Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Dr. Charles John Tizeba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buchosa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha tena kukutana jioni hii tukiwa na afya njema thabiti kabisa, ili tujadili yale ambayo yamezungumzwa kwa kipindi cha takribani siku tatu wakati Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakijadili mapendekezo ya mapato na matumizi ya Wizara yetu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utangulizi nimshukuru sana Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo Mifugo na Maji Mheshimiwa Dkt. Mary Michael Nagu, Mbunge wa Hanang, Wajumbe wote wa Kamati yetu, vilevile nimshukuru Mheshimiwa Cecilia Paresso Mbunge wa Viti maalum aliyewasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwa niaba ya Msemaji Rasmi wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi Dkt. Emmaculate Sware. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, niwashukuru Wabunge wote waliochangia katika hoja hii ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na kwa kutambua umuhimu mkubwa wa hoja hii Wabunge wengi wamejitokeza kuchangia, kutoa maoni na ushauri hali ambayo binafsi imenipa faraja kubwa kwani michango hiyo itasaidia katika utekelezaji wa mikakati ya kuendeleza sekta ya kilimo mifugo na uvuvi na ni ushahidi tosha kwamba kilimo mifugo na uvuvi ni sekta muhimu kwa ustawi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla Wabunge takribani 134 wamechangia kwa kauli na maandishi wakati tukijadili makadirio ya matumizi ya Wizara yangu. Kati ya hao Wabunge 87 walichangia kwa kauli na Wabunge 47 kwa maandishi. Kwa hali hiyo Wabunge hawa ni wengi sana na hivyo kwa dakika hizi arobaini sidhani kama naweza kuwataja wote na kujibu hoja ya kila mmoja, haitakuwa rahisi kwangu kufanya hivyo na kwa hivyo ntajitahidi kujibu kwa ujumla mambo makubwa yaliyojitokeza katika michango hii. Napenda pia niwahakikishie kwamba Waheshimiwa Wabunge yote mliyojadili mliyochangia, mliyohoji tutajitahidi kuyajibu kwa maandishi na kuwapatia kabla hatujamaliza mkutano huu wa Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo, naomba sasa uniruhusu nijibu baadhi ya hoja zilizojitokeza katika mjadala wa hotuba kama ifuatavyo; Nitaanza na hoja ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji halafu nitazungumzia machache yaliyojitokeza katika hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge karibu wote waliochangia wamezungumzia jambo hili la bajeti ndogo ya Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi. bajeti ya Sekta hii haiko yote katika Wizara yangu ili labda ndio nianze kwanza nalo ili tuelewane vizuri Waheshimiwa Wabunge, bajeti kubwa iko maeneo mengine nje ya hii Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara mtambuka zinazojihusisha na mambo ya kilimo kubwa kabisa ya kwanza ni Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Kule mipango yote karibia ya utekelezaji wa shughuli za kilimo inafanyikia TAMISEMI katika Halmashauri zetu Waheshimiwa Wabunge, Wizara inajihusisha zaidi na sera na miongozo ya Kitaifa, lakini utekelezaji unafanyika kule kwenye grassroot ambako haya mambo yanasimamiwa na Wizara ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ziko Wizara zingine kwa mfano Wizara ya Miundombinu, Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, hawa nao wanafanya kazi ambazo zinahusu kilimo ingawa sio moja kwa moja. Kwa hivyo, ukilichukulia katika ujumla huo mpana utaona kwamba sekta hizi tatu kilimo mifugo na uvuvi siyo kwamba zimepata bajeti ndogo kihivyo isipokuwa tu ile inayoonekana katika Wizara yetu ya Kilimo ndiyo kwa mtazamo unaweza ukaona kwamba ni bajeti kidogo. Halmashauri jumla ya bajeti yake inayohusu sekta hizi tatu ni kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hili zipo taasisi zetu karibia 11 ama 12 ambazo zinakusanya maduhuli ni taasisi za umma na zinajihusisha na mambo haya haya ya kilimo, mifugo na uvuvi ambazo maduhuli yale hayaji katika bajeti kuu ya Serikali wana-retain na kutumia moja kwa moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uchache, niseme tu hizi taasisi hizi zinakusanya na kutumia katika sekta za kilimo jumla ya shilingi karibia bilioni 260. Hizi ukiziongeza katika ile bajeti ya kwetu ya moja kwa moja kwa sababu ni taasisi ambazo ziko chini ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, ukiziongeza hizi utaona kwamba kutoka kwenye karibu 400 ile tunakwenda kwenye 600.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu kuna fedha nyingi ambayo inaingia katika miradi ya kilimo, mifugo na uvuvi nje kabisa ya utaratibu wa bajeti ya Serikali. Ziko taasisi nyingi za wabia wetu wa maendeleo ambao wanachangia sana katika kilimo lakini siyo kupitia mfumo wa bajeti ya Serikali. Hata hivyo, jambo la kuzingatia tu ni kwamba hawa wote hawa ushiriki wao katika miradi mbalimbali wanayoiendesha unakuwa na baraka za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni approach tu ndiyo ina- differ, kule kwenye afya wana basket wanayochangia, kwa hivyo zinaonekana zimepitia kwenye mfumo wetu wa bajeti wa Serikali, lakini kwenye kilimo wanakwenda wame-opt kwenda na kwa sababu wana complement kazi inayofanywa na Serikali hatuna sababu ya kufinyana nao. Kwa hivyo, tunawaacha watekeleze hayo majukumu ambayo otherwise ingebidi Serikali itenge bajeti hapa kwenda kufanya hayo majukumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano mdogo tu, katika mwaka 2015/2016, kwa ujumla wadau wetu wa maendeleo walichangia trilioni moja na bilioni 730 katika kilimo direct, wakati bajeti yetu ya Serikali kwa ujumla ilikuwa trilioni 1.001, wenzetu wakachangia trilioni 1.73; ukizijumlisha hizi ni karibia trilioni 2.7, ni fedha nyingi kuliko Wizara nyingine yoyote iliyopata mchango wa namna hiyo katika bajeti ya mwaka uliopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka tu kusema kwa maneno haya ni kwamba fedha inayokuwa directed kwenye kilimo ni nyingi, katika mwaka huu wa fedha tunaoendelea nao mpaka hapa ninapozungumza leo commitment za fedha hizi zinaendelea kutoka, lakini mpaka ninavyozungumza sasa hivi fedha kutoka kwa wadau wetu wengine nje ya mfumo wa bajeti wamesha-disburse karibu bilioni 400. Kwa hivyo, hizi ni fedha ambazo zimeingia kwenye kilimo kupitia programs mbalimbali ambazo wadau wetu tunashirikiana nao katika kukuza na kuimarisha kilimo chetu hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge tusipate wasiwasi kwamba kilimo kinakuwa under funded na kadhalika. Nasema kilimo ni kipaumbele hakuna asiyejua na mmesema vizuri hapa kwamba bila kilimo viwanda na nini vitakuwa tabu sana ku-achieve, yes itakuwa vigumu sana ku-achieve! Hata hivyo, hata ukiwa na priority maana yake ni kwamba utakataa misaada, utakataa ziada eti kwa sababu jambo hilo unaloshughulikia wewe kwako ni kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano mdogo. Taifa la Israel kipaumbele namba moja chao ni usalama, security of that country is priority number one, ulinzi bajeti yao ya ulinzi pamoja na kwamba ndiyo concern, ndiyo priority number one Taifa la Israel, bajeti yao ya ulinzi wanapata msaada kutoka Marekani. Mwaka jana tu wamepata msaada wa bilioni 38 dola wakati wao bajeti yao ya ndani ilikuwa imetenga bilioni 4.6. Hata hivyo, hiyo haimaanishi kwamba wameondokana na kufanya suala la ulinzi kuwa kipaumbele namba moja. Kwa hivyo, hata sisi wakati tuna bajeti tunaangalia pia kwamba wenzetu wanaotuunga mkono katika kilimo commitment yao ni kiasi gani ili tuweze kufanya rational distribution ya resource tuliyonayo ya ndani. Kwa hivyo, niwaombe Waheshimiwa Wabunge hili suala lisitusumbue sana kwamba kwa nini asilimia tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nielezee hapa asilimia tatu ambayo inasemwa kwamba kwa mwaka mzima bajeti ya Fungu 43 iliyotolewa ni asilimia 3.8. Ni kweli mpaka tunaandika hivi vitabu pesa iliyokuwa imetolea ni shilingi bilioni kama 3.4 ambayo ukiipigia hesabu inakuwa asilimia tatu, lakini ni asilimia tatu yaa shilingi bilioni 101 ambayo ilikuwa imetengwa kwa ajili ya mradi mmoja tu, mradi wa kujenga vihenge (silos) na hivi tunavyozungumza majadiliano almost yamekamilika na Serikali ya Poland ambako hizi fedha sasa zitapatikana dola karibu milioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa hivyo vihenge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, huenda wakati Waziri wa fedha anakuja kusoma bajeti yake hapa performance ya hiyo miradi ya maendeleo kwenye bajeti commitment ya Serikali inaweza kuwa imeshafika kwenye asilimia 98. Ndugu zangu ile asilimia tatu inayoonekana kwa sababu tusingesema uwongo, mchakato ulikuwa haujakamilika, lakini tuna hakika sasa kila lililohitajika ili tukamilishe upatikanaji wa hizo fedha kutoka Serikali ya Poland tumekwishafanya, zitapatikana, vihenge vitajengwa na kwa hivyo utekelezaji wa bajeti yetu ya maendeleo utakuwa umekwenda kwenye asilimia kubwa sana kuliko inavyoonekana kwenye maandishi yetu sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo limezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge kwa hisia ni hili suala la tozo tulizoziondoa. Nimesikitika kweli jana kuona baada ya kelele zote za wananchi wa nchi hii kuhusu tozo, kero zinazowasababishia kutonufaika na jitihada zao, baadhi ya wenzetu hapa ndani wamesimama wakibeza eti kwamba hili tulilolifanya ni jambo baya halina manufaa kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi siyo msemaji mzuri sana wa exchange hizi za mambo ya humu ndani, lakini itoshe tu kusema kwamba mambo ambayo ni serious kama haya tunatakiwa kuacha hizi politics za ajabu. Hapa tunazungumzia maisha na well being ya Watanzania. Watu wanalalamika anapeleka ng’ombe mnadani hajauza, anatozwa kodi ya makanyagio, halafu sisi tukae tuache kodi ya hivyo eti kwa sababu kuna mtu hapa anadhani kwamba tuko tunatafuta sifa, hatutafuti sifa! Sisi tunashughulikia matatizo ya wananchi, matatizo ya kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikia mdogo wangu Mheshimiwa David Silinde asubuhi hapa, anasema kodi hizi zimewalenga middle men hazijawalenga wakulima, hivi Tanzania hizi kodi tunaziweka kwa ubaguzi? Hizi kodi zinawaathiri wote katika mnyororo wa thamani, kodi hizi zinamuathiri kila mmoja kwenye mnyororo wa thamani. Mkulima akilima kama hakuna mnunuzi kilimo chake hakina manufaa, mnunuzi akiwapo bila mkulima, uchuuzi wake hauna manufaa, wote wanategemeana. Kama watu wana mazao lakini hakuna msindikaji, mazao yale yatapoteza thamani. Kwa hivyo, tulichokifanya tumeangalia mnyororo mzima wa thamani na namna hizi kodi zinavyowa-affect mmoja mmoja kwenye mnyororo huo wa thamani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuondosha kwa hizi kodi hakukulenga kundi moja tu la Watanzania, kumelenga Watanzania wote ambao wanakuwa affected na hizi kodi, wafanyabiashara, wakulima wasindikaji na wengine. Nitatoa mfano mdogo ili tuwe na ufahamu unaofanana. Kwenye tumbaku au tuseme kwenye mbegu ili mfanyabiashara mzalishaji wa mbegu aweze kuzalisha mbegu alitakiwa kuwa na mtaji wa tozo tu wa milioni 60, dola 20,000 kwa ajili ya kusajiliwa kama mzalishaji wa mbegu na dola 10,000 za kusajili mbegu anayotaka kuzalisha hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa huyu ni mfanyabiashara anazalisha mbegu auze kwa wakulima, ukimuachia hii kodi ibaki maana yake mbegu atakayozalisha lazima aweke ndani yake hizi gharama. Akiweka ndani yake hizi gharama bei ya mbegu inapanda, bei ya mbegu ikipanda
anayeathirika na kushindwa kuinunua ni mkulima. Kwa hivyo, tunalazimika kuondoa hizo kodi kwa yule ili finally mkulima apate mbegu kwa bei rahisi aongeze uzalishaji, akiongeza uzalishaji Halmashauri zetu zinatoza cess na tunapanga mipango mingine ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe tu ndugu zangu siyo kwamba watu walilala wakaamka usingizini wakaanza kufuta moja, mbili, tatu, nne, tano, sita, saba. Ndiyo maana kodi ambazo tumeona zina uhusiano wa moja kwa moja na kuongeza uzalishaji, kusimamia mazao yaendelee kuwepo na kadhalika hizo hatujazigusa, tumeziacha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mwingine mdogo, kwamba tumeondoa eti kodi ya vifungashio vya korosho, kwa hivyo hili jambo litawanufaisha wanaoingiza magunia yale ndani. Jamani wanaoingiza hayo magunia ni Vyama vya Msingi vya Wakulima, korosho ikitoka kule kwenye primary societies haiendi kwenye malori kama mchanga imebebwa, inawekwa kwenye hivyo vifungashio inaingizwa kwenye ghala na hapo kila mtu ndiyo anajua, hiii ya kwangu, hii ya nani na nani by weight and everything.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoondoa hii tozo maana yake ni kwamba hawa wakulima waliokuwa wanalazimika kulipa kodi kwa ajili ya magunia yale sasa hawatalipa hiyo hela inabaki kwao. Nilikuwa napiga hesabu, kwa hilo moja tu la tozo ya magunia saving itakayokuwepo kwa wakulima wa korosho msimu unaokuja, bilioni 11. Sasa hizi siyo hela ndogo zikibaki kwa wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, tumeondoa VAT kwenye mashudu ya pamba. Mtu anaweza akadhani kwamba tumewasaidia ginner’s siyo kweli! Ginners hawa katika mjengeko wa bei wanayonunua pamba kwa wakulima wanaweka mle ile VAT kama cost. Kwa hivyo, bei ya pamba kama ilikuwa iwe Sh.1,100/= kwa kilo moja wanaondoa shilingi karibu mia moja wanasema hii tutarudisha Serikalini kama kodi. Sasa hivi tunachofanya hiyo ikiondoka maana yake hiyo mia moja itabaki kwa mkulima, itamjengea uwezo wa kulima zaidi, itamjengea uwezo wa kununua dawa na uwezo wa kufanya nini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo niombe jamani ndugu zangu, haya mambo serious namna hii, tusi-relate nayo kimzaha mzaha kama tulivyoona wenzetu wanajaribu kufanya hapa ndani. Nawashukuru sana wote ambao mmetuunga mkono kwenye hili jambo, tutakuwa makini, tutaangalia impact yake. Haya ni mambo siyo static, tutaangalia impact yake katika tasnia nzima, yale yatakayohitaji adjustment tutafanya adjustment. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hili suala la ununuzi wa pamoja, uingizaji wa pamoja wa mbolea. Nashukuru sana kwamba Bunge limetuunga mkono Serikali katika hili jambo nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge. Maangalizo yenu yote kabisa tumeyachukua, yako maangalizo ambayo mmeyasema ni ya msingi tumeyachukua. Tutahakikisha wakati tunatekeleza hili jambo tunakuwa makini na hayo maeneo ambayo mmetupa angalizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ni la kuhujumiwa kwa sababu wako ambao watapoteza katika huu mchakato na kwa hivyo kama watakuwa wanapoteza wakipata uwezekano wa kuzuia tusifanikiwe watajaribu na tumeona attempt ilikuwepo na wote ninyi ni mashahidi. Kwa hivyo hayo maeneo ya hivyo tutakuwa makini nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwatoe wasiwasi wakulima wa nchi hii kwamba fall back position sijui niisemeje kwa Kiswahili. Kwamba jambo hili likipata tatizo lolote kwa mfano, namna ya kufikisha mbolea kwa wananchi kwa wakati kwa msimu huu tunayo. Nawaomba sana ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge mtu asidhani kwamba tunakwenda kwenye jambo blindly kwamba ikitokea something unforeseen basi sisi ndiyo tutakuwa tumeporomoka hatujui la kufanya, wakulima wamekosa mbolea na kadhalika, hapana! Fallback position ipo, siyo jambo la mjadala wa hapa ndani, lakini naomba tu muamini kwamba fallback position ipo.

Mheshimiwa Mweyekiti, ndiyo maana tumeanza kwa uangalifu na aina mbili tu za mbolea. Tumeanza na aina mbili kwa makusudi kabisa, sio kwa bahati mbaya, kwa makusudi! Kwamba uwezekano wa kuli-perfect hil jambo asilimia 100 tunasema who knows! Kitu chochote kinaweza kutokea huko tunakoagiza na nini, sasa tunafanyaje; kwa hivyo tumejiwekea na sisi hizo tahadhari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutumia nafasi hii kwa ruhusa yako kuwaonya hao ambao wanajaribu kutuvuta shati. Sisi dhamira yetu ni kuhakikisha gharama za uzalishaji katika kilimo zinashuka, watu hawaoni faida ya kulima kwa sababu margins zinakuwa ndogo sana, mtu anahangaika na tumbaku miezi tisa faida anayokuja kupata two, three percent. Sasa hiki tunachokifanya tunahangaika angalau hiyo faida iongezeke basi kutoka kwenye hizo three percent ifike angalau kwenye ten, fifteen percent. Tutalisimamia kwelikweli hili jambo. Kanuni hizi ziko strict kweli kweli, mtu yeyote akiingia hapo katikati atakiona cha mtema kuni. (Makofi

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwahamasishe Watanzania kwamba kilimo sasa hivi kitalipa. Wale ambao wamekuwa wanadhani kwamba kilimo hakitalipa, nataka niwaambie leo kwamba kilimo kitalipa, awe ni mkulima, awe ni mfanyakazi wa kuajiriwa, ardhi Tanzania ipo, hebu twende tulime. Tukilima kwanza unakuwa umejihakikishia kama ni umelima mazao ya chakula utakuwa na chakula chako mwenyewe hulazimiki kwenda sokoni, kama utakuwa ni mkulima utapata chakula chako lakini utalazimika kupeleka ziada sokoni. Kwa hivyo tunashusha, tunapunguza hizi gharama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uki-combine measure hii ya bulk purchase ya pamoja na hizi tozo na kodi mbalimbali ambazo tunaondoa kwenye pembejeo kwa vyovyote vile mbolea itashuka bei na huenda katika bajeti yetu hii hapa tunayoomba iko fedha ambayo tumeiomba Bunge lituidhinishie kwa ajili ya ruzuku ya pembejeo. Tukifanya vizuri mwaka huu katika huu mfumo yawezekana kabisa mwaka kesho Serikali ikaja hapa bila maombi ya ruzuku kwenye pembejeo kwa sababu pembejeo itakuwa sasa ni rahisi inapatikana na kila Mtanzania anaweza kumudu kununua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo limezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge wengi ni mbegu. Ni kweli kwamba utoshelevu wetu wa mbegu inayozalishwa hapa nchini bado uko chini, tuko asilimia 35 ya mahitaji. Hili jambo niliongelee kwa kujibu pia hoja ya kwamba hatuweki malengo yanayopimika katika mipango yetu. Jamani, tunayo mipango ya muda wa kati na muda mrefu, mipango ya muda wa kati tunaitekeleza kupitia bajeti za mwaka mmoja mmoja halafu finally tunakuwa na mpango wa muda mrefu wa miaka mitano au kumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuondokane na hali hii ya udhaifu wa upatikanaji wa mbegu bora hapa nchini kulikuwa na tatizo kubwa sana la kisheria. Utaratibu tuliokuwa nao ulikuwa haumwezeshi mzalishaji wa mbegu kuzalisha hapa nchini aina nyingi za mbegu kwa tija au akapata faida mwisho wa siku. Faida hiyo ilikuwa inamezwa katika sheria na kanuni tulizokuwa nazo. Kwa hivyo, hatua ya kwanza siyo kuanzisha mashamba, hatua ya kwanza lazima iwe ku-adress tatizo linalozaa mengine (root cause).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo tumeanza na hilo, tumeanza na kurekebisha sheria na kanuni za mbegu ili sasa tukishaweka mazingira mazuri kwa wazalishaji waingie kwenye uzalishaji kwa sababu suala la uzalishaji yeyote atakayeona sasa hiyo fursa iko nzuri kwake anaingia kwenye uzalishaji. Tutoke kwenye huu mtindo ambao mbegu inazalishwa Kenya, Zambia tunakuja kuuziwa Watanzania kama vile sisi hatuna ardhi hapa ya kuzalisha mbegu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo tumeanza na sheria. Tumefuta tozo za ovyo ovyo zilizokuwako kwenye uzalishaji wa mbegu, tumepunguza masharti ya muda na mlolongo ule tumeu-short circuit wa kupata vibali ili mtu uanze uzalishaji wa mbegu. Kwa hivyo, kwa combination ya hizi measures, tuna hakika mwaka kesho tutaona investment zaidi kwenye suala la uzalishaji wa mbegu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, iko mbegu moja imepigiwa kelele hapa ndani, naomba na yenyewe niitolee ufafanuzi, mbegu ya pamba UK91 ni ya tangu mwaka 1991, leo ina miaka 26 imepitwa na wakati, imechoka na mimi nasema ni kweli. Yaani aliye-observe namna hiyo ame-observe vizuri kabisa UK91 ni mbegu ya zamani, uzalishaji wake umeshuka chini lakini hata uhimilivu wa visumbufu wa hii mbegu sasa na wenyewe uko chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekubaliana ndani ya Serikali na tumeweka proramu ambayo tumeanza kuitekeleza mwaka huu na tumejiwekea lengo, wale wanaosema hatuweki malengo, tunaweka! Tumejiwekea lengo kwamba inapofika msimu wa kilimo wa 2019 tutakuwa na utoshelevu wa mbegu mpya aina ya UKM08 kwa nchi nzima. Hatutakubali tena mkulima yeyote wa pamba Tanzania apande pamba ya UK91.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu peke yake tumepanda hectares 80,000 katika Wilaya tatu, Wilaya ya Igunga, Wilaya ya Nzega na Wilaya ya Meatu. Tumepanda hectares 80,000 za UKM08 na tuna-control isije ika-mix na UK91 na tutapata kama tani 8,000 ya mbegu na baada ya hapo katika msimu unaofuata wa 2018 tukipanda mbegu ile tani 8,000 tutakwenda kwenye tani 14,000/15,000 ambayo ndiyo mahitaji ya nchi nzima kwenye aina hii ya mbegu ya UKM08. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo ndugu zangu wakulima wa pamba naomba niwahakikishie tu kwamba, hili jambo tutalisimamia kikamilifu na mwaka 2018 wakulima wote wa pamba tunatarajia kabisa watakuwa na mbegu mpya ya UKM08. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wako wafanyabiashara wanajaribu kuingiza mbegu feki, dawa feki na kadhalika.

Jambo la kusema hapa kwa kifupi tu ni kwamba ni lazima tuimarishe usimamizi, haya mambo ya feki na nini, dawa yake ni usimamizi. Tunapoimarisha usimamizi maana yake hatutoi mwanya kwa mtu kuchomekea mbegu au dawa ambayo sio sahihi. Tumechukua hatua, stern measures kweli kweli kwa Watendaji wa Serikali ambao wamekuwa wana-collude na wafanyabiashara kuingiza mbegu na dawa mbaya ambazo zinawaathiri wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikiliza kwa makini sana Mheshimiwa Maige akilalamikia wale waliopewa mbegu ya pamba miaka mitatau iliyopita wakapanda haikuota halafu mamlaka mbalimbali za Serikali zikaanza kutupiana mpira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo kwa sababu lina utaalam ndani yake huwezi kulirukia kusema kwamba ni TOSK au TPRI au ni nani waliotufanyia foul katika hili. Kwa hivyo, tutakapojiridhisha kwamba ni nani hasa culprit katika hili tutamchukulia hatua tu. Hata kama uwezo wake wa kifedha utakuwa hauwezi kuwa-compensate wale wakulima lakini tutamfunga, tutamfanyia chochote ili iwe fundisho kwa wengine kwamba uki-temper na mambo ya wananchi Serikali ipo itakuona na itakuchukulia hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la uvuvi wa bahari kuu na mchango wa uvuvi kwa ujumla. Mheshimiwa Abdallah Ulega amesema kwa maneno mazuri sana kwamba blue economy Tanzania ni kama haipo, haipo kwa sababu tulikuwa na kanuni legelege. Waheshimiwa Wabunge mtakumbuka, alitumwa Mheshimiwa Mama Tibaijuka kwenda UN kwenda kuomba hiyo EZ tukafanikiwa kwenye hilo jambo, lakini tangu tupate hiyo EZ nchi kama nchi kwa mwaka tumekuwa tunaambulia shilingi bilioni sita. Huu udhaifu ulikuwa katika kanuni tulizotunga wenyewe. Nchi zote zinazofanya uvuvi wa bahari kuu, majirani zetu hawa wamekuwa wanatushangaa, hivi Tanzania hawa wakoje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nilikuwa nafanya majadiliano na kampuni kutoka Spain kampuni 29 zinazofanya uvuvi bahari kuu walikuja kuniona wanahoji hizi kanuni kwa nini ziko hivi. Siku hiyo tunafanya hayo mazungumzo, South Africa walikuwa tempted kumleta Waziri wao wa Uvuvi aje kusikiliza kama tuta-yield/bow kwenye hoja za hawa watu. Mimi nikamwambia wewe kaa tu huko, tuko imara, tunajua tulichokifanya. Tume-research, tumeangalia best practice ya wenzetu wanafanyaje na sisi tumeji-peg katika mambo ambayo yanatekelezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwambia Mheshimiwa Ahmed Juma Ngwali by catch siyo mali ya aliyevua, mvuvi anaomba license ya aina ya samaki, tunampa license ya kuvuna huyo jodari basi, akikamata samaki mwingine huyo hakuwa ameruhusiwa na wala hajakata license kuvuna yule na ile ni rasilimali ya Watanzania. Tunachosema kwenye Kanuni zetu, hiyo rasilimali uliyokamata ambayo siyo ya kwako ambayo tumekuruhusu kuvuna leta. Tunazungumza modality ya compensation ya mafuta na kadhalika, lakini tumeweka suala la uhakiki wa volumes au tonnage wanazovuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zamani mtu akivua samaki kule akishakata license ile dola 50,000 miezi sita, anavua kiasi chochote atakachopata sisi hatuambulii chochote. Tulichokomea ni hiyo dola 50,000. Sasa hivi tumesema hii nayo ni maliasili kama zingine, zitalipiwa pia mrabaha na kwa maana hiyo tutapeleka observers wetu, wakajue bwana huyu kavuna kiasi gani kwa hivyo mrabaha wetu kiasi gani. Katika hizo alizovuna kwenda nazo huko anakoenda sawa, zile zisizostahili ngapi tuletee hapa Watanzania wapate samaki kwa bei nafuu tuongeze lishe kwa watu wetu na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, kuna multiply effect kubwa sana. Meli zile zitakapoleta ile by catch watakuja kununua chakula, kuweka maji, wataweka mafuta, watalipia sijui nini. Kwa hivyo, uchumi utanufaika siyo kwa samaki tu lakini uchumi utanufaika hata kwa mambo mengine zaidi ya hao samaki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeweka sharti la kuwa na Mabaharia Watanzania. Activity hii inafanyika ndani ya eneo letu la nchi, si ndiyo? Ni kama mtu aje aweke kiwanda hapa halafu asilimia 100 ya wafanyakazi ni watu wa nje tutakubaliana na jambo la hivyo? Kwa hivyo ile meli inapokuja kufanya activity ya mwaka mzima Tanzania, tunasema na Watanzania wa-participate lazima kuwe na local content Mheshimiwa Ngwali! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wako vijana hapa wanasoma vyuo vyetu hapa wanamaliza halafu wanatushangaa tu, kwamba watu wanatoka huko watokao, China, Indonesia na Taiwan wanakuja wanafanya shughuli ya uvuvi hapa, Tanzania hakuna hata Baharia mmoja huko ndani, hakuna kila kitu tumewaacha wanasomba wanavyotaka, mimi nasema jamani niacheni jamani niacheni nishughulikie hili jambo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wakati akiwa Waziri wa Uvuvi alikamata tani 290 tu ya meli iliyokuwa inafanya uvuvi haramu pale. Tani ile 290 ilisambaa Magereza yote Dar es Salaam, Morogoro mpaka Tanga. Sasa kwa wastani hesabu na wataalam wetu wanasema, ukivua tani moja at least asilimia 20 ni by catch, wanakamata kule zaidi ya tani 20,000, tani elfu ngapi. Kwa hivyo, tunatarajia tu hata ile by catch itakuja hapa maelfu ya tani.

WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.