Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kwa kuwapongeza Mawaziri wa Wizara hii, Dkt. Charles Tizeba pamoja na Mheshimiwa William Olenasha pamoja na Makatibu wa Wizara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nijielekeze moja kwa moja kutoa mchango wangu katika Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambayo ni Wizara nyeti inayotegemewa na Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kagera tumebarikiwa kwa kuwa na ardhi nzuri yenye rutuba na hali ya hewa nzuri yenye mvua za kutosha. Mkoa wa Kagera kilimo kimekuwa cha kusuasua kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo teknolojia duni pamoja na pembejeo kutokufika kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkoani kumekuwa na miundombinu mibovu ya kusafirisha mazao kutoka shambani hadi kwenye masoko. Naomba Wizara husika iweze kuwasiliana na Wizara ya Uchukuzi ili waweze kutuwekea miundombinu mizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, magonjwa ya mimea kwa mazao ya chakula yamekuwa yakiongezeka sana. Katika mkoa wa Kagera zao la mgomba linalolimwa na kutegemewa na wananchi wa Mkoa huo linashambuliwa na ugonjwa wa mnyauko ambao unatutesa sana kwa sababu ndizi ndicho chakula kikuu kwa mkoa wetu. Hivyo naomba Serikali itusaidie kutokomeza ugonjwa huo ili wananchi wa Mkoa wa Kagera waweze kunufaika na zao hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkoa wangu wa Kagera umebarikiwa kwa kuwa na mazao ya biashara kama vile kahawa na miwa. Kwenye zao la kahawa tuna changamoto ya masoko kiasi kwamba inasababisha wananchi kwenda kutafuta soko nchi jirani. Naiomba Serikali iweze kutatua changamoto hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa miwa napenda kuishauri Serikali kuweka mashamba darasa kwa wakulima wadogo wadogo ili waweze kuungana na wakulima wakubwa na hivyo waweze kupata utaalamu wa kulima kisasa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina imani kama Serikali na Wizara ya Kilimo wakiweza kuutumia Mkoa wa Kagera nina uhakika unaweza kuzalisha sukari ya kutosha nchini kwetu na kuuza nje ya nchi. Mawakala wa pembejeo za kilimo mpaka sasa wameendelea kupigwa dana dana kwa kutolipwa fedha zao. Tukumbuke mawakala wengi walichukua fedha za mikopo kwenye benki na sehemu nyingine kama dhamana hali iliyosababisha wengine kupigiwa minada nyumba zao na hivyo kusababisha wengine kupoteza maisha kwa ajili ya pressure (blood pressure).
Mheshimiwa Mwenyekiti, mawakala wote nchi nzima wanaidai Wizara ya Kilimo shilingi bilioni 64.4 ambapo Wizara inawapiga dana dana na hawajui hatima ya deni lao, japo Wizara ya Kilimo inasema bado ina hakiki uhalali wa deni hilo. Basi ni vyema Serikali ikaanza kuwalipa wale iliyojiridhisha kuwa wanastahili kulipwa na wale ambao bado hawajajiridhisha Wizara iangalie namna ya kuwasaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, usalama kwa wavuvi haupo vizuri wakiwa ziwani au baharini, wanatekwa na majambazi, wananyang’anywa samaki na wengine kupoteza maisha. Ninaomba Wizara waweke doria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wavuvi wasitozwe leseni zaidi ya mara mbili na kwa kweli ninaomba Wizara iwaangalie kwa jicho la huruma hawa wavuvi wanaoingiza nyavu ambazo hazifai. Itawasaidia wavuvi kupata nyavu zinazokubalika, za kiwango kuliko kuchukua mbovu ambazo zinawaletea hasara zikishachomwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.