Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Njalu Daudi Silanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Itilima

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Wizara hii muhimu ya wakulima na mimi nikiwa kama mkulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kuipongeza Serikali, nimpongeze Mheshimiwa Waziri na wataalam, kazi yao inaonekana. Kwa miaka miwili tumeona bei za mazao yetu zikiongezeka. Pamoja na hilo, ziko changamoto ambazo tunahitaji wazitatue kama Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia suala la tozo kwenye mazao yetu, zile tozo zinazopunguzwa moja kwa moja zinaongeza thamani ya bei ya mkulima. Nimepata tabu kidogo Waheshimiwa Wabunge wanasema inamsaidiaje mkulima. Ni suala la kujiuliza kwa sababu mfanyabiashara siku zote yeye hapati hasara, gharama zote anampelekea mkulima. Kwa hiyo, tunapojaribu kuchangia kwenye suala la kilimo tuwe makini sana pale tunapoishauri Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana unakuta kwenye zao la pamba kuna VAT na asilimia 70 ya wakulima wanaotarajiwa kuwezesha viwanda na vitu vingine wanatokana na kilimo. Sasa utaona asilimia 70 hii ya wakulima wote wanapelekewa VAT na akipelekewa VAT automatically ile VAT itakwenda kumpunguzia mkulima, kwa hiyo, utaona bei zinakuwa chini. Ndiyo maana unakuta mazao mengi wakulima wanakuwa wanayakimbiakimbia kuyatekeleza, wanaibua wao wakulima wenyewe kwa maarifa yao lakini yakishaibuliwa inakuja kodi mbele yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana Serikali mambo haya ya msingi tuyaangalie, huwezi kuweka VAT kwenye pamba. Mashudu kwani mfanyabiashara mdogo yule ambaye angenunua yale mashudu kwa ajili ya vifaranga vya kuku na vitu vingine vingeendelea kufanyika umeshamwekea kodi hataweza kununua na hivyo bei ya pamba haitapanda katika maeneo yale. Kwa hiyo, utakuta bei zinaendelea kushuka kwa sababu hatuwezi ku-control masoko haya tunatarajia kutoka nchi za nje. Kwa hiyo, naomba suala hili la mazao hususani zao la pamba mwangalie sana kodi hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kusema ametoa kodi kwenye pamba, Mwenge sio kodi, ni makubaliano kati ya DC na ginneries husika. Suala la msingi hapa ni kwamba toeni VAT kwenye suala hili ili bei za wakulima ziendelee kuongezeka na zikitolewa tutapata fedha nyingi za kigeni lakini tutapata ajira nyingi na viwanda vitaendelea kufanya kazi katika eneo letu hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la mbegu. Kwenye suala hili la mbegu watafiti wetu wanaendelea kutafiti vizuri tu kwa muda mrefu lakini ukijiuliza, mfano, nataka nizungumzie suala la pamba, kuna mbegu ya UK91 imeshapitwa na wakati. Ndiyo maana siku zingine Wabunge tunauliza kwa nini mbegu hazijaota, hii ni kwa sababu zimeshapitwa na wakati na watafiti na wataalam wanalifahamu hili hata mfumo wa kuzipitisha hakuna, zinakuwepo tu ili mradi lakini GOT yake ni kidogo asilimia 32 inayosababisha hata bei zenyewe za pamba zisipande. Kuna hii UK08 ikisimamiwa vizuri, ikizalishwa vizuri katika maeneo husika tuna uhakika tutazalisha GOT asilimia 40 ambayo itakuwa ni average kubwa sana na tutapata fedha nyingi za kigeni katika maeneo yetu haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Mifuko ambayo ilianzishwa ya CDTF ilikuwa na wadau watatu, Serikali, wakulima pamoja na wafanyabiashara wenye mfuko husika. Kwa muda mrefu sana fedha hii imekuwa ikitumika nje ya utaratibu badala ya kumnufaisha mkulima anakuwa anafanya double payment, amechangia kwa mwaka huu na mwaka unaokuja anaambiwa kuchangia halafu mwisho wa siku hapati pembejeo. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri kwa mwaka huu ambao tunaumalizia maeneo mengi yameathirika sana kwa sababu ya pembejeo hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile mfumo huu ulivyoanzishwa kulitengenezwa kitu kinaitwa pass book kwamba mkulima alikuwa anaweka benki yake, benki hii akienda kuchukua dawa ina maana apewe bure lakini matokeo yake mkulima huyu amekuwa akitozwa. Nimwombe Mheshimiwa Waziri hii pembejeo ya mwaka huu awatangazie wakulima na wananchi wa Tanzania nzima hususan mikoa inayolima pamba kwa sababu ni pesa zao walizozichanga, hakuna sababu ya mtu anakuja anasema anafanya kilimo cha mkataba na kilimo cha mkataba hiki tayari pembejeo zile alishachangia mwananchi. Kwa hiyo, hizo anatakiwa apewe bure ili aweze kujiendesha kwa msimu unaokuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niombe kwenye suala zima linalohusiana na suala la kilimo cha mkataba tungetafuta jina lingine, sio kilimo mkataba. Hii ni kwa sababu unaposema mkataba unapomaliza mkulima atakwambia nataka niuze bei hii na sisi hatupangi bei, tunategemea mataifa makubwa yanavyopanga bei ndiyo tunashusha gharama zetu na kadhalika ndiyo tunapata bei sahihi. Kwa hiyo, naomba litafutwe jina lingine, dhana ni nzuri ambayo itaweza kuboresha na kuleta tija kubwa katika uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona ukurasa wa 34 wamesema wastani wa uzalishaji umeongezeka kutoka 728 kwa hekta kwenda 925. Napata tabu kwa sababu mwaka jana takwimu walizotuletea walisema kwamba takribani hekari milioni moja za pamba zimelimwa. Kwa takwimu hii ukiizidisha tungepata milioni 328, matokeo yake kwa mwaka jana tumepata milioni 120 tu. Kwa hiyo, utaona hizi takwimu ni za kukaa na kujifungia na kubumba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana suala hili hasa la utafiti litiliwe mkazo na waangalie ni jinsi gani itakayoweza kusaidia. Haya mambo tunayazungumza sana, wakulima wanayazungumza lakini tuna tatizo la wataalam kwa maana ya Maafisa Kilimo, hatujui wanawajibika kwa nani, nalo hili ni tatizo kubwa. Kwa hiyo, tunamwomba Waziri aweze kukaa na kujua mamlaka haya husika, huyu mtu anawajibika wapi, bodi yupo peke yake, atazunguka na pikipiki yake katika Wilaya nzima lakini pale kwenye Serikali kwa maana ya TAMISEMI kuna Afisa Ugani kila Kijiji, Kata na kila maeneo lakini hawa watu hawawajibiki, wanawajibika kwa nani? Mwisho wa siku inapotokea sasa Halmashauri imetengeneza mapato ndiyo watu wa kwanza kuingia kwenda kutoza kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili ni tatizo na lazima tuliangalie kwa mapana Waheshimiwa Wabunge tujaribu kusaidia kwamba mifuko yetu hii na bodi zinazoundwa hizi ziweze kufanya kazi yake vizuri lakini ziweze kuisaidia Serikali. Waziri kwenye suala zima la Bodi ya Pamba sasa hivi ni mwaka wa tatu Bodi ya Pamba haina Board Members wake ndiyo maana tunakosa mambo mengi maeneo yetu kwa sababu hakuna ushauri. Mnakutana na wataalam wale wale mkirudi hakuna jambo jipya litakaloendelea kupatikanika katika maeneo yetu. Naomba hilo nalo Mheshimiwa Waziri ajaribu kuliangalia, hii bodi itatengenezwa lini na vitu gani vifanyike ili mambo yaende vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, nimpongeze Mkurugenzi Mtunga na Waziri kwa sababu mmeendelea kutengeneza mfumo mzuri wa bei. Nina imani na mwaka huu bei zetu zinaweza zikawa nzuri. Ombi kubwa kwa Serikali toeni hizi kodi na wananchi watajiendesha wao wenyewe. Haya mambo tunazungumza, leo tuna asilimia tatu tu ya kilimo lakini mwananchi huyu anaendelea tu kuhangaika kule lakini bado hatujataka kumsaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba sana hasa kwenye suala zima la mbegu tunajua kule Simiyu, wameanzisha na Meatu ni jambo jema na maeneo mengine tujipange kuhakikisha tunaweka utaratibu mzuri. Vilevile wako wakulima wazuri tu ambao wanaweza wakafanya
kazi hiyo kwa kuwaelimisha wengine. Nashauri angalau kila kijiji kuwe na wakulima wawili ambao watakuwa ni sehemu ya mfano, watu watafanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka kwenye suala la la mbegu za mahindi wakati zinakuja watu walikuwa wanalalamika lakini sasa baada ya kuona uzuri wa mbegu zinavyozalisha watu wanaenda kununua wenyewe tofauti na kutumia nguvu kubwa na fedha nyingi. Nina imani wakulima wa kanda zetu kule wakishajua jambo wao wenyewe hujiongoza. Unaweza ukasema wakati mwingine hata kilimo wanaweza wakawa wanakwamisha, wanawapa matumaini makubwa, matokeo yake hata mbegu hawaleti. Kwa hiyo, tufike mahali tusiwe tunatoa matumaini kwa wananchi wetu ambapo wanatarajia kwamba kuna kitu fulani kinakuja, pembejeo inakuja mwezi wa Nne au wa Tano kitu ambacho inakuwa muda wake umeshaisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, nashukuru sana, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.