Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Tanga tumeanzisha utaratibu wa kuhamasisha wakulima kila Wilaya kulima kilimo cha mihogo ambacho kitasaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Tunaiomba Serikali itusaidie kuboresha Chuo cha Utafiti Mlingano ili kiweze kupata fedha, wataalam na vifaa kwa ajili ya kusaidia wakulima kulima kilimo chenye tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Muheza na Lushoto ni maarufu kwa kilimo cha matunda, mbogamboga na viungo, mfano, machungwa, ma-apple, maembe, mdalasini, hiliki, pilipili manga na pilipili mtama. Pamoja na wakulima kujitahidi lakini kumekuwa na tatizo kubwa la magonjwa ya mimea na dawa zimekuwa bei ghali kweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali haioni ni wakati muafaka wa kuwasaidia wakulima kwa kupunguza gharama za upatikanaji wa dawa za kuulia wadudu ili wakulima walime kilimo chenye tija? Je, Serikali iko tayari kuwasaidia wakulima hawa kupata masoko ya uhakika kwa kuwa hadi sasa wakulima wa matunda hasa machungwa wanategemea walanguzi kutoka Kenya, kitu ambacho kinasababisha wakulima kutokuwa na maamuzi juu ya bei.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo cha mkonge. Moja ya mikoa ambayo inalima mkonge kwa wingi ni Mkoa wa Tanga na karibu kila wilaya ina shamba au mashamba ya mkonge lakini cha kushangaza mashamba mengi yamegeuka mapori na mengine yamekufa. Serikali haioni kuacha hili zao kupotea ni kuwakosesha wananchi ajira na kipato? Je, Serikali iko tayari kuwanyang’anya wawekezaji na kuwapatia wananchi ambao wako tayari kufufua mashamba hayo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vya samaki. Mkoa wa Tanga umejaliwa kuwa na bandari ambapo wavuvi na wananchi wanaozunguka au waliokaribu wanapata ajira lakini pia wanapata chakula. Wavuvi wamekuwa wakipata usumbufu wa kodi, ukosefu wa masoko ya uhakika na kupelekea kuuza samaki kwa bei ya hasara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo hili la bei linatokana pia na ukosefu wa viwanda vya samaki, hili limekuwa tatizo la muda mrefu. Je, Serikali kupitia Wizara hii ina mpango gani wa kujenga kiwanda cha kuchakata minofu ya samaki ili wavuvi wawe na uhakika wa kipato?