatujaliona kule Musoma lakini kwa uzalendo aliokuwa nao wa kulijengea Taifa hili amani na utulivu anaendelea kusomeka kwenye nyoyo za Watanzania. Mimi hilo ndilo ninaloliomba, nikasomeke kwenye nyoyo za watu wangu katika Jimbo langu.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la kilimo. Nafarijika kuna fedha za kilimo hapa nimeona hapa na kwa maana ya mkoa wangu wa Katavi kuna takribani shilingi milioni 46 lakini nataka kusema nini? Pamoja na fedha hiyo, kama mnavyofahamu Mkoa wa Katavi ni mzuri, unazalisha kwa kiwango cha hali ya juu, lakini maajabu ni kwamba kwa fedha hizi walizotengewa ni ndogo ukilinganisha na fedha za maeneo mengine. Leo nikiwaambieni kwa maana ya ziada Mkoa ule una zaidi ya tani 345,283 za mazao ya chakula. Kwa hiyo, tutakapokuwa tukitenga fedha hizi naombeni muangalie maeneo kama haya yenye uzalishaji mkubwa. Kuna maeneo ambayo leo hii watu wanazungumzia habari ya njaa, watu wana ukosefu wa chakula, sisi ambao tuna ziada angalia na fedha tuliyotengewa. Naomba hapo mpaangalie kwa umakini.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo napenda kuzungumzia ni eneo la madeni. Ni kweli watu mbalimbali wanaozidai Halmashauri zetu wasipolipwa inawafifisha Moyo. Nilikuwa naendelea kuomba watu hao waendelee kufikiriwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni maeneo mapya ya utawala. Mkoa wangu ni kati ya mikoa mipya lakini leo hii hatuna jengo kwa maana jengo la mkoa. Ndugu zetu wa polisi wanafanya shughuli zao kwenye jengo ambalo lilikuwa ni la wilaya. Kwa misingi hiyo maana yake wanawazuia wenzetu ambao ni wa Polisi Wilaya kufanya shughuli zao kwa sababu wao hawana jengo. Naomba please watu hawa wa Polisi Mkoa waendelee kufikiriwa kwa maana wawe na jengo lao lakini vilevile kwa maana ya jengo la Mkuu wa Mkoa ili kuweza kupisha kwa sababu wanafanya kazi kwenye jengo ambalo ni la Manispaa ya Wilaya ya Mpanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoke hapo nije kwenye suala la ukusanyaji mapato. Pamoja na kusisitiza matumizi ya vifaa vya kielektroniki, lakini niendelee kusema kuwa tunapokuwa hatufanyi utafiti wa kutosha kuhusu vyanzo vya mapato inapelekea mapato mengi kupotea. Naomba tuendelee kufanya utafiti ili hata pale tunapokusanya tuwe na uhakika ni kitu gani tunachokusanya, hilo ni la muhimu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nirudi kwenye hospitali yetu. Naendelea kuiomba sana Serikali hii kwa maana ya shilingi bilioni 27 ambazo ni makadirio ya ujenzi wa Hospitali hiyo ya Mkoa, kwa utoaji huu wa shilingi bilioni moja moja kwa mwaka, itatuchukua miaka 27 kuweza kumaliza hospitali ile. Naomba namna yoyote iweze kufanyika kuhakikisha tunapata fedha na hospitali ile ijengwe kwa wakati. Nalisema hilo kwa makusudi, jamani mtu kutoka Katavi aende Dar es Salaam, mtu kutoka Katavi aende Mbeya tutaendelea kupoteza watu wetu, kule ni mbali lakini ukombozi pekee ni kwa kuwepo kwa Hospitali ya Mkoa katika maeneo yale.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mfuko wa Jimbo. Kwa maana ya Mfuko wa Jimbo fedha ambayo Mbunge aliyetangulia alikuwa anapewa alikuwa na kata tisa leo hii Jimbo lile limeongezeka kuna kata 15 lakini bado fedha inayotolewa ni ile ile. Naomba suala hili nalo liendelee kufanyiwa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la TASAF, suala hili ni jema, watu wetu wanaendelea kuwezeshwa na mimi nimeliona. Kuna kipindi niliwahi kwenda kutembea Makambako nilikuta kuna mkopo mpaka wa siku moja kwa maana mama anakopeshwa fedha ya kununua jogoo kwa siku moja, akipata fedha ile jamani mama yule kwa maana amekopeshwa shilingi elfu kumi…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Sebastian Kapufi, muda wako umekwisha na tunaendelea.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja.