Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Zaidi kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai na sote tuko hapa tunazungumzia maendeleo ya nchi yetu. Sina budi pia kumpongeza Waziri wa Wizara hii, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote kwa hotuba nzuri waliyotupatia. Shukurani zangu ziende kwa Mheshimiwa Rais kwa kuondoa tozo mbalimbali ambazo zilikuwa ni kero kwa wananchi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kilimo kuna mambo manne ambayo ni muhimu, ardhi, unyevu, pembejeo na pia inabidi sasa nguvu kazi iwepo na nguvu kazi ni sisi. Nguvu kazi hiyo ipo katika matabaka mengi lakini nitazungumzia lile la chini ambalo ni wakulima wadogo wadogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wadogo wadogo nchi hii wanajitahidi sana sana na wengi hapa ni watoto wa wakulima. Tumeona na tumekuwa kwenye kilimo lakini kuna kero ambayo haijawahi kupata ufumbuzi, ni kero ya masoko ya bidhaa zao na nitatoa mfano wa zao moja tu zao la mahindi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu analima mahindi yake ili auze apate hela akafanye shughuli ambayo anataka yeye kulipa ada au kujenga nyumba na mengineyo, lakini siyo wakati wote ndiyo anataka hayo mahindi yafikie mpaka yakomae yakauke. Kwa mfano, mtu anategemea mvua mbili ikimpendeza Mungu, kuna vuli na masika. Wakati wa vuli anaweza akalima mahindi akaamua kuuza mahindi mabichi na mahindi mabichi haya ni mazuri. Katika hekari moja yanapatikana mahindi mabichi kama 45,000 mahindi haya akiuza hindi moja moja Sh.100 anapata Sh.4,500,000 lakini akilingoja hindi hili likakauka akaja kuuza anaweza akapata magunia 15 na labda akawa tu amepata Sh.700,500. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lililo hapa ni jinsi gani mtu huyu anakereka anapozuiwa kuuza mahindi mabichi. Wengi wenu hapa Waheshimiwa ni wateja au ni watu ambao wanafurahia mahindi wakati wanaelekea Dar es Salaam pale Dumila, Morogoro. Naiomba hii Wizara iwaache wakulima wauze mahindi yao pale ambapo wako tayari. Kwa nini nasema hivi? Wanaambiwa wasiuze, wanawekewa doria na mageti mengi sana halafu unamnyima nguvu kwa sababu yeye anafanya kazi ili aweze kupata kwa haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka hapo kwenye masoko baada ya ombi hilo ambalo najua watalifikiria Mheshimiwa Dkt. Tizeba yeye ni mtu mwenye uelewa mkubwa anaweza akaliwekea mikakati, naomba sasa nirudi pale kwenye kitabu chake kwenye ule ukurasa wake wa 14 na ule wa 110 anapozungumzia mitamba. Watu wengi ni wafugaji na baadhi ni zero grazing. Mifugo ninayoisikia inazungumziwa humu ndani ni yale makundi makubwa ya ng’ombe ya kuswaga. Mimi natoka eneo ambalo halina eneo kubwa, tunafuga ng’ombe mmoja, wawili lakini tunafuga kisayansi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri hii mitamba sasa tupatiwe kule Kilimanjaro tuweze kufuga kisasa. Mitamba hii ikishakuwepo ndani ya nyumba inatupatia mbolea, mbolea hii ndiyo inakuwa kwa ajili ya migomba na kahawa. Hiyo inakuwa kama mgonjwa na uji, migomba mizuri isipopata samadi haiendi. Kwa hiyo, naomba awamu hiyo inayokuja au popote anapoweza kunisaidia niweze kuwapelekea wale wanawake wangu wa Kilimanjaro wafuge kisasa na pia tupate maziwa tutakayopeleka kwenye viwanda, maziwa toshelezi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nienda haraka haraka kwenye ufugaji wa nyuki. Mimi mpaka sasa hivi ukiniuliza nyuki ziko kwenye Misitu au Kilimo sijui lakini naomba leo…
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.