Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Omari Mohamed Kigua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri na watumishi wote wa Wizara kwa hotuba ya Wizara yao ambayo inaonesha mwelekeo wa kutatua changamoto za wakulima wa nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii bila kilimo cha kisasa, chenye kutumia mbolea na zana za kisasa, bado ndoto ya kuzalisha mazao mengi haitafanikiwa. Niipongeze Wizara, katika hotuba hii inaonesha mwelekeo wa kuleta ukombozi kwa mkulima, kwa mfano uagizaji wa mbolea kwa pamoja (bulk). Eneo hili lilisababisha wananchi wengi kushindwa kuzalisha mazao yenye tija kwa sababu mbolea ilikuwa juu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri awe makini sana katika mpango huu, kwamba wale watakaopewa majukumu haya wawe watu makini na wazalendo wa dhati kwa sababu bado baadhi yao wanaweza kutumia nafasi hiyo vibaya. Kwa kuwa mpango huu ni mpya changamoto nyingi zitajitokeza, naomba tu uwekwe utaratibu wa kufuatilia utekelezaji wa mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo napenda kuchangia na ambalo naona Wizara haijalipa uzito ni kilimo cha umwagiliaji kwani yapo maeneo mengi nchini yanapata mvua za kutosha na yana mabonde mengi ambapo yangetumika vizuri nchi hii isingepata tatizo la njaa. Mvua zinanyesha maeneo mengi na maji yote yanaishia baharini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano katika Jimbo la Kilindi, Kata za Kilwa, Kilindi Asilia, Masagulu, Kibirashi pamoja na Mgera. Maeneo yote haya yana mabonde ambapo hata kwa shughuli za kilimo cha mbogamboga kingefaa pia. Tatizo Wizara haina mpango mkakati ili kuwasaidia wananchi kwa kutoa elimu, zana na hata mikopo ambayo ingeweza kusaidia katika kuboresha maisha yao kwa shughuli za kilimo.

Niombe Wizara hii, pamoja na mipango yake mizuri, wakati umefika Benki ya Kilimo isaidie sasa wananchi wakulima wa nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo napenda kuchangia ni eneo la Mkoa wa Tanga na maeneo mengine ambayo yana fursa za kulima mazao ya matunda. Mkoa wa Tanga ni miongoni mwa mikoa michache nchini ambayo inazalisha matunda lakini uzalishaji wake umekuwa hauna faida kwa sababu wanachopata, kwa maana ya bei, ni ndogo kwa sababu tu Wizara haina utaratibu mzuri wa kuwatafutia soko la uhakika wananchi hawa. Nishukuru, pengine kwa mpango wa Serikali wa kujenga tena viwanda, unaweza kurudisha tena imani na uchumi wa wananchi wetu. Niombe Serikali kupitia Wizara hii iwaangalie wananchi kutoka kwenye maeneo yenye fursa za kilimo kama ilivyo Mkoa wa Tanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia migogoro ya wakulima na wafugaji; je, zoezi la Wizara tatu au nne la kutaka kutatua migogoro ya wananchi wetu limefikia wapi? Nchi hii inawahitaji wakulima na wafugaji, hivi kwa nini jamii hizi mbili hazipatani? Tatizo ni upimaji wa maeneo; hivyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri ashirikiane na TAMISEMI na Wizara ya Ardhi kuhakikisha maeneo ya kilimo yanatengwa na ya wafugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inajitokeza mara kwa mara wafugaji wanaingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima lakini tatizo lingine la wakulima kupanua maeneo ya kulima kwenye maeneo ya wafugaji, tatizo hili halitakwisha kama Serikali haitapima maeneo ya ufugaji na kilimo, huu ndio mwarobaini pekee. Kwa mfano maeneo ya Wilaya ya Kilindi, Rufiji na Mkoa wa Morogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.